Home » Jamii/Maoni

Jamii/Maoni

Maoni ya wananchi kuhusu huduma za Afya wilayani Njombe

  CHRISTOPHER PAYOVELA: Huduma si nzuri na mara zote ili upate huduma nzuri ni lazima ufahamiane na mfanyakazi katika hospitali husika utakayokwenda kupata huduma vinginevyo utanyanyasika. Mazingira ni machafu kuanzia nje mpaka ndani, pia nafikiri hali hii inachangiwa na mishahara midogo wanayopewa wahudumu wetu.
JESCA MWINUKA: Huduma katika hospitali zetu hapa Njombe zinabagua kwa kuangalia uwezo wa kiuchumi alionao mtu, pia ili upate huduma lazima utangulize pesa kwanza vinginevyo utakaa kwenye foleni kutwa nzima.
MARIAM ELIAS: mie sijawahi kuombwa rushwa wala kupewa huduma mbovu, siku zote ambazo nimehudhuria katika hospitali ama kituo cha afya upewa huduma safi. Kwa hiyo naweza kusema kuwa huduma katika wilaya yetu ni safi.
GUSTAFU MSEMWA: kusema kweli huduma za afya hususani kwa watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI ni nzuri, Dawa zinapatikana na matibabu yapo safi, sijawahi kusikia malalamiko yoyote kuhusu huduma mbovu kwa watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI.

MARY ANTONY: binafsi suala la huduma naliona katika mtazamo tofauti kwa kuwa sidhani kama unaweza kutoa huduma na kumridhisha kila mtu, pia mtu anaweza kwenda hospitali akifika huko kwa bahati mbaya siku hiyo akapewa huduma ambayo hakuridhika nayo akitoka hapo anachukulia huduma mbovu hutolewa siku zote kumbe si kweli.

ZEDEKIA YAHYA: hali ni mbaya kwa watu wenye kipato  kidogo, kama huna pesa unakufa, si hospitali  za serikali wala binafsi. kwa mfano kaka yangu alilazwa katika hospitali moja hapa makambako kwa usiku mmoja tulitoa shilingi 25,000. Pesa hii kwa mwananchi wa kawaida si rahisi kuipata, maana yake ni kwamba utakufa kama huna pesa.

JENIFER FABIAN: huduma kwa kweli zinasikitisha sana, usishangae ukienda kulazwa ukapewa kitanda ambacho mtu kafariki muda si mrefu na blanketi za kitanda husika ni chafu na hazijabadilishwa, hali hii ni hatari kwa afya zetu kwani kwa mtindo huu ukiingia kutibiwa hospitali unatoka na magonjwa zaidi ya tatizo ulilokuwa nalo.

MLOTE BRIGHTON: hospitali nyingi katika eneo la makambako hazina madawa, ukifika katika kituoa cha afya kupata huduma unaambiwa hakuna dawa nenda kanunue. Hospitali hazina magari yanayotoa huduma kwa wagonjwa na hii upelekea watu wengi kufariki kwa kushindwa kufikia huduma kutokana na uhaba wa magari.
FELIX SANGA: huduma ni mbovu, ili upate huduma ni lazima uwe na pesa vinginevy utafia mapokezi, wakati mwingine unatoa pesa na bado unaambiwa hakuna sindano na dawa, ndio maan mie huwa naona bora niende hospitali za misheni kuliko za serikali.

 

 

Comments are closed.