Home » Featured, Habari

Maisha ya ujana ya Jenerali Ulimwengu, Shivji, Museveni, Sitta na wengineo UDSM

16 May 2009 10,614 views 10 Comments

Na Born Again Pagan

Makala haya kwanza yaliandikwa kwenye “Kijiji” chetu (mjengwablogspot.com) mwezi Mei, 2007, chini ya kichwa cha habari, “BAP Anavyomwelezea Yoweri Museveni”. Madhumuni yake yalikidhi ombi la “Mwenyekiti wa Kijiji” kunitaka nitoe maelezo kidogo juu ya wanafunzi wenzangu Darasa la 1970 hapo Mlimani: Yoweri Kaguta Museveni na Hirji.
Nilianza kwa kutoa hoja kwamba haiwezekani kabisa kuweza kusimulia ya Yoweri Kaguta Museveni na Hirji bila kutoa, pengine, “background” ya miaka kumi ya kuanzia 1960 na jinsi matukio hayo yalivyojenga mikitadha iliyozalisha wanafunzi wenye msimamo mkali, kama akina Yoweri Kaguta Museveni na Hirji.
Katika makala haya yaliyohaririwa na kuongezea maelezo zaidi (pamoja na kubadili kichwa chake), ninagusia baadhi ya matukio ya miaka hiyo, na jinsi yaliyochangia katika kuivisha maisha ya ujana wa akina Yoweri Kaguta Museveni (Uganda), Hirji, Issa Shivji (Tanzania) pamoja na wengineo wengi waliomaliza hapo Mlimani mwaka 1970, kwa mfano:
Souma (Guinea), Archibord Kapote Mwakasungura (Malawi), John Garang (marehemu) wa Sudani, Salim Msoma, Issa Shivji, Nimrod Mkono, Moses Maira (marehemu), Ali Mchumo, James Kateka, Augustine Mahiga, Adamu Marwa, Pius Ngw’andu, Crispin Hauli, (marehemu), Abdallah Ngororo (marehemu), Patrick Qorro, Jenerali Ulimwengu, na wengine wengi sana, kama mimi.
Vile vile, makala haya yanachangia juu ya hali hapo Mlimani miaka yetu ya 1966-1970; mkwaruzano baina ya vyama vya wanafunzi vya USARF/TYL na USU kuhusu suala la “Rag Day”; umoja wa USARF na TYL; makala yanamtoa Hirji kando kidogo na kuzingatia tu ya Yoweri Kaguta Museveni (kwa makusudi); na mwisho, mgomo wa Jumamosi, 22 Oktoba, 1966.
Sisemi kuwa hao waliomaliza mwaka 1970 hapo Mlimani ndio tu maisha yao ya ujana yaliiva na kuwa na msimamo mkali. La hasha! Wengine walikuwa hawana msimamo huo! Na walikuwepo wengine nyuma yetu wenye msimamo mkali, pia, ikiwa ni pamoja na hao waliotutangulia. Ila nawataja hao wa mwaka 1970 kwa sababu ndio lilikuwa darasa letu.
Matukio ya Miaka Kumi Kuanzia 1960
Tumetoka mbali; tunakwenda mbali, pia. Kati yetu (wewe na mimi) huko tuendako hakuna aliyewahi kupafikia, ingawa tunapanga kuwasili huko. Miaka kumi ya kuanzia 1960 ilikuwa ya matukio mengi na mikakati mingi, ki-ulimwengu na ki-taifa (Tanzania). Ufuatao ni mtiririko wa matukio na mikakati hiyo; lakini si ki-miaka (chronology).
Moja, misukosuko ya ki-mataifa ya miaka ya kuanzia 1960 ilikuwa ni kupanuka kwa itikadi eti ya u-Komunisti. Kudhibiti kupanuka kwa u-Komunisti duniani kuliongozwa na Amerika ikisaidiana na Nchi za Magharibi, mithili ya hadithi ya kuweka kifuniko jini lisitoke kabisa ndani ya chupa!
Nchi hizi ziliuona u-Komunisti kuwa ni utamaduni uliowania kuua ule wa ki-Bepari. Michakato hiyo ikazua, eti, Vita Baridi! Amerika ilikania kudhibiti (to contain) kupanuka kwa u-Komunisti huko Asia ya Mashariki ya Mbali, Amerika ikawania kuishambulia Vietnam.
Mbili, kutamalaki kwa udugu baina ya Afrika na U-Rusi na kufungua Chuo Kikuuu cha Lumumba Friendship kilichochukua wanafunzi wengi wa-Afrika. Sambamba na hilo, kupanuka kwa Vita Baridi kuliingilia mstakabali wa Bara la Afrika. Ugomvi wa Ulaya ukaletwa kwetu Afrika.
Tatu, kuuawa kwa Waziri Mkuu wa kwanza wa Kongo Emergy Patrice Lumumba kutokana na njama za serikali ya Amerika kupitia Shirika la Ujasusi la CIA na serikali ya Ubelgiji zikishirikiana na vibaraka wa ndani chini ya Joseph Désire Mobutu na Moisé Kapenda Tshombe wa Jimbo la Katanga lililotaka kujitenga! Amerika na Ubelgiji hawakupenda kuiona Kongo inakuwa ya ki-Komunisti, na, pengine, kuambukiza sehemu nyinginezo za Afrika, hasa Afrika Kusini.
Nne, mchakato wa Afrika kutaka kujitawala ulijikita katika ndoto ya Umajumuhi (Pan-Africanism) ya wasomi waliobobea wakishirikiana na wenzao wa Amerika na Karibe au niseme wenzao wa Diaspora. Hawa waliweza kuunda mtandao wao vizuri kuliko kuunda mtandao na walalahoi wa chini (grassroots). Pengine hapa ndipo kuna kitovu cha kuyumba kwa uongozi katika nchi zetu za ki-Afrika!
Umajumuhi (Pan-Africanism) ukabaki ni ndoto tu hadi leo kutokana na wa-Koloni kuweka vikwazo kuwa kwa waasisi wetu kuwa na u-haki wa kudai uhuru, iliwabidi kuthibitisha kuwa walikuwa ni wasemaji wa walalahoi. Hii iliuleta mchakato wa kupigania uhuru kwa uwanja wa nyumbani, k-taifa na sio ki-Bara la Afrika.
Nchi nyingi zilianza “kuruka juu na kujulikana”, kama majimbi kutoka majivu-moto (popcorns)! Na sisi tukawamo katika mchakato huo.
Tano, ingawa Umajumuhi (Pan-Africanism) ulishindwa kulikomboa Bara la Afrika kwa mkupuo (wholesale), waasisi wetu hawakukata tama ya Umajimuhi. Wengine walionelea kuwa Afrika ingeweza kukidhi lengo hilo kwa kuungana rejareja (piecemeal): wakaunda, kwa mfano, Umajumuhi-kipande, Pan-African Movement for East and Central Africa (PAFMECA).
Kiongozi wetu aliahidi kuchelewesha uhuru wa nchi yetu kwa kuzingoja nchi nyingine tatu za ujirani mwema (Kenya, Uganda na Zanzibar). Lakini wapi! Ilibidi nchi za Afrika zijitawale, reja reja. Leo zinalilia kuunda Afrika moja!
Sita, kwa Tanzania Bara, chini ya siku kama 1000 hivi, Waziri Mkuu Julius Nyerere alitangaza kujiuzulu. Sababu: Kuimarisha TANU. Ilimbidi aende kwa wananchi tena kupata kibali cha kuongoza mstakabali wa taifa la Tanganyika changa.
Lakini kuna pia ukweli kwamba Waziri Mkuu Nyerere alifanya hivyo ili kuepusha kura ya maoni ya wa-Bunge machachari, ambayo karibu ilikuwa impe “a vote of no confidence” kutokana na kupingwa kwa baadhi ya sera (za Chama Tawala na Serikali yake) kuhusu suala la uraia katika mikitadha ya Umajimuhi (Pan-Africanism), kwa ujumla, na Tanganyika, hasa. Nyerere alionekana ‘a statesman” kwa kunusuru maafa yaliyokining’inia usoni mwa nchi yetu changa!
Mtafaruki wa namna hiyo ulikikumba chama cha TANU kwenye mkutano wake wa Tabora kutoka Januari 25-28, 1958 na kuzalisha chama cha upinzani cha African National Congress, chini ya Zuberi A. Mtemvu.
Wa-Bunge machachari wa wakati huo, kwa mfano, Mheshimiwa M-Bunge Richard Wambura (East Lake Province – leo Mkoa wa Mara) alidiriki hata kutamka kauli kama hii: Endapo umeshindwa kuongoza, tuachie sisi tuongoze/waachie wengine waongoze. (Rejea Hansard ya mwezi huo ambao Nyerere alipojiuzulu).
Wa-Bunge machachari walihoji, kwa jina la Umajimuhi: Kwa nini ilikuwa ni rahisi kwa wa-Ulaya (hasa wa-Uingereza) na wa-Asia waliokuwa na uraia wa Uingereza) kuweza kuwa raia wa Tanganyika kuliko wa-Nigeria au wa-Ghana, kwa kifupi wa-Afrika wa kutoka nchi nyingine za Afrika?
Zaidi, wa-Bunge walilileta nyumbani suala la uraia na kuuliza kwa nini spidi ya Afrikanaizesheni (kutoa hatamu za uongozi wa ngazi mbalimbali kwa wazalendo wa-Matumbi) zilikuwa za mwendo wa “mzee kobe”?
Saba, suala la Afrikanizesheni lilijikita ki-jeshi: Jeshi la Polisi na Jeshi la Ulinzi (Tanganyika Rifles). Hatimaye, likachukua mkakati mwingine na kusababisha uasi wa Jeshi la Ulinzi uliozimwa kwa msaada wa aliyekuwa m-Koloni wetu (Jeshi la Uingereza), baada ya Rais na Makamu wake kujificha kwa siku kama tatu hivi.
Nane, baada ya kuzimwa uasi huo na Rais kutoka majifichoni, yalifuatia mambo kadhaa, ki-Katiba. Kwa mfano, Katiba ilibadilishwa; kufutwa kwa Vyama vya Wafanyakazi na kuundwa kwa NUTA; migomo kupigwa marufuku; sheria ya Kuweka Watu Kizuizini Preventive Detention Act); na matayarisho ya chini chini ya Tanzania kuwa ni ya chama kimoja. Mabadiliko hayo yalimpa Rais madaraka mengi kiasi cha Rais Nyerere kutamka kwamba angeweza kuwa dikteta, kama angependa!
Tisa, mtazamo mpya wa Amerika kuhusu hali ya ki-siasa Zanzibar, ambako kulikuwa na kituo chake cha mambo ya anga za juu (satellite surveillance station). Yasemekana baadhi ya wa-Zanzibari walikuwa na msimamo wa mkono wa kushoto uliotishia, eti, maslahi ya Amerika.
Hii ilitokana hao kuhusiana ki-ukaribu sana na Kwame Nkrumah (Ghana), Abdel Gamal Nasser (Misri), u-Rusi, u-China na Kuba.
Kumi, Muungano wa Tanzania. Kuna wenye kuamini kuwa Nchi za Magharibi ziliogopa kuiona Zanzibar ikiselea kuelekea eti, u-Komunisti, hasa kufuatia mapinduzi yaliyong’oa utawala wa ki-Sultani. Hawakutaka kuona Zanzibar inakuwa “Kuba” ya Afrika.
Tanzania Bara (Tanganyika) ilikuwa chini ya Julius Nyerere. Na Nchi za Magharibi zilimfikiria kuwa ni mpinga u-Komunisti (our man in Dear es Salaam). Hata yeye Julius Nyerere (m-Katoliki) aliwahi kutamka kuwa si m-Komunisti kwa sababu ma-Komunisti hawamwamini Mungu!
Nyerere alikuwa m-Majimuhi (Pan-Africanist). Kwahiyo, eti, Nchi za Magharibi zilimtumia Mwalimu Nyerere (m-Majimuhi) kuinasua Zanzibar na kuunda Muungano, kulingana na lengo la mikitadha ya Umajimuhi.
Na kwamba hata Sultani wa Zanzibar alipopinduliwa, aliishi katika meli yake kwa muda wa karibu siku tatu nje ya Dar es Salaam kabla ya kukimbilia Uingereza.
Kumi na moja, kutamalaki kwa udugu baina ya Afrika na Nchi za Asia (Afro-Asian Solidality) na pia kukua kwa uhusiano baina ya nchi huru za ki-Afrika na nchi za Mashariki ya Kati (Pan-Arabism, chini ya Abdel Gamal Nasser).
Kumi na mbili, Kumi na mbili, kuzaliwa wa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU), chini ya katibu Mkuu Diallo Teli wa Guinea.
Kumi na tatu, kutamalaki kwa umoja wa Nchi Zisizofungamana na Upande Wowote wa Vita Baridi. Lakini nchi zetu zikajikuta zinavutana kati ya itikadi ya Nchi za Magharib, kwa upande mmoja, na u-Rusi/u-China, kwa upande mwingine.
Afrika ikajigawa katika makundi mawili:
Casablanca Group – nchi zenye msimamo mkali wa kukataa misaada na kutegemea wengine: Algeria, Misri, Ghana, Guinea, Libya, Mali na Moroko.
Brazzaville Group (zenye kupenda ujamaa wa ki-Afrika pamoja na zisizo na msimamo mkali): Ethiopia, Liberia, Nigeria, Sierra Leone, Somalia, Togo, Tunisia na Congo (Kinshasa, kwa upande wa pili. Kundi hili lisilo na msiamamo mkali lilibadilika kutoka Brazzavuile Group na kuwa Monrovia Group.
Kugawanyika kwa vyama vya wafanyakazi kati vile vyenye msimamo mkali: All-African Trade Union Federation (AATUF) kilichobadilika na kuwa Organisation of African Trade Union Unity (OATUU), kwa upande mmoja, na All Africa Free Trade Unions (AAFTU), kwa upande mwingine.
Itaendelea wiki ijayo:

Barua pepe: romuinja@yahoo.com

10 Comments »

 • julius said:

  Hamjamboni

 • Edwin Ndaki said:

  Kwanza Jamii habari za hapa.

  Nimekuja kusoma muendelezo wa makala ya Makala hii lakini sijaona juma hili au nini kimetokea.Naomb msaada

 • amani said:

  Hongreni Kwanzajamii kwa kutujuza na pia kutupatia fursa ya kutoa maoni yetu.

 • Ntuli M.Mwakyusa said:

  Kujua ulikotoka na historia ya nchi pamoja na bara lako ni vitu muhimu sana.
  Hata mungu alisem mwanangu Esrael kumbuka niliko kutoa misri na ukatende mema,ktk nchi ya nyama na asali.
  Nimepitia makala ,hiyvo nawasa vijana wasikate tama bado tunayo nafasi ya kurekebisha palipokosewa baada ya kujua wapi tumetoka ,tupo wapi na tunaelekea wapi.
  Endelea kutuhabalisha kijaa;

 • Manace said:

  Muendelezo wa makala ya Maisha ya Jenarali Ulimwengu, Shirvji, Museveni, Sitta inapatikanaje? Tusaidie ndugu. It is very interesting actually. Nafikiri viongozi wa sasa wa Tz wana tatizo moja kubwa “hawajui historia ya nchi yao na afrika kwa ujumla” na hivyo wanashindwa watende kipi na kwa nini! Watathmini mmoja mmoja utagundua hilo, ni wachache sana wanaoielewa na ndio hao hao wenye maono.

 • nisile mwasulama said:

  I LIKE IT,…………….ni utaratibu unaopendeza/unaofaa kujua walikotoka watu maarufu,,…thank a lot for the article

 • muttayoba mtibora said:

  ulimwengu ameendelea kuwa kiigizo changu,naendelea kufanya jitihada za kukutana naye kabla ya kutenganishwa na ukutamkuu wa mwenye dunia…

 • mtweve,Joe said:

  Ok,inapendeza sana.ningefurahi sana kama ningepapata jua maisha binafsi ya kina Sita na mwenzie Ulimwengu.nadhani kwangu ni changamoto.

 • Hakeem said:

  kwa kweli nimefurahishwa sana na hii article..somo kama hili la historia ya afrika na tanzania kwa ujumla wala hatukufundishwa sie shuleni…..walimu wetu walikuwa busy na mito na maziwa pamoja na historia isio tuletea faida yeyote ile…its very interesting to know where we r comming from and where we r going actual… nadhani hata hao viongozi wetu wa sasa wengi wao waliozaliwa miaka ya 50 na 60 hawajui maswala kama haya…watu kama nyie ndio mnahitajika kuwafundisha walimu wa masomo kama ya historia ili waweze kuwapanua mawazo wanafunzi wa sasa..vijana wengi nadhani nikiwemo mimi.. hatulijui swala hili….i think somewhere something went wrong na ndio maana mpake leo hii afrika hatuwezi kuungana..for my opinion. nafikiri kutokana na kuwepo kwa vibaraka barani afrika hatutoweza kuungana…yani wanasaminiwa sana wazungu(western) kuliko waafrika wakati hao wazungu tunaowasamini hawatusamini…wenzetu wa european wanaungana sie waafrika bado tuko palepale…na pili nafikiri kutokana na nidhamu ya uoga kuwaogopa wazungu waafrika hawatoweza kuungana na kuwa kitu kimoja…Ili kujikwamua katika swala kama hili waafrika na afrika inawatakiwa tuwe na msimamo mmoja na sera zisitofautiana…pia tuache kabisa kuwategemea wazungu…ilikuwa imara zaidi na kupata heshima afrika or tanzania we need to follow the steps of our fellow brother India..economical and politically…sisemi kuwa wamejikwamua kutoka katika umaskini la. ila wamevumbua mbinu za kuweza kujikwamua kutoka katika hali ya kutegema MZUNGU…cha ajabu sasa wahindi ndio wanaotegemewa na western katika swala zima la(I.C.T Technology)waafrica if we do the same as India.. nadhani tutafika atleast where we aim to reach.. mungu ibariki afrika na watu wake.. wafunue akili na wape mawazo mazuri..washushie neema zako na wape hekima.. waondoe na umaskini kwani afrika si maskini ila watu wake ndio maskini.. tuondolee viongozi vibaraka na tuletee viongozi shupavu na wenye moyo wa kuwasaidia wenzao na sio wenye tamaa na kuwajali ndugu zao na familia zao ila wenye kujali umma wa watanzania…. Mungu nijaalie na mimi niwe kiongozi au mtu mwenye kuijali afrika na watu wake ili niweze kuwasidia watu wangu na afrika kwa ujumla.. love u afrika… love u tanzania..godbless us all.. amen!!!

 • Myonge said:

  HAKEEM. Asante sana kwa kunisemea. Ni siku hiyo tutakapojuwa nia ya wazungu na kukataa mambo yao, basi tutaanza kupiga hatua ya maendeleo.

  Asante Hakeem, unabusara na unaona mbali.