Mwaka wa 1961 tulipata uhuru wa bendera toka kwa wakoloni wa Uingereza, Wakati huo tukiitwa Tanganyika chini ya chama cha TANU na Mwenyekiti wake akiwa Mwl. Julus Nyerere. Kwa wale wanaokumbuka taifa lilitangaza vita dhidi ya maadui watatu, umasikini, ujinga, maradhi.
Miaka zaidi ya 45 ya uongozi wa TANU na sasa CCM bado hali ya nchi yetu ni mbaya sana kwa walio wengi. Wale maadui watatu bado wana tamba, yaani umasikini, ujinga, na maradhi. Na kama hiyo haitoshi hivi sasa tuna adui wa nne aitwe rushwa/ufisadi
Wengi wetu tumejiuliza tatizo liko wapi? Mbona hali inazidi kuwa mbaya? Bila shaka kuna waliokata tamaa na kuamini kwamba kamwe hatutaweza kuiondoa Tanzania katika umasikini uliokithiri.
Serikali iliyoko madarakani imeanda mikakati na sera nyingi za kupambana na hao maadui wa nne, lakini mwenye macho haambiwi tazama!
Miaka ya sitini tulitangaziwa Azimio la Arusha kama silaha ya kumkomboa mtanzania, watu wengi wakati huo walilipokea Azimio kwa matumaini makubwa, leo wote tunajua hatima ya Azimio ilikuwa nini wakubwa walipokutana kule Zanzibara; walilitosa Azimio la Arusha baharini!
Wakubwa hawa wakaja na sera mpya ya uwekezaji kama muarubaini wa matatizo ya Tanzania. Toka wakati huo wamezunguka dunia nzima kuwakaribisha wawekezaji waje kumkomboa mtanzania kwani hawa viongozi wetu kama wazazi wetu ndio haswa wanaojua dawa ya matatizo yetu.!
Leo (2009) ukizunguka nchi nzima utasikia kilio cha jinsi wageni walivyo chukua nchi na wenye nchi wakibaki kulia tu. Ukiuliza unajibiwa na hawa wakubwa wetu wanaotupenda sana kwamba hao wageni ni wawekezaji na bila wao tutabaki na umasikini wetu.!
Mtanzania amekata tamaa, aliikimbilia CCM akiamini itamkomboa lakini wapi, na anapojaribu kugeukia vyama vya upinzani anambiwa hakuna mtu mwenye uwezo huko, hao wapinzani ni wababaishaji tu. Sasa aende kwa nani?
Naomba niseme hivi na kuwakumbusha watanzania wenzangu maneno yaliyopo katika Azimio la Arusha, naamini maneno haya bado yana maana kubwa sana katika kumkomboa mtanzania hata leo:
“Tumeonewa kiasi cha kutosha, tumenyonywa kiasi cha kutosha, na tumepuuzwa kiasi cha kutosha, unyonge wetu ndio uliotufanya tuonewe, tunyonywe na kupuuzwa. Sasa tunataka mapinduzi; mapinduzi ya kuondoa unyonge, ili tusionewe tena, tusinyonnywe tena.”
Hali mbaya ilioko Tanzania leo ni matokeo yakuendelea kukubali kunyonywa, kupuuzwa na kuwa wanyonge katika nchi yetu wenyewe wakati tukiamini kuwa hatuna la kufanya ili kujikomboa.
Watanzania wenzangu, tukumbuke kuwa Tanzania ni nchi yetu wote, tuliyopewa na Mungu kuwa urithi wetu na watoto wetu. Tanzania sio mali ya kikundi cha watu wachache ambao wao ndio wanaotuamulia nini la kufanya. Tanzania ni haki yetu sote toka kwa Mungu. Sisi wenyenchi kwa pamoja ndio wenye haki ya kuamua mwelekeo wa taifa letu. Tanzania sio mali ya CCM, nchi hii ni yetu sote, Tanzania sio mali ya serikali ya CCM, nchi hii ni haki ya kila mtanzania. Ni dhambi kubwa sana kwa kikundi kidogo cha watu kupora haki ya kuzaliwa ya watanzania na kuwaamulia jinsi ya kuendeleza nchi yao.
Ninasema haya kwa sababu, kama sisi wenyenchi hatujui haki zetu na uwezo wetu katika kuamua hatima ya nchi yetu, daima tutakuwa watu wakuonewa na kunyanyaswa na kikundi kidogo cha watu wakishirikiana na wageni.
Hakuna mtu atakae kuja kuikomboa Tanzania kama sio mtanzania mwenyewe! Inasikitisha sana kuona kwamba kundi dogo la watanzania wenzetu wameingiwa na tamaa ya utajiri, na kuwa tayari kuiuza nchi kwa wageni ilimradi wao wapate neema hiyo hata kama sie wenyenchi tutashindia kipande cha mhogo na maji.
Na dhambi kubwa zaidi inayofanywa ni pale wanapotumia uchaguzi ili kumpora mwenyenchi haki yake ya kuzaliwa. Wote tunajua jinsi uchaguzi unavyoendeshwa kwa rushwa na wizi wa kura, halafu yule anae tangazwa mshindi anatamba kuwa amepewa ridhaa na wenyenchi ya kuwa kiongozi wao! Unajiuliza hivi kweli hawa ni watanzania wenzetu? Baada ya kuingia madarakani kwa hila, angalia wanapigania masilahi ya nani?
Mali asili zilizoko Tanzania ni mali ya watanzania wote bila kujali itikadi zao za kisiasa, leo hiyo haki ya serikali kuamua nani aje kuchimba dhahabu na almasi bila kuwashirikisha wenyenchi wamepewa na nani? Wanafanya hivyo kwa faida ya nani?
Hawa ndio wale wanaotaka kuitwa waheshimiwa na watukufu na ukimwita “ndugu” inakuwa shida kubwa. Huo uheshimiwa wameupata wapi? Viongozi wenye roho za kutaka uheshimiwa ndio hao hao wanaojiona wanajua lile lililo bora kwa watanzania bila hata kuwataka ushauri. Hawa ndio viongozi ambao wakati wa Mwl. Nyerere walikubali kuitwa ndugu!
Huko nyuma kulikuwa na sera ya Chama kushika hatamu, na leo na wahimiza watanzania wenzangu tushike hatamu za nchi yetu kabla hatujachelewa kabisa.
Watanzania wenzangu, inawezekana kuichukua tena nchi yetu. Historia inaonyesha kwamba wanyonge wanapoamua kuwa kitu kimoja na kauli moja inawezekana. Inawezekana kabisa kuondoa umasikini, inawezekana kabisa kuondoa ujinga, inawezekana kabisa kuondoa maradhi, na inawezekana kabisa kuondoa rushwa, ndio, inawezekana! Inawezekana kufaidi utajiri wa nchi yetu kwa pamoja.
Hili linawezekanaje?
• Kwanza, kutambua na kuamini kwa moyo wako wote kwamba wewe kama mtanzania unaweza kubadilisha hali ya nchi yako.
• Pili, kukataa kabisa kununuliwa wakati wa uchaguzi, na kuwaepuka kabisa wale wote wanao taka uongozi kwa kuununua. Mtu ye yote anae kubali kununuliwa ili ampe kura mtu fulani, huyo ni msaliti na mtu wa hatari kwa maendeleo ya taifa letu.
• Kudai haki zetu za kimsingi kwa kuhakikisha kwamba katiba ya nchi inatungwa na sisi wenyenchi na sio kundi la wachache wakipita mikoani kuuliza maoni yetu kuhusu katiba.
• Kutumia haki yetu kama watanzania ya kusema hadharani bila uoga yale ambayo tunaona sio sawa na kutaka yarekebishwe haraka. Sisi kama wenyenchi hatuiombi serikali hisani ili ituondolee kero, tunaiagiza serikali.
• Serikali yo yote itakayo kuwa madarakani, ielewe kwamba sisi watanzania ndio waajiri, nao wao ni watumishi wetu. Kwa maneno mengine, sisi wenyenchi ndio waheshimiwa na wao kuanzia Rais ni watumishi wetu. Kama tusipolizingatia hili tutaendelea kunyanyaswa na kundi la wajanja wachache na hatutakuwa na wakumlaumu.
Nimemaliza kusoma kitabu cha Mwalimu Nyerere cha UJAMAA NI IMANI;moyo kabla ya silaha. Katika mkusanyiko wa hotuba zake 4 hivi ambazo amezizungumza katika kipindi cha mwanzo cha utawala wake, zimegusa mambo muhimu kwa tiafa letu.
Katika hilo Nyerere anataja VIJIBWA kwa maana ya viongozi ambao kazi yao ni kutumika na wajkoloni huku wakiwatelekeza wananchi wao. Ukitazama hoja zake unaweza kuizifananisha na amzingira ya sasa kwamba watawlaawetu wengi hawana habari na wananchi wao, bali wengi wao wameelekeza akili zao kwa nchi za kigeni.
msingi mkubwa wanachojali ni wahisani,wafadhili, wawekezaji, na majina mengine…lakini hakuana aliyetayali kukubali kwamba kuna kasoro mhala ambapomfumo wa utawala wetu umeteguka ama haujaundwa.
Nimekuwa nikijaribu kuongea ana wazee wetu hawa kuwa hata suala la kupata uongozi wa kujenga umoja ni lazima tukubali kujitazama upya. Tujaribu kuangalia namna gani tunaweza kufauatlu kujenga msingi imara wa nchi yetu katika umoja wa kitaifa. Humo Nyerere anasisitiza suala la umoja wa kitaifa na suala la kuipenda nchi yako kabala ya lolote.
Inawezeakana tukasema kuwa suala hili ni suala la kujadiliana, na tunakubaliana ni suala la kuajdailiana. Lakini lazima tutzame ni namna gani tunajadiliana. Kwa mfano Nyerere anasisistiza mabadiliko kuendana na wakati. Nami hapa naumuunga mkono kwani mazingira aliyotawala siyo haya ambayo tunayosasa.
Mazingira ambayo yeye na wenzake walitawala siyo haya ambayo sisi tunaingia katika mvutano mkubwa wa mwingiliano wa kitamadunui. Kwa maana kuna mwingkliano mkubnwa wa kiuchumi, kisiasa, kitabaka n.k
Hebu tulitazame jambo hili la chama cha sisasa kunyinyakulia ushindi moja kwa moja na kupuuza nafasi za kuwepo kwa washindani wake.
Ni vema kabisa katika nafasi 10 alizoanazo Rias wa Tanzania kuteua wabunge, ni vema akatazma nafasi hizo kwa kuiangalia cnchi kuliko chama. Ukiangalia nchi unamaana kuna wanaharakati, wanasiasa wasio na vyma, kuna wataalamu wa fani mbalimbali, watumishi na wajuzi wa mambo mbalimbali.
Nafasi 10 hizi zingelitumika kuwachangua wabunge mahiri zaidi ili kuleta ushindani na kujnga umoja wa nchi yetu. Unaweza kuwateua akina Mbatia James, Mbowe Freeman, Ananilea Nkya, na wengine wengi tu ambao wanawakilishi wananchi wa kwa ujumla. Hawa niwaite wabunge wa kitaifa. Ni wabunge ambao wanasimamia maslahi ya taifa ingwa watakuwa kama wabunge wengine.
Kwa maana hiyo basi suala la kuwateua watu wa kada mbalimbali wenye sifa za kuwa wabunge ni muhimu sana kwa umoja wa nchi yetu. Wabunge hawa ni muhimu kwasbabu kwanza inaonyesha namna tunavyoheshimu demokrasia..wala tusllazimishwe mambo ya ughaibuni ya regime change. Tunaweza kujijengea utamaduni huo wa kuteua nafasi hizo kwa kutazama zaidi nje ya chama ingawaje haigombi kuwateua walio katika chama tawala ambacho kinawakilishwa na Rais mwenyewe.
Tunaweza kulifanyika kazi jambo hilo, kwani hata mzozo uliopo Zanzibar ni kutokana na kuharibu kile cheo cha makamu wa pili wa Rais ambacho kilik,uwa kikikaliwa na Rais wa Zanzibar. Tunaweza kurejesha hilo bila kujali ni chama gani kinashinda katika uchaguzi unaotuweka katika demokrasia yetu.
Ni vema tukafanya hivyo kuliko kuwa VIJIBWA kama ambavyo Mwalimu Nyerere alivyosema kwamba hivi kazi zake ni kubweka tu halafu hata having’ati vipovipo tu havina mwelekeo. Tujaribu kujisimiami katiika mhimili wa kujenga nchi yetu.
TIBA za jadi ni tiba zilizokuwa zikitumiwa tangu enzi za mababu zetu. Lakini tiba hizo kwa sasa zinatumiwa tofauti, kwani baadhi wameifanya kama biashara na kupoteza thamani ya aina ya tiba na hivyo wengi hukimbilia hospitalini.
Hivi karibuni nilifanikiwa kukutana na mganga wa jadi, Jongo Salum, maarufu kama Dk. Manyanyau ili niweze kujua sababu za mganga huyo kutumia paka wakati wa kutibu.
Dk. Manyaunyau alizaliwa Kigamboni, Wilaya ya Temeke, Dar es Salaam, miaka 28 iliyopita, na kupata elimu yake ya msingi katika Shule ya Kigamboni na kuishia Darasa la Nne.
Sababu za kuingia kwenye uganga
Dk. Manyaunyau anasema katika familia yao asili ya bibi na babu zake wako katika fani ya uganga. Na katika makuzi yake alikuwa karibu na na babu yake mzaa baba, mzee Abdallah Nyambo.
“Kilichomvutia babu yangu kuwa karibu nami ni utundu niliokuwa nao na pia katika ndoto nilizokuwa nikioteshwa usiku. Zilikuwa zikitokea ukweli, kitendo kilichompa babu yangu moyo kwamba ndiye ninayefaa kurithi mikoba yake, kwani kuna wakati kulikuwa kukitokea msiba karibu na mtaani kwetu, nilikuwa naweza kutabiri kwamba ni nani kafariki na nikienda unakuta ni kweli.
“Kutokana na hali hiyo, babu alianza kunitumia nimsaidie kufunga dawa za wagonjwa waliofika nyumbani kwake kwa ajili ya matibabu. Hata hivyo, kazi hii binafsi nilikuwa siipendi na hata nilipofikia hatua ya kumtamkia babu kwamba siipendi, aliendelea kunipa wasia na kuniambia mambo haya yapo katika jamii tunayoishi, hivyo nisiogope,” anasilimua Manyaunyau.
Anasema tangu babu yake amwambie maneno hayo, hakuwa anajisikia vizuri mara kwa mara, kwani kuna kipindi alipokuwa na homa, babu yake alimwingiza kwenye ofisi yake ya utabibu na kumwekea tunguli kichwani na kupona. Kitendo hicho cha kupona kila alipowekewa tunguli kilimzidishia babu yake faraja na kumwambia kuwa mizimu inamuhitaji.
Na kumwambia kuwa katika maisha ili afanikiwe anahitajika kuingia katika mambo ya uganga na kama hatokubali anaweza kuwa chanzo cha kutokea kwa vifo katika kizazi chao.
Dk. Manyaunyau anasema siku moja akiwa kijijini kwa babu yake huko Chole Samvula, alipelekwa na babu yake kwenye matambiko na aliporudi nyumbani kwa mama yake Kigamboni alimweleza mambo ayoambiwa na babu yake ayafanye. Hata hivyo, anasema umri wake ulivyofikia wa kuandikishwa shule, mama yake alienda kumwandikisha lakini hakusoma kwa raha.
Kuna kipindi wanafunzi wenzake walimtenga na kumuogopa kwa madai kwamba alikuwa akitoa macho wakati yeye alijiona kawaida.
Dk. Manyaunyau anasema ilifika wakati watoto hao wakaenda kumsemea kwa walimu na wazazi, jambo lililokuwa sababu ya yeye kuamua kukatiza masomo yake akiwa Darasa la Nne. Baada ya kuacha shule Dk. Manyaunyau alikwenda kufanya kazi ya kupaa samaki eneo la Feri. Baadaye alifanya kazi ya ubebaji takataka katika masoko ya Buguruni Kwa Mnyamani, wilayani Ilala.
Baadaye alijidumbukiza katika kazi ya upigaji debe ambako pia hakukaa sana katika kazi hiyo. Aliamua kwenda kujiunga na kikundi cha sanaa cha Kaole ambako alikuwa akiigiza kama teja.
Dk. Manyaunyau anasema pamoja na kupenda fani ya uigizaji, lakini hakuwa na raha nayo kutokana na vitu vilivyokuwa vikimwandama katika mwili wake kumsumbua kwani ilifika wakati hadi akashindwa kuigiza vipande alivyopangiwa.
“Siku moja nikiwa katika kazi hiyo ya uigizaji, nilishikwa na homa kali halafu kukawa na vivuli vikinitokea na kunikumbusha maagizo niliyopewa na babu. Vilinisisitiza kuwa hakuna riziki yoyote ya kifedha nitakayoingiza kama sitokubali kazi ya uganga,” anasema.
Anasema ndipo alipoamua kurudi tena kwa babu yake kijijini Chole na kurithishwa mikoba hiyo ya uganga.
Jinsi alivyorithishwa mikoba
Siku hiyo babu yake alimpeleka porini na kumchimbia shimo refu, akamtumbukiza na kumfikia kisha kumwacha sehemu ya kichwa tu.
Baada ya hapo alimzungushia nyoka mkubwa aliyezunguka shingoni na alitakiwa akae sehemu hiyo na nyoka huyo kwa siku saba na kuletewa dawa kila usiku na alipokunywa alijihisi kushiba.
Dk. Manyaunyau anasema babu yake alikuwa akizungumza na nyoka yule kila alipofika eneo hilo, na baada ya siku saba kuisha alichanjwa chale miguuni na mikononi ikiashiria kwamba ndio kinga yake.
Kama vile haitoshi baada ya kuchanjwa, aliletewa paka watatu ambapo babu alimchinja mmoja kati yao na kunywa damu. Na yeye akapewa anywe kwa maelezo kwamba ndiyo nguvu yake itakayokuwa inamuongoza.
Baada ya kumaliza zoezi hilo, anasema alitokwa na jasho jingi na kutetemeka takriban dakika tano, mwili ulipokuwa baridi, babu yake alimtaka kula na maini ya paka.
Dk. Manyaunyau anasema baada ya kumaliza kula maini yale, akaanza kuona ulimwengu mwingine. Aliweza kuona watu wakiwa majumbani mwao wanafanya shughuli zao na babu yake kumwambia sasa ameshaiva kwa ajili ya shughuli ya uganga na kumkabidhi rasmi vifaa vya uganga.
Vifaa alivyopewa na babu aliambiwa kwamba vitampa uwezo wa kupambana na ndondocha, wachawi, misukule na kumtaka kuwasaidia watu watakaokuwa wamekumbwa na vitu hivyo.
Vilevile babu alimlisha kitu alichokiita azima kilichomfanya aanze kuona vitu vya ajabu kama vile wenye kucha ndefu, watoto wachanga wanalia, watu wengine wakiwa wamevalia vizuri ambapo aliambiwa kuwa hao ndio misukule na kanzia hapo ndio akawa mganga.
Kazi alizowahi kufanya
Kwa Mkoa wa Dar es Salaam kazi ya kwanza anasema aliifanya maeneo ya Yombo Vituka ambapo alitoa wachawi. Anadai wakati huo bado watu walikuwa wagumu kumkubali na kumuona kama mwongo.
Kazi nyingine aliifanya Yombo Buza ambako baba mmoja alikuwa na mgonjwa aliyefunga kula kwa muda wa siku 25. Katika utabibu wake, Dk Manyaunyau aliwaambia kwamba mgonjwa wanayemuuguza siye na badala yake ndugu yao huyo yupo juu ya dari na miongoni mwa wanaomtesa ni baba yake mzazi.
Siku aliyotaka kumtibu mgonjwa huyo aliwataka watu wengi kujitokeza, ili washuhudie kile anachokifanya kuondoa dhana ya kutomuamini.
Siku ilipowadia alifika nyumbani kwa baba mwenye mgonjwa huyo na kuwakuta wametandika maturubai kuashiria msiba. Hata hivyo, anasema aliwaacha wakaenda kuzika na kuahidi kwenda kumtoa marehemu huko huko makaburini.
Alipofika kwenye kaburi lile alipiga ‘nyanga’ moja na kutoka mbwa aliyekuwa amening’inizwa. Mbwa huyo alikuwa akitoa harufu kali na baadaye kugeuka kuwa mtu, lakini kutokana na kuchukuliwa msukule kwa muda mrefu, hakuishi muda mrefu tangu afufuliwe na badala yake alifarikiUmaarufu mwingine anasema aliupata pale alipoenda kuagua katika Shule ya Sekondari Yombo Vituka ambako wanafunzi walikuwa wakianguka ovyo. Watu walianza kumuamini na kupata kazi sehemu mbalimbali. Moja ya kazi aliyopata Dk. Manyaunyau anasema aliitwa Mwananyamala kumtoa mtoto aliyepotea.
Baada ya kupatikana kwa mtoto huyo alipewa nyumba ya kuishi ili kuweza kutoa wachawi.
Magonjwa anayotibu
Mbali na kutoa mambo ya ajabu ajabu namna hiyo, lakini pia anatibu magonjwa mengine kama kisukari, pumu, ngiri, mgoro, kiarusi, malaria na magonjwa mengine
Anasemaje kuhusu mauaji ya albino
Dk. Manyaunyau anasema si kweli kwamba viungo vya albino vinatumika kazi katika kutibu. Amewaita watu wanaofanya hivyo kuwa ni majangili.
Anasema hakuna ukweli wowote kwamba utumiaji wa viungo vya binadamu ndiyo unaomfanya mtu apate mafanikio. Amewataka wanaoamini mambo hayo kuacha mara moja.
Akizungumzia kuhusu kufutiwa leseni waganga na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Dk. Manyaunyau anasema hiyo si njia pekee ya kupambana na vitendo hivyo. Badala yake serikali na waganga washirikiane katika kukomesha vitendo hivyo, kwani ukweli ni kwamba wao wenyewe wanajuana nani mganga wa kweli na nani si mganga.
Anasema kwa kusitisha huduma hizo za uganga kutakuwa ni mateso kwa watu ambao magonjwa yao yanatibiwa kwa dawa asilia.
Hata hivyo, anawataka watu wanaotumwa na waganga kupeleka viungo hiyo kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi, ili watuhumiwa waweze kukamatwa. Waganga wanaotumia viungo vya binadamu ndio wachawi
UMASIKINI, NJAA, UJINGA, MIUNDOMBINU MIBOVU INASABABISHWA NA WATAWALA WETU.
Na Ismail Mang’ola
Ni MIAKA MINGI imeshapita tangu nchi hii kupata uhuru pale mwaka 1961 chini ya muaasisi wa Tanganyika sasa Tanzania Mwalimu Julias Kambarage Nyerere ambaye tunaweza kumuhesabia kati ya watu 1000 waliokuwa na uchungu wa ardhi yao basi hakuna mwingine wa kumuweka mstari wa mbele zaidi yake.
Wakati wa uhai wake na pale alipokuwa madarakani, Mwalimu alipigania kufa na kupona kuhakikisha kila mtanzania anakuwa na haki sawa na wenzake bila kujali huyu ni tajiri kiasi gani na hata wakati mwingine aliweza kuwakemea waziwazi waliojinyesha kuwa mwenye nacho abaki kuwa nacho na asiokuwa nacho pia abikie hivyohivyo.
Hali hiyo Mwalimu aliipinga vikali kiasi cha kila aliyekuwa na mamlaka ya uongozi katika sekta yake alimuona Mwalimu kama vile alikuwa akiwavurugia mipango yao ya ukwanini usiendelea hali ambayo ilimlazimu muasisi huyo kukereka na tabia hiyo ya kibaguzi.
Katika haya yaliyochukiwa na Mwalimu wakati wa uhai wake na alipoonekana akiyakemea baadhi ya matendo hayo na kuwanyooshea baadhi ya watu fulani vidole kwa mfano, hali hiyo haikukoma kikweli kweli bali ilikuwa ni kama mtu apandaye mbegu ya nafaka fulani ili kwa ajili ya kuotesha kwa ajili ya kupata mbegu nyingi.
Leo hii tunashuhudia jinsi gani mbegu hizi zilivyoongezeka na kusababisha hata mimea mingine isiyofaa kuwepo katika ardhi hii ya mwenyezimungu kuwepo, hili kwa sasa limekuwa ni kero kubwa kiasi cha watanzania wengi kuanza kumkumbuka hayati Mwalimu Kambarage kwa yote aliyoyafanya na aliyokuwa akiyataka watanzania wayapate.
Neno Umasikini katika ardhi yetu hii ya Tanzania kimekuwa ni kitu cha kawaida sana’ licha ya kuwepo rasilimali nyingi ambazo zinaweza kukidhi hali halisi ya mtanzania kwa namna yeyote ile, vinginevyo tutakuwa tunadanganyana.
Watanzania tuelewe kwamba upendo na Amani ndio silaha yetu kuu hapa Tanzania, vilevile tunakitu kinachoitwa mshikamano na utulivu, hivi ndivyo ngao zetu za kujikingia na silaha hizo kali zinazosababisha mambo yote haya yaliyopo mbele yetu ambayo bado yanaendelea kuivuruga akili za watanzania wengi juu ya mstakabali mzima wa uchumi wa Tanzania.
Hivi sasa tunaelekea katika uchaguzi mkuu ambao unatarajia kufanyika nchi nzima mapema Novemba mwaka huu huku kampeni zake ziktarajiwa kutimua vumbi Augost kwa kila mmoja akishuka na sera zake za kuombea kura kwa watanzania wazalendo wasiopenda makuu.
Tanzania ni nchi ambayo imetawaliwa zaidi na Amani, upendo, mshikamano pamoja na utulivu kama nilivyoelezea katika paragrafu iliyopita ndio chachu ya watanzania kuwa pamoja, sambamba na kushirikiana katika matatizo mbalimbali yakiwemo misiba Nk.
Lakini nikirudi kwenye ukweli, naona kuna ubinafsi na ubaguzi katika maisha tuishio sisi kwa sisi tukiwa watanzania wenye usawa bila ubaguzi kitu ambacho mwalimu alikikataa tangu pale alipoanza kupigania haki ya Mtanganyika huko miaka ya Hamsini iliyopita.
Sasa tunaishi kama wakimbizi, hali ya maisha kwa mtanzania yamekuwa kama mchimba zahabu ambaye hajui ni lini atapata zahabu akauze, licha ya watawala walioko madarakani kuyashabikia maisha haya waishio wapiga kuwa wake ambao huwafanya wakae katika viti hivyo.
Kama atatokea kiongozi mwenye imani na nchi yake na anayeyajua hesabu ya rasilimali zilizopo hapa nchini pamoja na idadi ya wananchi wake kisha koingozi huyo akabalansi ni kifanyike angalau hata asilimia 40 ya mtanzania aweze kufaidika na rasilimali yake, hakika hakuna kisichowezekana kwani, Madini pekee yanatosha kumtoa kimasomaso mtanzania huyu anayeteseka katika ardhi yake yenye neema.
Uwezekano huo upo, Nishati tuliyonayo si ndogo. Kama Serikali na viongozi wake watafanya mikakati ya ukweli bila kuangalia huyu anawadhifa gani na kupanga bajeti ya kuchimba Tanzanite kwa muda miezi sita pesa hiyo bila kutumiwa na wizara yeyote au mtu, hakika nina imani kubwa watanzania wengi wanaweza kukwamuka na umasikini huu na matokeo yake kila mmoja ataweza kufurahia matunda yanayotoka katika aridhi yake hii na hapo hakutakuwa na malalamiko.
Serikali inauwezo huo si kwamba inashindwa, sidhani kama kufanya hivyo kutakuwa kumeiathiri sana Serikali kwa imani ya kuwa na rasilimali nyingi.
Tuna Gesi ambayo inaweza kuwakomboa watanzania kama Serikali itakuwa makini na wawekezaji ambao naamini wapo ambao wanahitaji kuisaidia Tanzania kwa mtindo huo wa kuwekeza.
Vilevle Dhahabu tuliyonayo inatosheleza kabisa kusaidia harambee hiyo ya kuwatoa wazalendo hawa katika hali ya umasikini.
Kama ikiwa kama kuna baadhi ya watanzania wenzetu tena wachache waliweza kupata fedha mbalimbali za mikopo tena mamilioni ya shilingi ya Tanzania je iweje hata Milioni moja moja ya kuwagawia watanzania wasiokuwa na kazi ishindikane kama sio ubaguzi nini?.
Naamini rais anawashauri wake na yeye pia ana maoni yake, nasikitika kitu kimoja ambacho rais wetu anashindwa kutoa maoni hayo kama ambavyo alivyoahidi kipindi cha kampeni za uchaguzi wa mwaka 2005 kuwa atahahkikisha kila mtanzania anakuwa na Maisha bora Ari mpya huku akimalizia na Nguvu mpya.
Hii iliwapa matumaini makubwa watanzania, lakini kinachosikitisha ni kutoyaona hayo yaliyotajwa licha ya kuwepo mambo mengi ambayo nampigia makofi kwa jitahada zake, lakini bado hakijamkomboa mpiga kura wake.
Nasikitika kuona wafanyabiasha wanakuwa na sauti kuliko Rais, kwa sasa wafanyabiasha wamemgeuza rais kama vile ni mtu wa kutaniana naye hasa pale rais anaposema tabia ya upandishwaji wa bidhaa kiholela ikome lakini utakuta kauli hiyo ya mkuu wa nchi inaingilia siko9 hili na kutokea siko la upande wa pili.
Ni jinsi gani wanavyonekana ni watu wa madharau kitu ambacho kinaonekana kitaalam nchi haiwezi kujengwa kwa stahili hiyo, kwani katika mataifa ya wenzetu, wafanyabiashara wake wanakuwa na nidhamu pia mara kwa mara wanakuwa karibu na kiongozi wao wa nchi kwa kubadilishana mawazo mbalimbali kuhusiana na biashara waziagiziazo nje ya nchi na hata wale wa ndani ya nchi.
Leo hii mtanzania amebanwa sana katika suala la chakula, hivi sasa mchele, Maharagwe, Mafuta ya Kupikia, Mafuta ya taa, Unga, Unga wa ngano vitu ambavyo vingetakiwa kuwa bei ya chini ili angalau kuepusha malalamiko ya wananchi, lakini cha kushangaza vitu hivi kwa sasa vipo bei juu tofauti na hali halisi na kipato cha mtanzania wa kawaida anachokipata, je hawa watu wakimbilie wapi?.
Kwa sasa hakuna asiyejua juu ya Miundombinu yetu hapa jijini na nchi nzima kwa ujumla, hali ni mbaya sana kiasi cha kuhatarisha magonjwa ya kuambukiza, mifereji imechakaa, kila kona ya jiji hali mbaya barabarani, maji safi na salama utata mtupu, sasa watanzania asilimia 75 wanakunya maji ya visima ambayo si safi na salama, lakini asilimia ishirini na tano ndio watu bora wanaoweza kupata maji safi na salama hasa maji ya chupa yenye thamani kubwa.
Mnyonge mnyongeni lakini japo hata kama ana haki kidogo basi apewe!, tusisubiri mpaka ashtuke kitu ambacho kinaweza kuigharimu Serikali kwa kutumia mamilioni ya pesa kulitafutia ufumbuzi suala husika wakati ambapo kama tutakuwa makini gharama hizo hazitatuhusu kwa wakati huo kila mmoja atakuwa akijishughulisha mwenyewe kwani kama mtaji atakuwa nao kwa hiyo Milioni moja aliyopewa.
Kuna vitu vichache sana ambavyo mtanzania huyu anavihitaji: Kikubwa ni mtaji, apate milo mitatu kwa siku, maji safi, barabara safi ambayo itaondoa usumbufu wa foleni nyakati za kwenda kazini ama wakati wa kurudi nyumbani.
Barabara za sasa zimekuwa kero tena kero kubwa, inafikia mtumishi kugombana na bosi wake kwa madai ya kuchelewa kazini kutokana na foleni zilizopo karibia barabara zote hapa jiji.
Unaingia kwenye daladala saa kumi na mbili kasoro asubuhi unafika kazini saa mbili na robo au na nusu kitu ambacho ni hatari kwa tajiri na ukimweleza shida uliyoipata huko barabarani hakika hawezi kukuelewa, hili ni tatizo kwa mtanzania na linahatarisha kukosa kazi kwa muhusika.
“Niguse bahati mbaya; nikuumize makusudi,” Imam Abbas kwenye wimbo wake ‘Bila Sanaa.’ Wanadamu wenzangu, mbona utu umetukimbia?
Kelele za “mwizi, mwizi!” zinapopigwa, unyama na ukatili usio wa kawaida huamshwa ndani ya roho za baadhi yetu. Huu ni ukweli usiopingika kutokana na maovu tunayowatendea binadamu wenzetu, wanaoitwa wezi. Tunawapiga na hata kuwachoma moto bila kujua kama wana hatia au la; kama wameiba fedha za umma au wamekwepua tu cheni bandia. Kuendelea kwa matendo haya ya kinyama, kikatili na kutisha, ni kosa letu wote. Na ni lazima tugawane lawama sisi sote kama wanajamii.
Inatubidi tujiulize: Huu ukatili uliojengeka na kuwa sehemu ya utamaduni umetoka wapi? Ni kwanini bado tunakubali uendelee katika jamii yetu?
Hoja za majibu hayo ni nyingi, lakini pia nyingi ni za kijinga na kipumbavu, tena hutoka kwa watu wanaojidai kuwa na akili timamu — kumbe ni makunyata tu! Hili suala la kuongezeka kwa hali ngumu ya maisha, huja na ongezeko la hasira, ngeni, hasa pale mtu anapoibiwa kile alichokihangaikia kwa jasho na damu yake, tena kihalali. Hilo linaeleweka, lakini halitoi idhini kwa mwananchi kujichukulia sheria mkononi. Watu wote wanaojichukulia sheria mkononi, wao pia wamevunja sheria sawa sawa na yule muhalifu wanayempiga. Tena uhalifu wao ni mkubwa zaidi kwasababu wao wameua! Wameiba uhai wa mtu ambae aliiba simu, ambayo inayoweza kununuliwa tena. Inaonekana ukatili ukitupanda, basi unatupanda kweli na tunatupa pembeni mawazo na maamuzi ya busara, na kuanza kumcheka nyani na makalio yake bila kujua kuwa yetu ni mekundu pia. Tena yetu ni mekundu zaidi kwani yanatiririka damu ya huyo tunayempiga na kumchoma moto.
Lakini, je, ni sahihi ‘kutetea’ ukatili wa baadhi yetu na kudai unatokana na ukata wa maisha na umasikini unaotusumbua? Labda hasira na misongo yetu binafsi huishia kutolewa kupitia ukatili kwa tunayemtendea unyama mtu anayeiitwa mwizi. Hapa ndipo ninaanza kuona umuhimu wa madaktari wa kisaikolojia, au therapists. Baadhi yetu, ambao ni wehu na wakatili kupindukia, tunadhani kumpiga mwizi itapunguza kuchanganyikiwa au misongo ya maisha yetu. Kwani, kumbonda binadamu mwingine na jiwe kichwani ni kama therapy session… tiba mbadala.
Sasa ujuha na ukatili ndipo hapo huingiliana kwasababu kuna watu – tena tunaishi nao majumbani mwetu, tunafanya nao kazi, tunasalimiana nao mitaani, na hata kwenda kusali au kuswali pamoja – wanadiriki kutetea ukatili huu. Hoja zao za kikatili na kipuuzi hudai kuwa, kuwauwa wezi ni fundisho kwa wengine; tatizo la uhalifu litapungua.
Nasema fikra hizi ni za kikatili, kipumbavu na kipuuzi! Na watu wenye mawazo haya tuwaogope zaidi ya ukoma!
Kwasababu ifuatayo: Hali halisi ni hivi, hata tukiwachapa na kuwachoma moto vibaka kwa kasi mpya, nguvu mpya na ari mpya, kamwe hawatapungua. Hii ni kwasababu, mwisho wa siku, tumbo lenye njaa litakoroma tu; njaa itauma, na binadamu huna budi kukubali kulitumikia vile uwezavyo. Utake usitake. Na jinsi ajira zilivyokuwa finyu, kwa waliosoma na ambao hawakubahatika au kupata nafasi ya kusoma, hawawezi kuacha kuiba mpaka wapewe maisha mbadala. Sisemi kwamba kama hujasoma na huna kazi basi uibe. Hapana! Lakini ndio hali halisi ya vibaka wengi. Jambo la msingi hapa ni kwamba, kujaribu mabadiliko ya mazingira hubadilisha tabia za watu; kwani hata siku moja mkulima wa mahindi havuni mihogo.
Upande wa pili wa sarafu ni hivi vyombo vyetu vya habari. Waandishi wa habari wanazidi kutuangusha katika kupinga huu ukatili. Vyombo vya habari vimekuwa vikichochea badala ya kukemea, na hata wale ambao wanakemea, wanafanya hivyo kinafiki! Sio wote, ila kuna wale ambao wanakemea huku wakitumia lugha ya uchochezi.
Vyombo vya habari vina nafasi nyeti sana katika jamii, kama tulivyoona katika mauaji ya halaiki Rwanda mwaka 1994. Vyombo hivi vilitumika kujaza watu uhasama na kuchochea mauaji, huku wakiita upande mmoja “mende.” Hiyo ilisaidia kufanya upande huo kuonekana sio binadamu tena, hivyo thamani yao kupotea na utu wao kuyeyuka. Matokeo yake tunayatambua vizuri.
Kwani, si ni vigumu kumuua kuku? Ujue, pindi utakapomuona binadamu mwenzako kama kiumbe tofauti na binadamu, basi kumuua inakuwa sio vigumu tena! Leo hii vyombo vya habari wanadiriki kutumia lugha kama mwizi “akibanikwa.”
Hebu tuangalie matumizi ya lugha hapo. Kuku hubanikwa, mbavu za mbuzi hubanikwa, hao wote ni wanyama! Lakini utumiapo neno hilo kwa binadamu mwenzako, ina maana umemvua utu wake. Thamani ya uhai wake haizidi ya mnyama mwingine yoyote tunayemchinja kama kitoweo. Hivyo, pamoja na kuwa tunaweza tukawa tunapinga mauaji hayo, lakini matumizi ya lugha yetu yanahamasisha na kuchochea.
Halafu vyombo vingi hupenda kutumia maneno “wananchi wenye hasira kali.”
Kuna chembe za kuhalalisha dhana ya ukatili. Eti kwasababu walikuwa na hasira, na tena ni haki yao kuwa na hasira… Huu ni ujinga mtupu ulio tukuka! Kwani mara nyingi hao wananchi wenye ‘hasira kali’ ukiangalia picha kwa ukaribu, utagundua wengi wao wana nyuso za kushangilia, kuchekelea na kushabikia. Hivyo hiyo dhana ya kuwa na hasira ni potofu.
Vyombo vya habari na waandishi wamekuwa wakipotosha jamii kwa kuchapisha na kuongelea mambo ya uongo. Hapo hapo, vikizidi kuwachochea wakatili hawa badala ya kukemea moja kwa moja kwa lugha sahihi — kali. Hivi kwani, tukiwaita wananchi hao wakatili, wauaji, kuwapiga picha na kuwaanika mbele ya jamii, si litakuwa jambo la busara? Mbona wezi wa mali ya umma, mapapa wa nchi hii, tunawaita mafisadi? Kwanini wao tusiwaite wajasiriamali?
Inabidi baadhi ya vyombo vya habari viache unafiki na ushabiki. Mimi na wewe hatuna budi kupinga na kukumea vikali unyama huu! Na kuacha kuwaita hao wauaji ‘wananchi wenye hasira kali’, kwani (nadhani) tunawapa kichwa kwa uwenda wazimu wao.
Tuwapige picha, na tuanze kuwatafuta. Tukianza na huyu aliyebeba tofali na huyu anayemvisha tairi mwizi!
Jeshi la polisi nalo libebeshwe lawama kwa kushindwa kukomesha huu unyama. Tabia ya kuwaachia wahalifu kutokana na sababu wanazozijua wao wenyewe linachangia ukatili huu kuendelea. Wakuu wa Jeshi la Polisi nawashangaa kwani hawaoni aibu kwa kufanyiwa kazi yao na wananchi. Kwani hii imekuwa hadithi ya mkia kuongoza kichwa? Jeshi la Polisi liwatie nguvuni wahalifu na mkondo wa sheria uchukue nafasi yake. Pia, iwatie nguvuni wananchi wanaoshiriki katika haya mauaji ya kutisha. Hata kama atakamatwa mmoja, huo ndio utakuwa mwanzo. Jeshi likikaa na kushangalia haya mauaji, na sisi raia wa kawaida tufanyeje? Mheshimiwa IGP Mwema, hili ni tatizo ambalo nadhani linahitaji suluhisho, au haya maradhi yatazidi kuendelea kwenye jamii, na kidonda kuishia kuwa ndugu.
Mimi ninaamini kunaweza patikana njia mbadala ya kuadhibu wahalifu tunanapowakamata mitaani. Kwanini tusifanye kama nchi nyingine, mwizi akikamatwa, achapwe mijeledi kadhaa, kisha apelekwe polisi? Hili linaweza kusimamiwa na balozi wa nyumba kumi kumi wa mtaa aliokamatiwa mwizi huyo, au hata kiongozi yoyote wa mtaa huo. Lakini utekelezaji wa adhabu hii utafanywa ndani ya vipengele vya sheria na si kienyejienyeji tu.
Hoja ya pili ni hii ya kukata viungo pindi mwizi akamatwapo. Hilo lisipewa hata nafasi, kwani haliwezi kuwa adhabu mbadala. Najua baadhi yetu hapa ambao wanadhani hilo ni jambo la maana katika kukomesha wahalifu. Hilo ni jambo la kikatili sana, kwani ukishamkata mtu mkono umezidi kumrudisha nyuma kimaisha. Kivipi? Wezi wengi ambao tunawakamata mitaani ni watu ambao hufanya kazi za kutumia nguvu “blue collar jobs,” kama zikipatikana. Hivyo basi, pale tunapoamua kumkata mkono, tunamfanya ashindwe kuweza kujitegemea. Kazi gani atapata akishakuwa na mkono mmoja, na hana elimu? Hivi kweli atapata kazi ya kubeba mizigo Kariakoo, au ataishia kuwa omba-omba, halafu aanze kufukuzana na wana-mgambo? Hilo la kukomeshana kwa kukatana viungo halina mantiki, tena ni ukatili mwingine ambao utaongezea watu shida za kimaisha badala ya kuwasaidia.
Kuna mambo mengi sana ambayo yanaweza kufaidisha Taifa letu pindi wezi wanapopatikana na kufungwa jela. Tanzania ina ardhi kubwa tu, kwanini wasilimishwe? Au hata kwenda kusaidia wanavijiji kuvuna na kulima, na kushughulishwa na kazi nyingine za kijamii? Serikali haitakuwa na haja tena ya kuajiri watu wengi kufanya baadhi ya kazi zinazohitaji nguvu nyingi kwani zitashughulikuwa na wafungwa. Tayari, si wanalishwa na kodi zetu? Basi watumiwe ipasavyo katika jamii ambayo inawalisha. Moja, watajifunza mbinu mbadala za kuendesha maisha yao. Pili, watasaidia kujenga jamii badala ya kuendelea kuiharibu kwa matendo yao maovu.
Mwisho, tusikae hapa na kujazana ujinga. Eti jicho kwa jicho, jino kwa jino ndio suluhisho la uhalifu. Sote tutaishia kuwa chongo au vibogoyo. Sasa sijui nani atamwongoza nani baada ya hapo. Wadau wa kwenye vyombo vya habari wajue kwamba wao wana nafasi kubwa sana katika kukemea na kusaidia kutokomeza huu unyama wa baadhi ya manduli wachache katika jamii yetu.
Pia tusisahau kuwa, hata tukichomana moto kila siku, kama hali ya maisha ni ngumu, ni ngumu tu. Na watu watafanya vyovyote kukidhi mahitaji yao; hapo ndipo viongozi wa maisha bora kwa kila Mtanzania inabidi waulizwe, kulikoni? Hivyo, wachochezi wote wa huu unyama, wananchi wenye roho za kikatili za namna hii na viongozi mafisadi wanao sababisha hali ya Mtanzania kuzidi kuwa ngumu, wote ni makunyata!
Vijana wenzangu, hatuwezi kuendelea kufanyiana ukatili kama huu sisi wenyewe kwa wenyewe. Tuelewe kuwa umasikini wetu unasababishwa na mafisadi wachache walio juu… Hao ndio maadui zetu wakubwa.
TANZANIA KUBADILIKA INAWEZEKANA

[...] ” Makala [...]
VIJIBWA VYA MWALIMU NYERERE.

MARKUS HONORIUS
Dar Es Salaam, Novemba 30, 2009

TUKEMEE UFEDHULI!
[Makala hii inatoka kwenye tovuti ya http://vijana.fm

Tazama video hii kama tu una moyo mgumu.
Weka maoni yako hapa!
Maoni mapya
Zinatembelewa zaidi
Makala mpya
Habari zaidi
Burudani
Makala mpya
Zenye maoni mengi
Zinazotembelewa zaidi
Counter:347,251
Maintained by Daima Solutions | Log in | Entries (RSS) | Comments (RSS) |