Kalenga:Afumania Ugoni, Apofuliwa Macho
Na Francis Godwin,Iringa
MTAMBUE kijana Frank Joseph Kalenga (37) mkazi wa Mtaa wa Ngelewala Kata ya Mwangata mjini Iringa aliyepata kuwa mfanyabiashara mkubwa. Kwa sasa amegeuka omba omba katika mji wa Iringa baada ya kucharangwa mapanga usoni na kupata ulemavu macho (upofu ) wa kudumu. Hii ni kutokana na kile anachoeleza kuwa ni kufanyiwa unyama huu na mgoni wake ambaye mwisho wa yote alimpokonya mke na kumwacha akiugulia maumivu ya mapanga .
Maisha ni safari ndefu iliyojaa raha na mahangaiko ya kila aina na iwapo utabahatika kupata historia ya kila mmoja bila shaka unaweza kukuna kichwa na wakati mwingine kujiona kuwa matatizo yako si lolote ukilinganisha na matatizo yale ambayo umepata kuelezwa na rafiki yako.
Baada ya utangulizi huo nikurejeshe katika makala haya ambapo kama ilivyo ada ningependa kutumia usemi ule wa wahenga wetu kuwa hujafa hujaumbika.
Kijana Frank Kalenga si mgeni kwa wakazi wa mkoa wa Iringa hasa wale waishio katika manispaa ya Iringa, kwani, amekuwa akifanya jitihada kubwa za kuzunguka huku na kule katika maeneo mbali mbali si kwa maana ya kufanya utalii, lah hasha, bali ni kwa ajili ya kuomba msaada wa fedha na misaada mingine ya hali na mali kutoka kwa wasamaria wema ili kuweza kupata mahitaji yake kama binadamu awaye yeyote mwenye pumzi .
Bw. Kalenga ambaye siku zote ni mtu wa utani mwingi anayependa kucheka na kila mtu hata kama hamwoni amekuwa akipendelea zaidi kutembelea ofisi za chama cha waandishi wa habari mkoa wa Iringa (IPC) ambako amekuwa akifika kuomba msaada wa fedha kutoka kwa katibu mtendaji wa IPC Bw Frank Leonard ambaye amekuwa akimtania kuwa ni wajina wake na kama asingepata yeye mkasa huo basi yawezekana wasingefahamiana.
Kwa upande wangu niliweza kumfahamu Bw Kalenga kupitia katibu huyo wa IPC ambaye aliweza kujaribu kunieleza juu ya upofu wake kuwa ni ulemavu alioupata akiwa ukubwani hivyo hana njia nyingine ya kuendesha maisha yake zaidi ya kuzunguka mitaani kuomba fedha .
Japo Bw Leonard hakuweza kunieleza kwa undani zaidi juu ya mkasa wa kijana huyo ila kutokana na maelezo ya awali aliyonipa niliweza kufanya jitihada za kumtafuta mwenyewe ili kuweza kupata undani hasa wa kile kilichomsibu hadi leo hii kuwa katika hali hii ya ulemavu wa macho .
Bw Kalenga ambaye kama kawaida yake mara baada ya kukutana nami alionyesha kuwa mwenye furaha huku akitoa tabasamu la nguvu kwa kama vile amepata kuniona alianza kunitania kuwa ndugu yangu mwandishi kama ulivyojitambulisha kwangu ni vyema leo umekuja kuzungumza na mimi, kwani wapo watu wanapenda hata kunikwepa njia ili wasipate kujua maisha yangu.
“Ujue Bw Godwin Watanzania tulio wengi tumekuwa tukipenda sana kuchangia sherehe mbali mbali na misiba ila sio kumsaidia mgonjwa fedha za matibabu ama watu wenye shida kama mimi ….. hivyo najua utaandika na watu watasoma ila sina uhakika kama kweli nitapata kusaidiwa japo naweza kusema nayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu” anasema
Bw Frank kuwa toka amepatwa na mkasa huo ni zaidi ya miaka 5 sasa na siku zote amekuwa akizunguka mitaani kuomba na kuwashukuru wasamaria wema ambao wamekuwa wakinyosha mikono yao na kumsaidia chochote.
Akielezea juu ya mkasa huo ambao umemsababishia ulemavu wa maisha anasema ilikuwa ni mwezi wa 11 mwaka 2001 akiwa anatoka katika biashara yake ya kuuza vitunguu katika jiji la Mbeya ambako ndiko alikuwa akiishi kwa wakati huo alifika nyumbani kwake na kumkuta mke wake akiwa na mwanaume mwingine chumbani. Kabla hata ya kumuuliza ama kusalimiana na mke wake huyo alimpa panga mwanaume huyo kwa ajili ya kumuua.
“Kweli namshukuru sana mwenyezi Mungu kwani mara baada ya yule mwanaume kukabidhiwa panga na mke wangu alianza kunicharanga usoni na kichwani kama vile mimi ndiye niliyefumaniwa huku mke wangu akisaidiana na mwanaume huyo kutaka kuniua….nilikatwa mapanga mawili ya usoni usawa na jicho na kulia moja kisogoni na baada ya hapo walichukua kitu chenye ncha kali na kunitoboa jicho la kushoto ili nisiweze kuona kabisa wakijua kuwa nimekufa”
Bw Kalenga anasema kuwa baada ya kukatwa mapanga matatu usoni alianguka na ndipo mwanaume huyo na mkewe walipochukua fedha zote za biashara pamoja na mali nyingine ndani ya nyumba hiyo na kutoweka kusikojulikana hadi leo hii.
Baada ya kutendewa unyama huo alifungiwa mlango kwa nje kabla ya kukutwa na rafiki yake Bw Bahati ambaye alikimbia kutoa taarifa kwa mtendaji wa mtaa ambaye alilazimika kuvunja mlango ili kufanikisha kuokoa maisha yake pamoja na kumkimbiza hospitali ya Rufaa Mbeya kwa matibabu zaidi ya majeraha. Alichukua muda wa mwaka mmoja hadi 2002 aliporuhusiwa kutoa hospitali .
“Kabla ya kukutwa na mkasa huu mwanamke huyo nilipata kumfumania na mwanaume huyo kama mwaka mmoja hivi baada ya ndoa yetu ….kubwa lililofanyika hapo niliweza kumtoza faini ya ugoni na akatoa hivyo mara hii ya pili nafikiri akaamua kuniwahi kwa mapanga ili kukwepa kulipizwa faini tena”
Hata hivyo anasema kuwa mwanamke aliyetenda unyama huo anaitwa Nsiwe Sambonga mkazi wa kijiji cha Ibomba kata ya Rungwa Mbeya ambaye alipata kumuoa mwaka 1992 na kubahati kuzaa naye watoto 4 akiwemo mtoto mkubwa mwenye miaka 15.
“Hakika nachoweza kusema maisha yangu kwa sasa ni ya kubahatisha na nimekuwa nikiishi kwa nguvu za mungu kwa kuzunguka huku na kule kuomba msaada kwa ajili ya kusomesha watoto pamoja na kupata fedha za chakula. Hapa nilipo sina kazi wala sina ndugu wa kunisaidia chochote kwa ajili ya kuendesha maisha yangu”
Bw kalenga anasema kuwa kwa sasa amebahatika kumpata mwanamke ambaye ametafutiwa na wasamaria wema kwa ajili ya kumuongoza mitaani baada ya kukosa kabisa msaada wa mtu wa kumuongoza mitaani.
Pia mbali ya mkasa huu anasema kuwa baba yake mzazi alifariki dunia akiwa na miaka miwili huku mama yake mzazi akiishia kumtelekeza akiwa na mwaka mmoja na nusu na hivyo kuchukuliwa na baba wa kambo ambaye ndiye aliweza kumfikisha mkoani Mbeya.
Bw kalenga anasema kuwa pamoja na kuwa baadhi ya wasamaria wameweza kumsaidia kujenga nyumba yenye vyumba viwili na sebule bado anawaomba wasamaria wema kuweza kumsaidia mtaji wowote ili kupata fedha za kuendesha maisha yake badala ya kuendelea kuzunguka mitani kutafuta misaada kwa watu wasiojulikana.
“ Toka nimeanza kuomba kwa zaidi na miaka mitano sasa msaada wa maana ambao nimebahatika kupata ni ule wa kujengewa nyumba pamoja na kusaidia kuanzisha kigenge msaada niliowezeshwa na mzungu mmoja hivi ambao hata hivyo wezi walikuja kuniibia vitu vyote usiku “
Bw Kalinga anakuomba wewe msamaria mwema ambaye utaguswa kumsaidia kuwasiliana na mwandishi wa makala haya . Anapatikana kwa simu namba 0754 026 299 au 0712 750 199 barua pepe;francisgodwin2004@yahoo.com
Pia unaweza kutembelea :www.francisgodwin.blogspot.com










Mungu atamsaidia atapata tu msaada
yaani story yake inasikitisha sana ,dunia hii
inaunyama wa kila aina ,na huyo mwanamke na mwanaume waliomfanyia huo
unyama mungu atawaadhibu,yote mwachie mungu
pole sana ndugu yangu. hayo yote ni maisha. ninachokuomba usikate tamaa kwani mwomba Mungu achoki hivyo usijali my brother.
Swli ni kwamba Huyo mwanamke bado yuko hai?
pole sana ndugu yangu, ama kweli dunia ni mzunguko so usikate tamaa yuko aliyewekwa kwa ajili yako. endelea kuomba asubui, mchana na jioni ( kila saa)
Namuombea kwa MWENYEZI MUNGU aendelee kumpa NGUVU kwani ndio kitu cha maana ili aweze kuyamudu maisha ikiwa ni pamoja na kuwaendeleza watoto wake ambao baadaye watakuja kuwa NURU kwake na kwa jamii nzima !!!
Weka maoni yako hapa!
Maoni mapya
Zinatembelewa zaidi
Makala mpya
Habari zaidi
Burudani