Mheshimiwa Pinda: Ya ‘ Ze Comedy’ tuwaachie kina Joti na Masanja
Na Andrew Mushi
OKTOBA 22 mwaka jana, Waziri Mkuu , Mizengo Pinda (MP), alitembelea Wilaya ya Hai , Mkoa wa Kilimanjaro, pamoja na shughuli mbalimbali alizofanya , alisomewa taarifa ya Wilaya.
Taarifa inafikia zaidi ya kurasa arobaini. Nasema zaidi ya 40 kwa sababu sikupata nakala halisi ya hii taarifa ila nimetumia iliyoko katika mtandao wa tovuti (wavuti), ambapo nilipojaribu kuiweka katika kurasa za kawaida ilifikia kurasa 50.
Wakati nasoma hii taarifa , niliwaza juu ya hotuba na taarifa mbalimbali viongozi wanazosomeana na kutusomea (kuhutubia). Mojawapo ya nilichokiwaza sana , ni kama kweli hii hotuba yote aliyosomewa Waziri Mkuu na Uongozi wa Wilaya ilichukua muda gani kumalizika? Na je, Waziri Mkuu hakusinzia, ingekuwa mimi nina uhakika ningelala fofo na kukoroma.
Mawazo yaliyonijia ndio ninataka kujadili na wewe ndugu yangu unayesoma makala hii. Najua utakuwa na mengi tena zaidi yangu ambayo umekuwa ukiwaza na kuwazua.
Kila siku ijayo kwa Mungu , Tanzania kuna hotuba na risala nyingi zinasomwa na wananchi kwa viongozi wao, na viongozi nao wanapokea hii ngonjera kwa kuwatolea ngonjera yake. Basi hali mradi tumefungua kinywa kusema chochote. Siku unajua tena hizi ni zama za semina elekezi. Kama zisingekuwa ngonjera, tungekuwa tuko mbali.
Kuanzia Rais Mpaka Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wanazunguka huko na huko kukagua na kuhamasisha shughuli za maendeleo , na kila mmoja anasoma na kupokea risala. Sasa cha kuchekesha ni huu mchezo ninaouita ‘Ze Comedy’ ya hizi hotuba.
Kwanza hizi hotuba ni zile zile, nikitumia mfano wa ile hotuba ya Hai, akija Rais kesho atasomewa hiyo hiyo, Mkuu wa Mkoa naye akija hiyo. Akija waziri wa wizara yeyote ile vitanyofolewa vifungu vyake na kusomewa, Mwenge ukija nao ndio usiseme. Kwa kifupi kinachofanyika ni kubadili tarehe na mlengwa.
Mara nyingi hatujiulizi umuhimu wa hotuba mbali mbali tunazosomeana katika shughuli mbali za kisiasa na maeendeleo. Mara nyingi hizi taarifa ndefu ni mazoea yasiyokuwa na tija wala hayatupeleki popote.
Ndio maana ukifika katika hizi shughuli wakati wa kusomeana hizi hotuba na taarifa kwa wastani hakuna anayesiliza, ndio maana nikaziita ze comedy. Tena afadhali ya ‘Ze Comedy’ inaburudisha, tofauti na hizi hotuba zinazoumiza na kuchosha masikio.
Mara nyingi nimesikia watu wakiwalumu Wabunge kwa kusinzia Bungeni, ila mie nimekuwa mzito kuwalaumu, kiasi fulani, naelekea kuwaunga mkono. Wewe niambie unaposikiliza bunge letu, ingekuwa ni wewe ni kitu gani kingekufnaya usisinzie. Kama ni hotuba ya bajeti, unajua Waziri alichosema mwaka juzi na mwaka jana ndio atakachokirudia.
Kama anajibu swali, hataenda mbali zaidi ya ile story ya siku zote kuwa barabara ‘korofi’ ya kwenda ‘Busanda’ au ‘Biharamulo’ inashughulikiwa, na Mheshimiwa Mbunge avute subira, sasa akivuta subira kwa kulala kidogo ana kosa gani-embu tuacheni kuwaonea Wabunge.
Wewe ona kunapokuwa na mijadala motomoto kama wakati wa kujadili Richmond mwezi Febuari mwaka jana, nani alisinzia-hamna!
Kwa wanaomjua Rais Museveni wa Uganda, akiwa katika shughuli na mtu anatoa hotuba au longolongolo, yeye hufumba macho na hata ikibidi husizia kabisa. Ukiona hivi,ujue anakuambia kama huna cha maana cha kusema ishia hapo. Mapema Febuari mwaka huu, Rais Gaddafi wa Libya alipochaguliwa Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika alitoa hotuba ndefu sana iliyoenda mpaka usiku wa manane. Marais wengi wakasinzia. Ila yalipomshinda Museveni, alimfuata Gaddafi jukwaani, akamwambia maliza, tunataka kwenda kulala. Naye akawa mpole, akamaliza.
Tuyaache ya Museveni turudi kwetu. Cha kuchekesha zaidi, mara nyingi wanaosomewa hizi hotuba ndio wao wameziandika. Nikupe data kidogo. Mfano, kama Waziri fulani amealikwa kuwa mgeni rasmi katika shughuli iliyoandaliwa na NGO fulani. Ile NGO itaandaa hotuba mbili, moja ya kwao ya kumsomea mgeni rasmi, na nyingine ya mgeni rasmi kwa ajili ya kujibu ile ya kwao, ila yeye atamalizia kwa kusema, natangaza , washa hii imefunguliwa au imefungwa rasmi. Makofi, kisha kila mmoja atatawanyika kwenda kusubiri hotuba nyingine.
Sasa niambie, katika hali kama hii, huyu waziri anawajibika kutekeleza nini katika hotuba ambayo hakuiandaa. Sidhani, hata kama ukimuuliza kesho yake, katika ile hotuba nini alichosema, kama atakuambia-hakumbuki!
Hali haishii hapo tu. Katika hizi hotuba zinazosomwa zisizokuwa na miguu wala kichwa, kuna utamaduni wa kulipwa posho kwa kufanya hiyo shughuli nzito ya kuhutubia. Huu mchezo uko kwa mawaziri mpaka viongozi wa ngazi ya chini kabisa. Nina uhakika, Rais, Makamu wa Rais, na Waziri Mkuu hili hawahusiki. Ila mawaziri, makatibu wakuu, wakurugenzi, maofisa, bila bahasha hajakufungulia au kukufungia warsha yako kama hana uhakika wa bahasha.
Kama huamini, kamuulize mtu yeyote aliyekwisha kuandaa warsha au kongamano. Mbaya zaidi, wengine wanauliza bahasha yangu ina bei gani, akiambiwa bei ni ndogo hasemi ongeza, ila anasema siku hiyo atakuwa na shughuli nyingine, atamtuma mtu wa ngazi ya chini (wa bei hiyo), na unajua ukipata wa ngazi ya chini na shughuli yako itaonekana ya chini, hata kwenye TV haitoki.
Mimi nashawishika kusema tumeongea na kusundubua sana, inabidi tubadilishe hii tabia, tena sio tabia tena, bali imeshakuwa ni utamaduni. Tuwe na hotuba zinazoruhusu kushikishana na kujadiliana zaidi. Na kama ukiamua kuyapa tafsiri sahihi ya yanayotokea sehemu nyingi za Tanzania, utagundua wananchi wako mbele hatua moja zaidi ya viongozi. Sidhani kama inaisha wiki bila vyombo vya habari kutueleza kiongozi huyu au yule amezomewa .
Hii kuzomea zomea, wakati mwingine sio kuwa wananchi hawataki kusikia kiongozi akiongea, la hasha! Wanataka staili mpya ya kuongea. Hawataki hotuba, wanataka mazungumzo na mijadala. Uzuri wa mazungunzo na mijadala, mara nyingi inapelekea pande zote zilizoshiriki kuchukua hatua. Upande wa hotuba , unapoweka nukta, na ndio mwisho wa kila kitu.
Wananchi wanataka kujadiliana ili kujua njia za kutatua matatizo yao ya kila siku. Hii mara chama changu, shirika langu, litawafanyia hivi au vile, litawaletea hiki, hawataki, maana licha ya kujua ni kuwazuga tu, wanajua hata mwenyewe humaanishi unachoongea. Japo mdomo wako unakitamka, wakikuangalia usoni, wanaona sura na macho yako yanakana mdomo ulichotamka.
Nina uhakika Waziri Mkuu anaweza akafungulia njia na kutuletea njia mbadala katika hizi hotuba na taarifa. Kwa watu wanaomjua Mh. Pinda, watakubaliana na mimi kuwa sio mtu wa longolongo na haendekezi longolongo. Na ninamsikitikia sana anavyoweza kusikiliza hizi ’Ze Comedy’ kila siku. Najua anajionea kero tu.
Pinda siku zote amekuwa ni mtu wa maneno mafupi lakini yenye vitendo. Nina uhakika akipania tunaweza ndani ya muda mfupi tukajikuta tunaacha kupoteza muda na kuchoshana. Tukajikuta tunakuwa na utamaduni mpya wa kupeana taarifa na mipangilio ya kazi bila maneno mengi yasiyo na kichwa wala mkia.
Kwangu huu ni ufisadi. Kila siku tunafikiri ufisadi ni kukwapua pesa za EPA na Richmond tu. Hapana, ni pamoja na huku kuchorana katika hizi hadithi za akaenda, akaenda, akaenda… na hadithi yangu ikaishia hapo.
Nani hajui, huduma za afya, elimu, barabara, na nyinginezo hazitoshi. Kwa nini kurudia rudia maneno kama kasuku. Tutumie muda mwingi kupanga mipango inayotekelezeka, ya ’Ze Comedy’ tuwaachie kina Joti, Mpoki na Masanja.
amushi1@yahoo.com










Ee bwana Mushi,
Kwa kweli hata mimi hizi hotuba zinanikera mno! Lakini zaidi ni hii protokali ambayo watanzania wamejiwekea kuanzia ngazi ya chini hadi ya juu. Kiongozi ananyenyekewa kama mungu, hata pale anapokuja amechelewa au anapozungumza utumbo mtupu! Hakuna wa kuhoji na anongezewa heshima na ukitokea kuhoji wenzio wanakuona mwanga!
Huu utaratibu wa kumwandikia mgeni mliyemwalika hotuba nafikiri tunapaswa kuachana nao, ni ujuha wa hali ya juu! Kwanza tunawalemaza viongozi wetu- hawana haja ya kujiandaa kwenda kwenye warsha, semina, mikutano, makongamano n.k kwa kuwa tunawaandalia majibu sisi wenyewe!
Nilipata kuandaa workshop pale Impala Hotel Arusha nikamualika mkuu wa mkoa, sikumwandalia hotuba basi karibu asusie ufunguzi! Na kuna Waziri mmoja (alitupwa nje na JK) huyu alikuwa hajibu maombi yako hadi umhakikishie msaidizi wake kuna bahasha ya Mzee! Eti naye alikuwa kundi lile la G55!
Halikadhalika, mimi nafikiri umefika wakati wa kubadili mfumo wa kutawala hasa katika suala la uwakilishi. Mfumo tulionao sasa una gharama kubwa na unatumika vibaya. Hivi kweli hakuna njia nyingine ya kuwasilisha matatizo/maoni/matakwa ya wananchi bila kuwa na Bunge? Mimi naaimini mbunge anapowania jimbo anakuja kwa wananchi ili awe mtumishi au mwajiriwa wao, sasa inakuwaje mtumishi / mwajiriwa akishapata kazi anajipangia mshahara na marupurupu yeye mwenyewe? Wajimeni, hapa tunaliwa! Tunao wasomi kedekede, haiowezekani kila kijiji kikawa na wataalamu watakaotayarisha bajeti ya kijiji na kuwasilisha wilayani, mkoani na hatimaye serikali kuu? Huko kote kuna wataalam waliobobea. Serikali isipotekeleza bajeti za vijiji/wilaya/mkoa inawajibishwa kupitia sanduku la kura (isiyokuwa na wagombea wa ubunge).
Ni mawazo yangu tuu, lakini huko tuendako, Bunge litakuwa mzigo wa mwendawazimu unaoishia mabegani!
Chakushangaza ni pale wanapotoa takwimu za maeneo ambayo hawajawahi kufika. Takwimu hizi huptikana kwa watendaji wa kata ambao nao hupewa na watendaji wa vijiji ambao walipewa na wenyeviti wa vitongoji walioagiza mabalozi waziandae na mabalozi wakaziandaa majumbani mwao kwa kukisia kuogopa lawama.
Hujawahi kusikia msafara wa Lowasa ulipotea njia huko Tabora? Kwani wewe hujajua kwanini siku hizi kuna askari kila inapochepukia njia? Kutoka Boma hadi Moshi mjini siku anayopita mkubwa utakuta askari zaidi ya arobaini. Wanafanya nini ? Wanalinda msafara usipotee njia. Kweli !!!!!!!!!!!!!! Kwani mkuu wa wilaya hajui wanakokwenda au ni mgeni kila siku?
Ama kweli ukistajabu ya Richmond utaona ya L………….!
Asante ndugu Mushi kwa kutuelimisha. haya mambo ya hotuba yanatakiwa yaishe. Yanatupotezea muda muhimu badala ya kufanya kazi za kuleta maendeleo. Natumaini baadhi ya viongozi watasoma hii nyambulishi wabadilike.
Kimsingi mfumo wa utoaji taarifa tulionao haupo kwa mantiki ya uhalisia wake. Kama ulivyoainisha bwana Mushi kwa maneno mengine ni kama mchezo wa kuigiza. Penginepo kuhitimisha na kuonyesha mkuu alifika mahali hapo. Kwa kuwa tunaona hili ni tatizo basi tuzungumizie na namna ya kulitatua. Nimefanya tafiti katika wilaya fulani kwa kama mwaka na nusu.Ushahidi ni kwamba kila kitu watu wa wilayani, kata, vijiji,, shina, kila kinachofanyika kinategemea na nani [kiongozi gani] atakuja. Watu watabiidika kwa yule anae kuja ili aandaliwe “taarifa” kwani hicho ndicho wanaona cha msingi. Na wao wamekuzwa kwa mtindo huo. hili linaitaji kuvunjwa. Mara nyingi walikua wanalalamika wakiniambia kuwa jamaa wanatoa taarifa gafla na kila mmoja anakuja anataka taarifa. Utasikia mara waziri wa kilimo aja kesho, mkuu wa wiliya ijumaa, mkuu wa mkoa j3, mwenyekiti wa halmashauri jumane, mkurugenzi wa tasaf wiki ijayo, mwenyekiti wa NGO fulani leo, sijui mwenyekti wa chama tawala kanda keshokutwa…na mlolongo waendelea.
Njia nzuri ni kuangalia historia ya mifumo ya utoaji taarifa. je ni lazima waziri mkuu au kiongozi mwingine akija mahali lazima apewe taarifa? hii imetoka wapi? hakuna mfumo wa kumpa taarifa waziri kuhusu eneo fulani kabla hajaenda huko? Taarifa za serikali za wilaya haziendi taifa? kwa nini bwana Pinda asiwe hata na ka “blackberry” while en route huko anasoma ripoti akifika huko waweke mjadala wa kujua lipi halijafanyika na kwanini, na aoneyshwe kwa vitendo hivyo vinavyodaiwa kufanyika?
Mimi hua na admire sana mifumo ya watu wa nchi za scandinavia mathalani Denmark [angalau na idea nako]. Hawa jamaa katika kila kikao cha halmashauri zao pale wanapo kaa madiwani wananchi wanaruhusiwa kuingia na kushuhudia wanavyojadiliana na kutoa maamuzi. Rai yeyote wa eneo anaweza kwenda halmashauri na kuomba taarifa za halmashauri, tena sio kuomba, hua zimewekwa pale reception unafungua kabati unasoma kilichoandikwa. Kama hujaridhishwa na kitu, mtu mmoja anaweza kwenda akamuona muhusika akamuuliza au kumwambia hakupendezwa na jambo fulani na akasikilizwa. Kwetu wanasema taarifa ni “Siri kuu”!!!. Kwa mtindo huu kama wa wenzetu nafikiri hata vioingozi wa ngazi za chini wangekua na taarifa safi na WAziri akija atakua anashugulika na mambo ya msingi, pengine yale yaliyo juu ya uwezo wao. Mfumo wetu hauko wazi hivyo unapelekea “ufisadi” huo, kama bwana Mushi alivyo ainisha.
Naomba kuwakilisha.
Bwana Mushi,
Uliyoyasema ni kweli, na ni wakati muafaka kwa viongozi wetu kuwajibika kwa wananchi. Asante sana kwa kutufungua macho maana wengi tulishalaa kwenye ufunguzi na ufungaji wa shughuli mbalimbali, na pia kushuhudia uandaaji wa Speech za wageni rasmi. Eti hawana muda wa kujiandaaa, hivyo wakifika wasoma tu na ndio imetoka hivyo….Lakini sasa si wangeongeza basi tamko la serikali kuhusiana na warsha au shughuli hiyo, lakini wapi!!!!…. Watanzania wamechoshwa na ahadi za “uongo”. Nasema uongo kwa sababu hakuna ufuatiliaji wala utekelezaji kutoka ngazi zinazohusika.
Sasa nini kifanyike: Pengine ni jukumu letu sisi wananchi kuendelea na mijadala hii inayowakumbusha watendaji kutimiza waliyoyasema–Naamini hii itawafanya kuona aibu na kuwajibika zaidi huku wakielewa kuwa wamepewa dhamana ya uongozi na wananchi waliowaamini la sivyo waachie ngazi!!!!. Pia tuendelee kuandika, kuipasha jamii na hata viongozi habari pindi tunapogundua “Hizo staili za commedy wanazotumia waheshimiwa”. Hii ita-demand accountability hata baada ya nukta kuwekwa katika hotuba. Kwa waandishi wetu wa habari na wachambuzi wa sera hii ni changamoto ili mweze kuweka mambo wazi na kuelimisha jamii. Msiogope magazeti kufungwa laaa….Ukweli ni ukweli tu bwana……Na kwa vyama vya kiraia- CSOs/NGOs/ CBO n.k amkeni kufuatilia
Hiii Mushi!
Nadhani mambo haya yanatuuma zaidi. Lakini sababu kubwa ni kwa kuwa viongozi waliopo ni wale wale na watendaji wa ngaji za juu ni wale wale. Kwa hiyo! Waandaaji wa hotuba za maendeleo wanafahamu BWANA MKUBWA ANATAKA KUSIKIA WIMBO UPI LEO….Then wanaandaa wimbo huo na mashairi kwa kuweka vina vinavyoimbika vizuri. Ndo maana inakuwa “slash ‘n burn …cut ‘n paste”.
Kwa muda wa miaka 14 sasa nimefanya kazi kwenye NGOs (mostly international), lakini nilibahatika kuongoza miradi ambayo ilipata kufunguliwa na mbio za mwenge! Unafahamu nini? Kila maa hotuba zilipokuwa zinasomwa, wananchi wanahoji hizo hela zilizotumika kujenga mashule, madaraja, barabara, zahanati mbona kwenye karatasi zinaelezwa kuwa nyingi wakati wananchi hawakuzishuhudia zikiletwa au kutumika. Hizi zote ni SI-HASA!
Ninachosema hapa ni kwamba, endapo jamii ityapata fursa ya kuwahoji watendaji na kupata nakala za hotuba zinazosomwa, inaweza kuwa njia nzuri ya kupelekana mahakama/baraza za kiraia - citizen jury.
Hadi tukifikia hapo, wananchi kuacha kuwasikiliza viongozi na kuanza kuwaambia viongozi wanataka kusikia nini, itasaidia zaidi. Kwa sasa hali ilivyo ni kwamba kiongozi knows it all, kwa hiyo wananchi wanamsikiliza. Ndo maana RC, DC au waziri anaposomewa hotuba ya utekelezaji mbele za wananchi, huwa hawana uthubutu wa kuhoji. Wale waliojaribu waliambiwa kuwa wapinzani kana kwamba kuwa upinzani ni sacrilege (kufuru na kosa lisilosamehewa).
Basi jamii ihamasishwe kuuliza maswali na kuhoji uhalisia wa hotuba wanazosomewa kina Pinda na wengine.
Tchao
Kaka Andrew nimeona vyema, nimesoma pia coment za wengine. Suala hilo linakera sana ila labda kwa kuboresha ningeenda mbali hawa viongozi wanatakiwa wafike pale na kuwauliza watu mambo mbalimbali yaliyo katika eneo husika kama ni wilaya basi waziri aanze kuwa uliza watu kuna mazuri gani na mabaya yepi then wale wahusika watoe majibu kwa watu mbele ye waziri husika. tunakuwa na mahakama ya umma na kujua ukweli wa mambo nafikiri kutakuwa makini na usingizi wa museveni na wabunge wengu hautapatikana. hapo lazima protokari tuzitupe na uhalisia wambambo upewekipaumbele. Thomas Sankara rais wa Bukina faso aliweza hayo.
najua wageni rasmi wanataka kufanyiwa hivyo kwakuwa VIONGOZI WETU HAWASOMI KAZI YAO NI KUUZA SURA KAKA
Na mimi katkati ya maelezo yako nilisinzia
hii article yako nakubaliana nayo haya mambo niliyaona kwa mwajiri wangu kulikuwa na ku recycle speeches sana na its true audience huwa faifuatilii kinachosemwa! ni kama ceremony tu au formality sidhani kama speech nyingi za wanasiasa wetu zina chochote cha maana. nadhani wangetumia muda mwingi kwa Q/A kama ulivyo suggest. kitu ambacho nakimiss vile vile ni speech za watu kama nyerere ambaye alipenda kusema anachokifikiria yeye na sio anachokisoma. kwa hiyo kwa wakati wa nyerere ilikuwa rahisi kupata mawazo yake directly. quotes nyingi za nyerere ambazo mpaka leo tunazitumia kukumbuka legacy yake hakuwa ameandikiwa alikuwa anasema tu spontaneously kutokana na experience. bahati mbaya siku hizi hatuna orators tanzania na maybe africa?
Bw. Andrea,
Makala nzuri sana. Mimi nafanya kazi kwenye NGO ukweli ni kwamba viongozi wa serikali ndio husisitiza kuwa tuwaandalie hotuba na baadae ukiwakabidhi rasimu ya hotuba hizo watakuwa wameirekebisha kidogo sana, sasa ukimpa chizi rungu unategemea nini, si lazima utoke manundu? Sisi huwa tunahakikisha tunamlazimisha huyo kiongozi wa serikali kutamka maneno yale ambayo yataibana serikali itimize ahadi au malengo fulani-fulani ya maendeleo kwa wananchi ili kesho tuweze kusema ‘mkuu, lakini si uliahidi kule Songea kuwa serikali itatekeleza hili na lile?’. Hili ndilo jukumu letu sisi tunaofanya kazi ya kuzengea na kuzongea sera na michakato mingine ya maendeleo hapa nchini. Labda hili linastahili makala ya-kipekee, tuachane nayo turudi kwenye mada husika.
Ze Comedy ya kisiasa haishii hapo uliposema ndugu yangu Mushi bali hata sehemu nyinngine nyeti. Na mara nyingine mambo hufanyika ili kuweka ‘kiwingu’ - kwa kiingereza wanasema ’smokescreen’ - ili kuhamisha mawazo yetu kutoka kwenye mambo ya maana yanayotokea nyuma (in the background) yetu. Mfano tunasikia waarabu wa Saudia wanataka hekta 500 za ardhi yetu kiasi ambacho ni kama asilimia sitini ya ardhi yote ya ‘hii nji yetu ya asali na maziwa’ iitwayo Tanzania! Yako mengi na hata yale mashtaka ya ‘ufisadi’ ni komedi kali kabisa iliyoandaliwa na kupikwa vilivyo ili kutufanyia kiini macho - leo mashtaka yamerekebishwa - kesho ushahidi utapotea, n.k. Mwishowe tutaambiwa bwana eeh si mmeona wenyewe tumewapeleka watuhumiwa mahakamani ila tumeshindwa kuwatia hatiani?
Naomba niishie hapa kwa leo Bw. Andrea, aikambe hongera kwa kuwa mwandishi mzuri wa blogu, kumbe unautumia vizuri muda wako huko ughaibuni!
Samahani kwenye maoni yangu hapoo juu idadi ya hizo hekta sio asilimia sitini ya ardhi inayofaa kulimwa hapa nchini…..lakini ukweli unabaki kuwa michakato ya kuwakabidhi, kuwamilikisha au kuwakodisha wageni ardhi yetu lazima iwekwe wazi (to public scrutiny).
Weka maoni yako hapa!
Maoni mapya
Zinatembelewa zaidi
Makala mpya
Habari zaidi
Burudani
Makala mpya
Zenye maoni mengi
Zinazotembelewa zaidi
Counter:347,262
Maintained by Daima Solutions | Log in | Entries (RSS) | Comments (RSS) |