JK hana dawa
Na Andrew Mushi
KWa muda sasa tangu nimekuwa nikiandika makala na mada nyingine katika vyombo vya habari , nimekuwa nikipokea maoni mengi sana kwa njia ya barua pepe, simu, ujumbe mfupi wa simu na hata ana kwa ana. Wengi wa wanaotoa maoni wanakimbilia kunyooshea vidole viongozi wa vyama vya siasa na zaidi chama tawala, na taasisi nyingine za utawala ndio wanawajibika kuchukua hatua ili kuleta mabadiliko na maendeleo ya nchi yetu.
Kitu kimoja kinachojitokeza wazi ni kuwa viongozi ndio wanapaswa kuwa wabunifu, kupangilia vizuri mipango ya maendeleo. Zaidi tegemeo limewekwa kwa Rais, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu na baraza la mawaziri na kwa mbali kidogo wabunge. Kwa mtizamo wangu, hapo ndio tunapokosea.
Mbaya zaidi, ni taasisi za kitaifa ndio zinazotazamwa kuwa ndio zenye nafasi ya kuleta mabadiliko. Taasisi kama kijiji, kata au hata wilaya hazionekani kuwa nafasi ya kuwa chachu ya kuleta mabadiliko tunayoyatamani kila kukicha. Pia, kuna asasi na taasisi kama makanisa, misikiti, hospitali, mashule, vyuo na nyinginezo nyingi zina nafasi kubwa sana katika kujenga jamii iliyo tayari kuhamia katika dunia ya kwanza.
Katika mawawasiliano yote hayo niliyotangulia kusema hapo juu hakuna nafasi anajipa mtu wa kawaida -yaani mimi na wewe, katika kuwa sehemu ya ufumbuzi wa haya masahibu yanayotukwamisha kusonga mbele kimaendeleo. Ninaamini kabisa, kuwa matatizo yanayotukabili yamesabishwa na mimi na wewe. Sio viongozi. Usianze kusema nimeongwa na mafisadi niseme hivi. Subiri nifafanunue. Kwa kifupi ni mimi na wewe ndio tunapiga kura. Tunaridhika na t-shirt na pilau ya siku moja, na kuwa radhi kusota kwa miaka mitano. Hili la pilau sitaliongelea leo.
Kwa kutumia nafasi aliyo nayo mtu mmoja mmoja katika kutumia mianya mingi iliyomo katka nafasi na sehemu mbalimbali tunamoishi, kufanyia kazi, kusali ua kuabudu, kusoma, kutembelea, tunaweza kuitumia ikawa chachu ya kupanga mipango mizuri ya maendeleo, kuwa na mitaala bora ya elimu itakayotupa uwezo mkubwa wa kupambana na mazingira yetu. Pia utaweza kuitumia kupiga vita na kuondoa ufisadi, rushwa na uchafu mwingine wowote katika jamii yetu.
Nitajaribu kutumia mifano halisi zaidi kuliko kuongea kinadharia ambayo itakuwa ngumu kueleweka. Kuna walimu wameweza kuleta mbadiliko makubwa na kutisha katika shule zao bila kusubiri wizara ya elimu au Taasisi zinazomiliki hizi shule. Mfano mzuri ni shule za sekondari za Jitegemee na Makongo za Jijini Dar Es Salaam. Jitegemee inamilikiwa na Jeshi na Kujenga Taifa na Makongo inamilikiwa na Jeshi la Wananchi. Miaka ya 1980 hizi shule zilikuwa ovyo kabisa. Mkuu wa shule ya Jitegemee Kanali Massawe aliweza kuwa mbunifu akaigeuza Jitemee ika shule inayofaulisha sana na kubwa na tena yenye mazingira bora ya kusomea. Kanali Kipingu naye alifanya Maajabu Makongo mpaka ikawa inatisha. Hawa wakuu wawili wa shule hawakuishia kuulaumu uongozi wa Jeshi-waliamua kuwa wabunifu.
Miaka ya 1993-96 alisoma bwana mmoja pale Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam. Anaitwa Emmanuel Makundi, huyu jamaa alikuwa anapenda maua sana. Mbele ya chumba chake akaotesha maua pakapendeza sana. Aliishi chumba cha chini na si ghorofani. Wakati huu ndio mazingira ya chuo yalikuwa yameharibika sana na hayatunzwi vizuri.
Wakati anakaribia kumaliza masomo mwaka 1996 Uongozi wa Chuo ukamuuliza amewezaje kutunza maua na mazingira yakapendeza hivyo. Kwa kifupi akawa amepata mwanya wa kuwasimulia na kuanza kushirikiana na uongozi wa chuo. Kwa hizo jitihada za Makundi ulianzishwa mradi mkubwa sana wa kuotesha maua na miti pamoja na utunzaji wa mazingira pale Chuo Kikuu. Bahati nzuri huu ndio wakati pia chuo kimeanza mkakati maalumu wa kuboresha majengo ya chuo ili kiweze kuchukua wanafunzi wengi zaidi.
Ili kuweka mambo vizuri zaidi, kwa kushirikiana na wanafunzi wengine pamoja na chuo wakaanzisha asasi ijulikanayo kama JEMA- Joint Environmental Management Action. Taasisi kwa kushirikiana na chuo kikuu walibadilisha mazingira ya chuo yakawa ya kupendeza na kuvutia sana. Kama Makundi hakuona mwanya na kuchukua hatua ninaamini, labda ule uoza wa Chuo Kikuu wa katikati ya miaka ya 1990 ungekuwepo mpaka leo.
Kwenye miaka ya 1980, kijiji cha Nronga Wilayani Hai kilipoteza watoto watatu kwa kuzama mtoni wakati wakienda kuuza maziwa katika kijiji cha jirani cha Foo. Kijiji cha Nronga ni wafugaji wakubwa wa ng’ombe wa maziwa. Kati ya hivi vijiji viwili kuna mto mkubwa sana, ambao wakati wa masika hufurika. Kuona hivyo akina mama wakasema hatuwezi kukubali watoto wetu waendelee kufa. Wakaanzisha ushirika wao wa kuuza maziwa. Huu sio sawa na ule ushirika ambao serikali inasisitiza vijiji vianzishe. Ni ushirika uliotokana na watu kuamua wenyewe kwa kuona shida na mahitaji yao.
Wakawa wanakusanya maziwa yote kijijini wakaenda kuuza Moshi mjini na Arusha. Leo hii huu ushirika una wanachama zaidi ya 400 na hata vijiji vya jirani wamejiunga nao. Sasa hivi kijiji kina uhakika wa soko la maziwa na hali za wanakikiji ni nzuri sana. Kuna mtu alipata kunisimulia juu ya hiki kijiji, kwamba nyumba za wanakiji zote ni za matofali na kuezekwa kwa bati.
Cha kufurahisha zaidi, wameanzisha mpango ambapo watoto katika shule mbili za Msingi hapo kijijini, shule za Naluti na Nronga, wanakunywa maziwa mara mbili kwa wiki. Tangu wameanza kunywa maziwa, maendeleo yao darasani yamekuwa mazuri sana. Hii ni kwa mujibu wa Hellen Usiri, Mwenyekiti wa huu ushirika wa kina mama. Pia watu waliotembele hiki kijiji wanathibitisha hili.
Kuna huyu Mbunge Zitto Kabwe. Kabwe tangu anasoma Chuo Kikuu cha Zanzibar na baadaye kuamia Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam alisimama imara kupiga vita uoza ndani ya Chuo na hata ndani ya Umoja wa wanafunzi, yaani DARUSO. Kwa kuelewa ujasiri wa Zitto, Wananchi wa Kigoma Kaskazini wakampa ubunge katika umri mdogo tu wa miaka 29 . Na mpaka leo kila mtu ni shahidi kuwa wananchi wa Kigoma kaskazini wamelamba dume.
Nimalizie kwa kusema ndani ya makanisa, misikiti, vijiji, kata, baraza la madiwani, mashuleni, NGOs, vyuonm, viwandani, Mitaani tunao akina Zitto wengi sana wa kuung’oa uovu. Usiogope, chukua hatua na utashangaa utakavyopata jeshi kubwa nyuma yako. Akina mama wa Nronga wametuonyesha inawezekana, kina mama na vijana tuamke.
Pia tunao kina Makundi na Kipingu wengi sana ambao ni wabunifu na wanaweza kubadilisha sehemu mbalimbali na kukawa na mabadiliko makubwa sana. Tutazame ndani ya nafsi, dhamira, roho, na akili zetu. Kuna chachu Mungu amekuwekea ndani yako, ukiitumia vizuri na mimi nisipojidharau, tutaibadilisha Tanzania. Sio mafisadi, wala wenye akili mgando watakaoweza kutuzuia. Sijakata tamaa, na najua wewe hujakaa tamaa. Tuamke, tukaze buti na tusonge mbele. Tusimsubiri Rais Kikwete, hatutafika!
amushi1@yahoo.com










Hii ni kweli tupu. Mwenye majibu na dawa ni mimi na wewe. Asante ndugu Mushi kwa changamoto hii.
Wasalaam, Musa
Kwamba nimefikwa na ujumbe wako huu bila ya shaka jina na anuani yangu si siri kwako. Kisingi nakubaliana na wewe kwamba mabadiliko ya nchi hasi au chanya yanachangiwa kwa kiasi kukubwa na wanancho wenyewe.
Ni maradhi ambayo nitayaita hapa katika kukuunga mkono kuwa donda ndugu ambalo rutuba yake kubwa ni ubinafsi. Ni pale tunapokuwa na watu wasiojali wengine, wanaodhani wao pekee ndio wanaostahili na kwamba upinzani ni kasoro tupo tunapojikuta katika hali hii ya kutoweza kupiga hatua.
Jingine kubwa na ambalo naafikiana nawe ni kuwatumia watu mintaarafu karama zao. Kipingu alikuwa turufu katika kuongoza shule na hata kuibua na kuipua vipaji vya vijana katika soka. lakini sidhani ni mwenye ufanisi hivyo baraza la michezo la taifa kwa nini? watu anaoshirikiana nao na je alikuwa na taswira yoyote akiingia huko?
Matumizu mabaya ya karatasi za kura kwa maana ya ufahamu mdogo wa wananchi wa maana ya kupiga kura ni tatizo kubwa saana lakini pengine unafiki, wizi na udanganyifu katika hilo ndio unaodumaza hata akili madhubuti na kukatisha tamaa waja kuendelea kuwa na imani na sanduku la kura kama njia ya kubadilisha uongozi na pengine kuiimarisha demokrasia.
Jingine kubwa kuliko yote kwangu ni nchi kukosa ajenda zilizo wazi za kitaifa. Harueleweki tunakwenda wapi sasa, tutakuwa wapi baada ya 2010 na hali itakuwaje 2015. Utawala kwa mawazo yangu umnejaa dhahaka na maisha ya watanzania kiasi ni kama wanaofanya uongozi kwa mtindo wa mchezo wa kuigiza wakiamini kwamba utafika wasaa wa pazie kufungwa na waja kurejea katika maisha yao ya kweli.
Nina mengi na usongo lakini niishie hapa tu kwamba watanzania tunahitaji ukombozi mkubwa ambao Nyerere aliuzingatia ukombozi wa kifikra.
NAHITIMISHA
Rais ana sehemu kubwa ya kuleta mabadiliko kwa kuhimiza yale anayotaka yafanyike na kujua matakwa ya watazania anaowaongoza. Vilevile anawajibu wakuthubutu (to risk) kuhakikisha mabadiliko ya kweli yanafanyika mara moja.
Inampasa kukemea na kuwawajibisha viongozi wabovu mara moja. Hata kama watashtakiwa baadaye, maramoja kiongozi anaposhukiwa lazima ajisafishe au aachie madaraka. Si hivyo anaponyamaza kimya viongozi wazuri hawana mahali pa kusimamia kutiwa nguvu kuijenga nchi yetu. Vilevile jina la Rais linanenewa vibaya na ukweli unashindwa kujidhihirisha.
Hao wakuu wa shule za jeshi walisimama katika nafasi zao kama viongozi. Na kiongozi maana yake kuwa wa kwanza, kuona mbali, na kufanya maamuzi kwa manufaa ya umma sio kwa kutafuta faida ya wachache. Rais vilevile ni lazima asimame kwa dhahiri kabisa, bila woga mashaka walasubira kukemea, kuwajibisha bila kuangalia uso wa mwanadamu, kinyume cha hapo ni kucheza na muda tu kabla mtu mwenyewe k.m mkuu wa shule, mkurugenzi kuonekana mzaifu katika kuongoza.
Ndugu Mushi,
Napenda kukufahamisha kuwa huwa ninapataga fursa za kusoma uchambuzi wako makini na wengine kama Richard Mabala ambaye hupenda kutumia lugha ya fasihi. Kwa muda mrefu nimekuwa naishia kusoma na kujadiliana na wale niko nao karibu. Mara chache nimechangia mijadili ya FCS kupitia mail list yao ila sijaona impact.
Kwanza nakibaliana na wewe kuwa kila mmoja wetu anyo nafasi ya kufanya kama tumewezeshwa kufanya hivyo. Mimi na wewe na John na Febe tuko wengi ila hatujatumia nafasi zetu vizuri. Ni kweli hatuna haja ya kukata tamaa na kusema mabadiliko lazima yaletwe na viongozi wa juu. Ni wajibu wa pamoja. Ijapokuwa tutatofautiana kwa kuleta matokeo, lakini ni heri kuanza kufanya kidogo chako kwani wahenga husema, “Bandu bandu humaliza gogo”. Tusonge mbele kuendelea kulibandua gongo na hakika litaisha. Asante. Nico
Kaka Andrew Mushi,
Hongera kwa kuamua kuingia katika vita sahihi ya kujengea Watanzania fikra sahihi za kubadilisha maisha yao ili hatimaye tuweze kujenga taifa ambalo halina aibu ya kuomba wafadhili fedha za kujenga choo au shule/hospitali/barabara/ au fedha za matumizi nyumbani mwetu. Tuwe taifa lenye hadhi (integrity) kwa sababu Mungu katupa mali nyingi na watu wenye akili na uwezo mkubwa wwa ubunifu.
Hayo uliyoyazungumza katika makala yako hii ni ukweli mtupu na hicho kijiji cha Nronga unachokitaja nilizaliwa huko miaka 50 iliyopia na hakika ingawa kwa zaidi ya miaka 30 sijaishi huko, lakini maendeleo uliyoyataja na chanzo chake ni dhahiri nami nafahamu. Tena niongezee wakati mimi nikiwa mdogo wakati wanakijiji wa Nronga hawajajitambua kuwa maendeleo yao yataletwa na wao wenyewe na si Misaada kutoka Ughaibuni au serikali, wanafunzi wengi wa shule ya Msingi (mimi mwenyewe nikiwa mmoja wapo) tulikuwa tunakwenda shuleni peku peku bila viatu kutokana na umaskini wa kipato. Leo fika Nronga kijijini shule zote za Msingi na Sekondari hakuna mwanafunzi anayetembea peku peku wala kwa ndala shuleni bali kila mmoja utamkuta kavaa viatu na yote hayo yanatokana na ushirika wa Maziwa maana kahawa si mali tena tangu ilipoingiliwa na na ugonjwa wa CBD na soko lake kuyumba. Lakini pia shule zote za Nronga kijijini (mbili za Msingi na mbili za Sekondari ) na zahanati zimejengwa kwa nguvu za wananchi. Wananchi hao hao wanaikarabati barabara yao ili ipitike kila wakati. Wasingekuwa wanachukua hatua wenyewe hata kwa mambo makubwa ambayo kimsingi ni jukumu la serikali/Halmashauri leo wangekuwa ni muiongoni mwa vijiji maskini vya kutupwa. Lakini naamini Nronga ni moja ya vijiji vya mfano wa kuigwa Tanzania nzima kwa mambo mengi. Lakini nisema maendeleo hayo ya Nronga hayakuja bila uongozi imara wa huo ushirika wa Mazima na uongozi wa kijiji na madhehebu ya dini. Kanisa la Kilutheri Usharika wa Nronga unahimiza sana maendeleo kijijini. Unaamsha watu wafanye kazi, watu wafikiri. Kiongozi akiyumba anakemewa hawasubiri kusema usichanganye siasa na dini. Kwenye watu dini na siasa vyote vina mchango. (ile makala yako iliyopita Mushi naihunga mkono pia). Jambo ninalolisema hapa ni kwamba hakuna umaskini mbaya kuliko umaskini wa fikra. Mtu akiwa na umaskini wa fikra anajiona dhaifu na haoni rasilimali alizo nazo ikiwa ni pamoja na kura yake katika kushinikiza viongozi wafanye kazi za maendeleo ya wananchi. Ni umaskini wa fikra ndio umewafanya wananchi kugeuzwa kama nganya na dagaa za kununuliwa/ kutishwa wakati uchaguzi unapokaribia badala ya wananchi kuwa fimbo kali ya kuadabisha viongozi wote ambao watakuwa hawakutimiza ahadi zao. Tuna kazi kubwa mbele. Lakini naamini kwa fursa hizi za kushirikishana mawazo kupitia vyombo vya habari fikra mpya zitajengwa miongoni mwa Watanzania na nchi yetu tutasonga mbele kwa kishindo. Hongera kijana songa mbele na endelea kuchambua mada kwa mifano kama hii. Imesomeka na kueleweka.
Kaka Andrew,
Asante kwa makala nyingine, yenye mifano na uchambuzi yakinifu. Nawaunga mkono wote waliotangilia. Lakini napenda kusisitiza Rais kama kiongozi tuliyemchagua anasehemu muhimu sana katita kufanya maamuzi yatakayo leta mabadiliko. Hii aimaanishi wananchi wabweteke, laaa!! Ni lazima kuweka juhudi katika kuanzisha, kufuatilia na utekelezaji, hapa ndio tutaweza kusema nani kalala na hakutimiza wajibu wake.
Lakini jamani, wakati mwingine hawa wananchi wanahitaji taarifa muhimu/kuelimishwa ili waweze kujenga nguvu za pamoja na zaidi ya hayo kupata viongozi wenye ujasiri wa kutamka bila hofu na wasiojali maslahi binafsi ili wasonge mbele.
Sasa hawa viongozi wako wapi? AU wakishatishiwa kidogo wananyamaza kimya? Au ni “Nguvu za soda” na zitaendelea hadi lini? Na wanaharakati na wasomi katika taaluma mbalimbali mnafanya nini?OK….wanapiga kelele na kutetea halafu? mnaachia hapo?? Mnasubiri hadi issue nyingine iibuke tena ndio nanyi muinuke??
Asante Andrew kwa kuibua mijadala muhimu kama hii, inayotuwezesha kujichambua wenyewe.
Ndugu Mushi, nina kila sababu ya kukupongeza kwa kuamsha hisia za watu wengi wanaotaka maendeleo na wanaokerwa na hali yetu ya umaskini katika nchi iliyobarikiwa! Nimepitia makala yako na maoni ya wote waliochangia kwa makini na funzo kubwa nililolipata ni kuwa matatizo yetu tunayafahamu na tunajua namna ya kuyatatua. Kwa nini tunachelewa kuyatatua na kwa nini katika baadhi ya maeneo wameweza na maeneo mengine bado hilo ndilo eneo la kujikita. Mifano hai uliyoitoa na mingine aliyoitoa dada Nkya kuhusu kijiji cha Nronga ndiyo majibu halisi ya matatizo yetu. Majibu yako kwetu wenyewe mtu mmoja, kama kikundi, taasisi na jamii kuanzia pale tulipo ama kama watumishi kwenye sekta ya umma au sekta binafsi.
Ziara za mafunzo kwenye maeneo yaliyofanya vizuri kama kijiji cha Nronga na katika mashule kama yaliyotajwa ni njia mojawapo muhimu ya kubadilisha fikra na kuleta chachu ya maendeleo. Wakati umefika wa kila kijiji sasa kujipangia ziara hizi za mafunzo (study visits/tour)katika mipango yao ya maendeleo ambayo kila mshiriki atachangia angalau asilimia 50% na akirudi aanze utekelezaji utakaofuatiliwa na Uongozi wa kitongoji na kijiji/kata husika
Tanzania kwa hakika tuna hazina kubwa ya Rasilimali watu - tukishirikiana tutaweza kufikia malengo
adam swai
Weka maoni yako hapa!
Maoni mapya
Zinatembelewa zaidi
Makala mpya
Habari zaidi
Burudani
Makala mpya
Zenye maoni mengi
Zinazotembelewa zaidi
Counter:347,505
Maintained by Daima Solutions | Log in | Entries (RSS) | Comments (RSS) |