Home » Featured, Headline, makala

Wasomi wetu wanapogeuka wafagiaji mabanda ya kuku

12 May 2009 3,326 views 18 Comments

Na Andrew Mushi

NIMECHOCHEWA kuandika makala haya kufuatia mjadala ulijitokeza kati yangu na rafiki yangu Nkwabi anayeishi, kusoma na kufundisha Uingereza.
Huyu bwana ni mwalimu wa Hisababati na Fizikia, na ndio anavifundisha Uingereza. Mjadala ulianza pale tulipokuwa tunakatiza katika mitaa ya chuo kikuu cha Birmingham hapa Uingereza tukaona jengo moja limeandikwa (Physics and Astronomy). Kwa Kiswahili cha haraka haraka maana ya haya meneno ni Fizikia na Elimu ya Anga za juu.
Kuona maneno ya Physics and Astronomy ilizusha mjadala mkali sana lakini unaorutubisha akili kati yangu na huyu rafiki yangu. Bwana Nkwabi alianza kwa kusema wenzetu Waingereza wanachokisoma wanakifanyia kazi kwa vitendo ndio maana wanaweza kupeleka vyombo mwezini na katika anga nyingine za mbali, achilia mbali mambo mengine luluki makubwa wanayoyafanya. Elimu ya Waingereza inaendana na uhalisia wa mambo. Hawaandai mitaala ya masomo ili tu kujiridhisha.
Nikupe mfano mwepesi, wiki jana nilienda shuleni kwa binti yangu anayesoma shule ya awali, kumchukua baada ya muda wa masomo kwisha. Kwa kawaida kwa sheria za Uingereza watoto wa shule za awali, na msingi lazima wapelekwe shule na kufuatwa kurudishwa nyumbani na wazazi au walezi wao. Hii ni ili kuakikisha usalama wa watoto.
Nilipofika shuleni nikakuta mapokezi wameweka machine mbili ndogo za kuangulia vifanga vya kuku na wakawa wanaanguliwa. Ukubwa wa kila machine ni futi moja kwa futi moja.
Kwa hiyo watoto wakawa wanoana vifanga wa kuku wanavyoanguliwa. Bila kuambiwa chochote watoto wanajifunza vitu vingi sana. Mie mwenyewe binti yangu japo ana miaka miwili na nusu, alianza kuniuliza maswali mengi sana kuhusu mayai, kuku, ndege na kadhalika.
Bwana Nkwabi akaigeukia Tanzania, na kusema wasomi wetu, hasa akimaanisha maprofesa na madakitari wa falisafa wanachojifunia ni ‘papers’ ngapi wameandika na kuwasilisha katika makongamano. Nami nikachapia kwa kusema pia wanaona sifa na fahari kwa wingi wa kuku na ngombe wanaofuga na bar wanazomiliki. Naye akachombeza, sasa kwa mtindo huu ni saa ngapi tutaona elimu yao ikitembea barabarani.
Kutoka hapa tukajadili je ni kwanini wasomi wetu wanashindwa kutafsiri elimu walio nayo katika bongo zao ikaonekana na jamii na kutunufaisha kama Taifa. Tukakimbilia jibu rahisi na labda la kichovu kwa vile hatukupenda kufikiri kwa kusema wasomi wetu hatuwapi rasilimali pesa na pia nafasi. Ila hatukujadili je kwanini wasingepewa hizi pesa za EPA badala ya kuwachia akina Green na Kagoda Industrial wazisunde wavavyotaka.
Sikuvunjika moyo maana nilikumbuka nchi ya Ghana, ambayo ni waafrika wenzetu.
Wao mitaala yao imeelekezwa kumuanda Mghana kufanya kazi pahala popote duniani. Ndio maana katika katika kazi kubwa na mashirika ya kimataifa hutakosa Mghana.
Kwa jinsi hii siwezi kushangaa Kofi Anan wa Ghana alifanikiwaje kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, maana ni matunda ya mikakati ya makusudi kielimu.
Katika mada hii nitajaribu kujadili na kuchokoa kuwa licha ya kisingizio cha kutokupewa pesa na nafasi bado wasomi wetu wanaweza kutoka katika vyumba walivyojifungia na kutumia mianya mingi iliyopo na kuweza kutafasiri elimu yao katika vitendo.
Ila ni lazima tuanze na msingi nzuri na imara
Nitajaribu kujikita katika elimu ya msingi na kiasi fulani elimu ya awali kujadili tufanye nini. Maana naamini tukishakuwa na msingi na mitaala mizuri huko chini, sekondari, vyuo vya kati na hata nyuo vikuu haitakuwa kazi ngumu, maana itakuwa ni jadi yetu.
Pa kuanzia ni kuifanyia ukarabati mkubwa mitaaala yetu ili iendane na hali hali halisi ya kiuchumi na dunia na zaidi izingatie mazingira yetu. Nitatoa mifano michache ili ichokoze kufikiri kwetu.
Nianze na mfano wa somo la historia, badala kungangania kujua historia ya kila pahala duniani. Somo la historia lifundishwe na kuakikisha mwanafunzi anaijua historia ya nchi yetu barabara.
Tunawacheka Waingereza au Wamarekani watoto wao wanapokua hawajui historia au mambo ya nchi nyingine, ila ya kwao wanayafahamu kama sala ya Bwana. Wanaona haiwasaidii chochote watoto wao kuimba kama kama kasuku mambo ya kila pembe ya dunia, wakati yalio uhani kwao wanayajua nusunusu.
Mfano mwingne ni somo la Jografia. Kwa jinsi linavyofundiswa sasa hivi halimuandai na kumfanya mtoto aelewe mazingira ya Jografia ya Tanzania na jinsi ya kupambana nayo.
Mtoto atakariri wee Tanzania kuna mito, maziwa, milima, madini kiasi gani, bas! Tungeenda hatua moja zaidi na kumfanya aone je, hivi vitu vinagusaje maisha yake moja kwa moja.
Mathalan, badala ya kujifunza juu ya Tanzania kuna bahari, mito na maziwa mangapi, mtaala unaweza kwenda mbali zaidi kwa kutoa mwanya watoto wakajadili kwa kina ni jinsi gani hayo maziwa na bahari vinaweza vikatumika kusaidia kuinua maisha ya maeneo ya watu husikika.
Wakati huo watoto wa maeneo mengine nao wanajadili kwa kina Jografia ya eneo lao na jinsi ya kuitumia vizuri kwa manufaa yao.Hata kama ni mtoto wa darasa la awali bado kitu kama hiki kitamsaidia sana badala ya kukimbilia kukaririsha watoto wetu vitu vingi visivyo na kichwa wala mkia.
Masomo mengine kama hisabati, kiswahili, maarifa na hata uraia navyo tusivifanyie ajizi.
Mfano, somo la uraia, tuligeuze kimwandae mtoto kuwa raia makini na mzalendo anayeipenda nchi yake.
Badala ya kukariri habari ya bunge, vikao vya vyama siasa na mifumo ya uongozi na kuishia hapo hapo tuvuke mpaka twende kwenye uhalisia wa mambo.
Mfano, kwa shule zilizo karibu na halimashauri au makao makuu ya wilaya. Mtaala uruhusu watoto wapate nafasi ya kutembelea wakati wa vikao vya madiwani na kuona wanavyoendesha vikao vyao.
Na pia wapewe nafasi waongee na madiwani na waulize mswali, namna hii watajua jinsi siasa na uongozi unavyoendeshwa.
Na kwa upande wa walio mbabali na makao makuu ya wilaya, wakati wa vikao vya wa vijiji, kuwepo na fursa ya kuona jinsi hivi vikao vinavyoendeshwa.
Kwa lugha nyepesi, maadam kila shule hapa nchini iko ndani ya kijiji na au mjini, basi kuwepo na kipengele kinachosistiza watoto wajue kwa vitendo jinsi uongozi wa kijiji unavyofanya kazi.
Kwa mtoto kuelewa mfumo wa uongozi wa kijiji chake na jinsi unavyofanya kazi, unaampa nafasi ya kujiskia mwakajiji/mtaa. Na kwa jisi hii anaweza kutumia haya maarifa akayahusisha na ngazi ya wilaya, mkoa taifa na hata umoja wa mataifa.
Afya nalo ni eneo linaweza kushughulikiwa katika mitaala ya shule za msingi na likawa na mafanikio mengi sana katika maisha. Mfano, mtaala unaweza kutoa nafasi kwa watoto kufahamu huduma za afya zilizoko ndani ya maeneo yao.
Hospitali, vituo vya afya, zahanati zimetapaka kila mahali. Watoto watembelee hizi sehemu wajifunze zinavyonya kazi. Wajadili na waganga na wauguzi walio katika haya maeneoa ni jinsi gani watoto wanaweza wakawa na afya njema bila kwenda hospitali.
Watoto kupata nafasi ya kuongea na wauguzi na waganga na hata kuona wanavyotibu watu, kuona maabara zinavyofanya kazi, itakuwa na matokea mazuri sana kwa watoto wetu. Mathalan, watoto wakitembelea hospitali na muuguzi akawaelezea umuhimu wa kuchemsha maji ya kunywa, labda wakaonyeshwa kwa darubini vidudu walio katika maji yasiochemshwa na badaye yakachemshwa wakaonyeshwa yalivyo salama. Nina uhakika baada ya hapo hakuna mtoto atakunywa maji bila kuchemsha.
Ninaweza kutoa mifano mingi sana, lakini ujumbe ninaojaribu kuletwa kwako ni kuwa tutumie vitu vinavyopatikana katika maeneo yetu kujifunza na pia kuwapa nafasi watoto kuvielewa. Nataraji wizara ya Elimu watazingatia changamoto hii, na pia sisi wananchi tuwashinikize watunge mitaala ya kutukomboa badala ya hii ya sasa inayotudumaza kila kukicha!

amushi1@yahoo.com

18 Comments »

  • Shilatu said:

    Nimevutiwa sana na mjadala wenu, naichukua hii kama changamoto na kuifanyia kazi. Mungu aniwezeshe.

  • Elinsarie E maimu said:

    Nimevutiwa na makala yako bwana home boy,

  • Chacha Matoka said:

    Ulichoandika kuhusu elimu ya Tanzania ni sahihi.
    Wanafunzi wanaandaliwa kupata A katika certificate. Masomo mengi kuanzaia elimu ya msing mpaka vyuo vikuu hayaendani na hali halisi ya Mtanzania wa karne ya leo. Ndiyo maana mfano mzuri ni ajira kila leo vijana wetu wanalalamika kuwa waliosoma nje wanapewa kipa umbele au Wakenya na Waganda. Tatizo ni mfumo mzima mzima wa elimu ambapo wanafunzi hukariri Theories, principles na formulars amabzo hazina matumizi katika maisha.
    i.e wakati nasoma sekondari Nilikuwa Abbot Third edition ambayo nillisoma na kusolve all queastions. Hivyo swali lolote likitoka katika Abbot na has a Third Edition wamekwisha. Nelkon, n.k. Lengo ni A nikimaliza O level. Mtazamo huo huo ulikaa kichwani mwangu ku aim A nyingi mpaka nafika pale mlimani. Lengo lilibakia moja tu kupata first class na sio elimu hiyo itanisaidia vipi katika maisha ya mbeleni. Then mtazamo ukabadilika kidogo kazi nitakayofanya itategmea na masomo gani nimesoma na inalipa kiasi gani. na kazi nzuri inategemea na Grade gani gani First class au Upper second au Lowe second ama Gentleman degree.

    Nilipofika kazini msituko, maana hakuna cha theories na principles, na kazi yenyewe vilevile haikunipa mwanya wa kutumia matheory yangu niliyojilimbikizia bali what the boss want me to do!! Ngoma!! it took time ku adapt.
    what yo are saying like industria visit ni mfano mzuri, Lakini also kuna kitu kinaitwa work experience. Tanzania ni chuo kikuu tu wanakwenda work experience na tena ni wanaosomea ualimu na engineers labda na wanaosomea udaktari. Lakini wengine hakuna. kazi utakutana nayo siku ukiajiriwa!! Mimi nilipangiwa kazi wakati huo sikuomba kazi! ndiyo maana usishangae ukimuona Kipanga ana first class lakini barua ya kuomba kazi ( covering letter hajui na hajui hata kujibu maswali ya interview)!!
    Mfano easy ni idadi ya masomo wanayasoma watoto ni mengi mno!! sekondari ndiyo hasa usiseme na mtihani same sitting!!! what do you expect? craming without knowledge.

    Ingawa nilipofika ughaibuni shule ilikuwa rahisi mno!! maana nilifundishwa kile kinachofanyika ama kinatakiwa kufanyika na kucremishwa ma theories mlima!!

    yr article well researched. Congrats.

  • Malila Erasto said:

    Ndugu Andrew,

    Ahsante sana kwa kuleta changamoto nzuri ya kuihamasisha serikali yetu hasa ukilenga Wizara ya Elimu; maana hata sisi sote tukiwa ni miongoni mwa wengi tuliosoma masomo mengi kwa nadharia zaidi bila vitendo. Mfano si ajabu sana hata mtu wa mkoa wa Kilimanjaro kushindwa kujua kama aina ya mlima huo ni volkano. Au mtu wa pwani kushindwa kujua kupwa na kujaa kwa bahari au hata kutembelea visiwa vilivyopo mahali walipo.

    Mie natamani tufikie huko kwani kila ninaposafiri ndio ninakumbuka tulijifunza juu hiki na kile sasa hapo ni kwa jitihada binafsi. Mungu aiwezeshe serikali yetu kuchukua hatua za utekelezaji maana kama ni pesa zipo, sisi wafanyakazi/wakulima/wafanyabiashara tunalipa kodi kila siku/wiki/mwezi/mwaka lakini mapato hayo hayatumiwi kuwanufaisha wananchi wake.

  • E.S.Kimambo said:

    NDUGU NAONA MJADALA WENU ULIKUWA MZURI NA WAKUVUTIA SANA,NAONA NINGEKUWEPO HAPO NINGEFAIDI SANA MAMBO MENGI KATIKA MJADALA HUU.
    MUNGU AWABARIKI KWA KULIONA HILI,NADHANI NDANI YA BARAZA LA MAWAZIRI WA TANZANIA KUNGEKUWEPO NA VIONGOZI WENYE vision KAMA YA KWENU,NCHI YETU INGEKUWA MBALI SANA.
    HATA MIMI NILISHAKAA MAHALI NIKAJISEMEA MWENYEWE “kama uongozi wa nchi ndio kama hivi ulivyo,kwa maana ya baraza la mawaziri na jinsi wanavyowajibika kwa sirikali,mbona hata mimi uwaziri nauweza?”
    NINAJIULIZA JE HAWA MAWAZIRI HUWAHAJIFUNZI TOKA KWA MAWAZI WENZAO WANAPOTEMBELEA NCHI HIZO?AMA HUWA HAWAENDI NA WAKATI ULIOPO? AMA KAZI NI KUITISHA SEMINA NA MAKONGAMANO ILI KUPATA MIANYA YA POSHO ?
    MAANA KAMA WAZIRI WA,MFANO (ELIMU) NI LAZIMA UKAE NA KUFIKIRI UFANYE NINI KUBORESHA ELIMU KWA KUTUMIA USOMI WAKO (UPROFESA)HALI KADHALIKA WAZIRI WA NISHATI.HAIWEZEKANI MITAMBO YA UMEME ILYOFUNGWA TOKA UHURU NDIYO INAYOZALISHA UMEME MPAKA LEO,WAZIRI UMEKAA KWENYE OFISI TU,WALA HUONI NJIA ZINGINE ZA KUZALISHA UMEME UNATEGEMEA UMEME WA KIHANSI,MVUA ZIKIPUNGUA BASI UMEME HAKUNA.SANA SANA KUKODI MAGENERETA.
    WAKATI TUNAWEZA KUTUMIA SOLAR,WIND MILLS,MFANO UKANDA WA MWAMBAO KUANZIA TANGA MPAKA MTWARA,KUNA UPEPO WA KUTOSHA TU KUZUNGUSHA WINDMILL PROPELLERS,UNADHANI KOTE HUKO TUNGEFUNGA WINDMILLS TUNGEINGIZA UMEME KIASI GANI KWENYE GRIDI YA TAIFA?JAPOKUWA HATUWEZI KUZIFUNGA KOTE HUKO KWA WAKATI MMOJA,ANGALAU TENGEENDA KIDOGO KIDOGO,MWISHO TUNGEMALIZA.MAREKANI WANATUMIA UMEME WA WINDMILLS NA SOLAR POWER,LAKINI SISI TUNAKOROMA BADO NDANI YA USINGIZI.
    HII YOTE NI UFINYU WA AKILI NA KUTOKUSUMBUA UBONGO UFANYE KAZI.
    UMEME UKIKATIKA OFISI YAKE INA GENERETA LA DHARURA,JE,VIPI KULE MANZESE,KIGOGO,MBAGALA NA TANDIKA WANA MAGENERETA YA DHARURA?
    KAZI NI KUFUGA NG’OMBE KATIKATI YA JIJI NA KUONGEZA MKE WA PILI NA WA TATU.
    SISHANGAI KUONA MSOMI ANAKWENDA MAREKANI BADALA YA KUFANYA KAZI KAMA ZA AKINA ANAN ,BOUTROS BOUTROS GHALI,WAO WANAOMBA KAZI ZA KUFAGIA MABANDA YA KUKU.
    THNX,Kim.

  • godluck said:

    Mdau,
    Hoja yako ni inavutia,ila inaacha hewani baadhi ya mambo ya msingi.
    Nitajaribu kugusia kwa kifupi.

    Moja.
    Kabla ya kuingiliwa na wageni,jamii ya kiafrika,mathalani Tanzania(hususani,tangayika),ilikuwa na mfumo wake wa elimu uliokidhi matakwa ya jamii hizo.Wazee/kungwi/jamii iliweza kuipa elimu mahsusi jamii mpya inayochipukia kwa ustadi na uadilifu ulijaa weledi.Matunda ya elimu yao yalipimwa kwa vigezo yakinifu ktk enzi zao,na kufuzu vyema.

    Mbili.
    Baada ya kuingia kwa wageni katika Afrika,tamaduni mpya ziliingizwa pia..ni nyingi,mojawapo ni namna mpya ya kutoa/kusambaza/na kudumisha mfumo wa elimu.Wao walikuja na mapya (naam,yaliwafaa wao) na kuyatumbukiza kwa nguvu katika jamii za kiafrika..mojawapo ya njia ya kurutibisha hili,ni kudhoofisha mfumo walioukuta.Na hapo walifanikiwa haswa!

    Tatu.
    Tatizo linakabili jamii nyingi zilizoathiriwa na tatizo hili,ni namna ya kuoanisha mifumo miwili (mmmoja,wa kizani uitwao si rasmi,na mwingine wa kisasa ulio rasmi)katika kukidhi hitaji la kizao hiki na kijacho.Ktk hili,juhudi za kila mmoja zatakiwa,na hata ikiwezekana,mjadala utakaozaa makubaliana ya pamoja.

    Mwisho,
    Tunashuhudia nchi ambazo tunadhani zimefanikiwa kielimu (india,nigeria, etc)..naam,hazikifanikiwa kirahisi..tuyaonayo ni matokeo halisi ya juhudi dhati na umakini wa watu hao ktk masuala ya msingi.

    Hatujachelewa bado..Rome haikujengwa kwa siku moja..tuache vihoja vya viongozi kama Mungai(alitoa mchanyato mkali wa masomo ya secondary),na kutoa suluhu la kudumu la hitaji hili..

    Nasema tena,..hoja hii inavutia,ila tusisahau misingi ya dhati ktk kuleta suluhisho la kudumu.

    Aksante,

    Naomba kuwakilisha.
    wenu mtiifu,
    Godluck

  • Eunice Massanja said:

    Kweli mada hii ni nzuli sana lakini ni kweli kuna wasomi wengi sana na sasa hawana kazi, pamoja na kwamba wamesoma. Naomba jamani itafutwe njia ya kuweza kusaidia hao watu ili waweze kukizi mahitaji yao ya kila siku.

    Naomba Mungu pamoja na mimi pia anisaidie ili niweze kupata kazi nzuli Serikalini ambayo naamini itanisukuma katika kuinua maisha yangu pamoja na famili yangu.

  • HELLEN USIRI said:

    Kaka Andrew,
    Asante sana kwa changamoto uliyoitoa na iliyo muhimu katika karne ya sasa.Elimu ta Tanzania inahitaji marekebisho lukuki ukiongezea machache na ya msingi uliyotoa.
    Ukiangalia Mawaziri wanapopewa kusimamia wizara ya elimu kila mmoja anapoingia ofisini anafikiria jinsi ya kubadilisha mtaala,swali langu linakuwa je mitaala inayobadilishwa kila mara je waalimu wa mitaala hiyo wameandaliwa? Je zana za kufundishia zipo? Je maabara zipo? shule nyingi mpya za sekondari wanafunzi walishaona hata chumba chenyewe? wanafunzi hawa unategemea wataweza kuingia katika ushindani wa elimu uliopo duniani Je watanzania wanatarajia kupata ajira wapi kwani hata kujiajiri wenyewe haiwezekani kufuatana na mfumo wa elimu ulivyo mbovu.
    Sisi kama kikundi kidogo kijijini tuliona umuhimu wa afya ya mtoto awapo shule ya awali na shule ya msingi, Tukaona maziwa yana uwezo mkubwa sana wa kumjenga mtoto ukizingatia mtoto wa mkulima ambaye kipato chake ni duni ni shida hata kupata kifungua kinywa asubuhi na hukaa darasani hadi saa 8 mchana au 9 matokeo yake husinzia na mwl huwa mkali bila kuelewa tatizo la mtoto ni njaa na kumchapa, adhabu juu ya adhabu jamani sasa apate angalau nusu lita kwa wiki,jambo la kusikitisha wazo hili ni maeneo machache yameona umuhimu wake ambapo serikali ina uwezo mkubwa sana wa kuliwekea mikakati na lifanyiwe kazi kwa kunusuru hawa watoto wetu hizo hela za EPA walizojirundikia kwenye akaunti zao na nje hawana huruma hata lepe kwa kizazi kinachokuja Mungu okoa Tanzania kupitia viongozi wanaopewa madaraka.Ni mambo mengi yanayotakiwa yafanywe na sisi wenyewe kukomboa elimu yetu na mengi mengine.
    Asante Hellen

  • Kitoto said:

    Andrew hii ni zaidi ya hoja ni changamoto kwa wasomi wetu, nilipoisoma hoja hii nikakumbuka kitu kimoja, siku moja pale Chuo Kikuu cha Sokoine kulikuwa na kitu kinaitwa Edward Sokoine Memorial day,na walimualika Mh Mizengo Pinda kama msemaji mkuu, katika mengi aliyoyasema Pinda ninakumbuka kitu kimoja tu, Mh Pinda alishangaa sana ni vipi Maprofesa wa SUA ambao ni mabingwa wa kutoa ushauri juu ya kilimo wao wenyewe hawana hata shamba moja la mfano! well majibu yalikuwa mengi lakini ukweli ni kuwa hakuna hata moja lililotosholeza swali la Mh Pinda. sasa nimeweka hili ili kuonesha udhaifu wa wasomi wrtu linapokuja swala la ku implement elimu yetu into reality!

  • Sobe Peter said:

    Asante sana kwa makala yako ya “Maana” Mungu kwanza akubariki sana kwa kazi hiyo.
    nirudi kwenye maada ya msingi nina rafiki yangu anaysoma uingereza naye aliniambia kuwa wenzetu waingreza wanahakikisha kuwa kile wanachokiita limu ya msingi ni ya msingi ki kweli kweli mathalani mtoto anayemailiza elimu ya msingi anatakiwa kujua baadhi ya vitu vilivyo vya msingi kwa mfano:
    1.kijana wa kitanzania anamaliza kidato cha 6 ila hajui hata mlo kamili(balanced diet)
    2.kijana anamaliza kidato cha 6 hajui kuwa utapiamlo unasababishwa na nini ukimuuliza anasema kuwa ooh mimi nimesoma uhandisi hayo hayanihusu au mimi nimesoma masomo ya sanaa.
    kiujumla ndio maana maendeleo ya elimu itabaki ya kufaulu sana na si kumuanda mtu aweze kupambana na mazingira yetu.

  • OB said:

    Wanangu na ndugu zangu,
    Ninashukuru kwa makala haya. Na ni kweli na ni kweli tupu. Hoja kubwa sana ila nitaiendeleza kwa kuona nimeshambuliwa kidogo. Mimi ni mmoja wa hao waalimu wenye kutegemea nime_publish jarida ngapi. Kwa hilo nadhani ni la lazima kwa sababu ni kigezo chetu swali liwe kuwa ni kwenye majarida yapi? na uasilia (originality) iko wapi? Tanzania au kuna kupiga chabo kidogo na kufanya usanii… wenzangu wasinisute kwa maana tupo wale wagushi. Kwani kule primary si kuna walioibia mitihani unadhani yale yaliishia palepale! Turudie mada yetu.
    Si kwamba waalimu hatutaki au hatuwezi huu ni uongo uliokiuka mbali. bali usanii umezidi kwenye vyuo vyetu. hakuna maabara, vifaa na kila kitu kimekuwa kwa vitendo. Kwa wale wanaokumbuka kufanya mitihani ya mazoezi na wale waliofanya alternative… hali inaendelea mpaka kwenye vyuo vyetu. Njoo UDSM ulizia hawa wanaosoma computer engineering maabara yao yako wapi, utaambiwa mazoezi viwandani. wale wa Telecom. engineering vile vile wakati wa industrial training. Na waalimu waende huko? Njoo kwenye maktaba, kama kuna kitabu cha karibuni basi ni miaka si chini ya tano. Halafu ni kimoja. Mtandao je? wangapi wanaweza ku_access international journals? utaambiwa ni budget finyu. Sasa leo hii tufanye vitu kwa njia gani watanzania wenzangu? Tuombe hali ya nchi ibadilike . Ama tuwe tajiri ama nchi itambue umuhimu huu.
    Kwa kumalizia, usisahau kule kuibiwa kwa mitihani ya NECTA…
    Kwa heri.

  • OK said:

    Nimesoma makala na michango yenu kwa masikitiko makubwa sana. Tanzania ni nchi yenye uwezo wa kuondokana na huu ubutu wa kufikiria lakini kama alivyosema mmoja hapo juu tatizo ni muda wa kufikiria mambo kwa mapana kila mtu mwenyewe katika eneo lake. kumekuwepo na fikra tegemezi katika maisha ya watanzania wengi wasomi na hakuna mahali imeonekana hao wasomi walioko ndani na nje ya Tz wanaweza kukutana pamoja wakaweka mawazo yao sawa nakufanya jambo ila wanaishia kulaumu tu.

    Hapa chuoni kwangu UK katika idara moja maarufu sana kwa mazingira wanakutana kila wakati kupeana changamoto za ufanisi na wanatafuta sources of funds kutatua shida wanazokutana nazo. kule kwetu kuna kitu kinaitwa divide and rule kuanzia mashuleni, vyuoni na maofisini, ni mara chache sana uone vikao vya kujadili challenges and the way foward yamambo mbalimbali. mikutano mingi imeishia kwenye kuonyana kuwa usiguse vitu vya wazee,matumizi ya agrarian leadeship na mambo yanayofanana na hayo. Kuna viongozi walipanda cheo kwa sababu ya heshima ya uoga ya NDIO MZEE/BOSI KATIKA KILA KITU, JE WATU KAMA HAO NI LINI WATAKAA CHNI NA KUGUNDUA MAMBO WAKATI ANASUBIRI KUSSEMA NDIO KILA SIKU IITWAPO LEO ILI MWISHO WA MWAKA AITWE MFANYAKAZI BORA.

    Huku kwenye hizi nchi mambo hayaendi bila kuonesha competencies and efficient, unaachishwa kazi kwa tabasamu murua ukiwa hopeless, kule kwetu ukichallenge system ndio unashushwa cheo au unahamishiwa namtumbo ili tu UFIKE MAHALI PA Kuseme hutaki kazi au wakati mwngine unaachishwa kwa maslahi ya taifa ambayo mimi natafsiri kwa kusema kwa maslahi ya wazee wa nchi. Hivi tunaelewa chanzo cha kuhamishwa wizara moja kwenda nyingine hata kama huna huo ujuzi? Basi watanzania wanafurahia hiyo bila kujiuliza sababu nini hasa! Kulikuwa na chama cha wasomi kama mnakumbuka lakini kiliuawa ghafla kwani ilikuwa imeundwa na vichwa vilivyojaa ugunduzi na mzee mmoja kule top used a divide and rule kwa kuwapa wale top leaders vyeo serikalini na chama kikafa.

    Hebu sisi basi tuform mtandao wetu na kutumia mbinu ya infiltration badala ya confrontation kuleta mabadiliko Tz na sio kuongea tu bila kufanya jambo

    Nawasilisha wapendwa wangu

  • neema said:

    kweli ndugu yetu umechambua vizuri sana. maana ata wengine tuna elimu ya juu lakini ata muundo na kazi za serikali za mitaa sijui matokeo yake ata kushiriki ktkmikutano muhimu sishiriki maana sijui hiko vipi. na kituko zaidi ata hao madiwani na viongozi wa mitaa sijui wapo au hapana ni kituko. na hii inatokana na utamaduni tulio nao kutoshiriki na kutokuwa na mechanism za kutufanya tushiriki. matokeo yake ata maamuzi atuwezi kuchangia tunaamuliwa na wachache yanayokuwa hayatuwakilishi tulio wengi.
    tunashukuru sana kwa uchambuzi wake wenye kutujenga atanzania kama tutafuata. Mungu azidi kukupa nguvu uzidi kutufungua macho.

  • Ferdinand said:

    Wanamtandao
    Swala la wasomi kuzagaa bila kazi za kufanya ni kwamba kuna sababu za kisisa kiuchumi na kiutamaduni pia. Kisiasa ni kwamba watengeneza sera (Policies) za kisekta kwanza wanalenga kukidhi malengo ya kisiasa na hivyo kutekelezwa na kusimamiwa kisiasa zaidi kuliko kitaaluma kwa maana ya kutokuwa na wasimamizi wa utekelezaji kitaaluma.
    Sera hizo hazina impact ya wasomi kwa sababu wasomi wenyewe wamesoma kwa rushwa, wamefaulishwa kwa rushwa, hawapati kazi kwa sababu hawana pesa ya kuhonga ili waajiriwe. Wakiajiriwa kwa rushwa hawatakuwa wabunifu kwa kujua kuwa wakitaka kupanda vyeo bila rishwa watabakia pale pale. Kwa hiyo hali ya sasa hata uongozi sharti uwe na pesa ya kuhonga. Huwezi kuwa kiongozi ikiwa hujulikani. Kujulikana kwako ni pesa yako ndiyo itakayokufanya ujulikane kupitia sherehe utakatakazowaandalia wakubwa wakati wa ufunguzi wa nyumba yako yako yakifahalri au sherehe ya ubatizo wako,nk. Ama kupitia mkubwa fulani hivi uliye karibu nawe atakye kukingia kifua kwa umaarufu wake. Bila hivyo kaka ama dada pamoja na tudigrii twako utakuwa unajidanganya bure. Ndiyo kwanza wenye visomo vya chini utawaona wanapeta kwa vyeti vya kughushi. Hata kama unaushahidi wakutosha bado sheria haitafanya kazi dhidi yao shauri ya kitu PESA. Habari ndiyo hiyo.

  • Mdau said:

    Kuhusu waghana sio wamesoma sana ila wameanza kutoka nje ya nje yao miaka mingi ni kama waNigeria.Koffi ANNAN hakupata ukatibu mkuu kwa vile ni Mghana bali ana mke mzungu na ameishi canada kwa muda mrefu.kama ni kigezo ni mitaala tunaye Asha rose Migiro na tibaijuka wamesoma kwetu.

    waGhana wanasaidiana sana hasa wanapokuwa nje ya nchi.mfano university of London metropolitan wako zaidi ya wanafunzi mia tatu wenye asili ya Ghana.

    university of Leicester kwenye distance learning wao ndio wanaongoza kwa number kubwa.
    masomo kama ACCA ni waghana ndio wanafanya kwa wingi. kifupi sera za nchi yao kuwaruhusu kutoka mapema na moyo wa kukumbuka kwao ndio chachu ya wao kupata kazi za kimataifa.

  • Hellen Willy said:

    Japo kwa kuchelewa nami nimesoma na kuona kuwa mada yenu brother inagusa sana jamii ya kitanzania. Changamoto ninayoiona kwa upande wangu ni kwamba hivi sasa waalimu wengi wa ngazi za juu yaani wanaomaliza vyuo vikuu n.k wamekuwe wakiajiriwa na mashirika mengine wakikimbia fani ya ualimu ili angalau wapate kipato cha kueleweka si hao tu bali hata walimu walifanya kazi miaka mingi wakijiendeleza na kupata elimu ya Juu hawarudi tena kufundisha na wanamezwa na mashirika makunbwa .Hawa wangeweza kutusaidia sana kuleta mabadiliko kwa vile wanailewa vizuri system ya elimu yetu na udhaifu wake.
    Pia Naona roho ya ubinafsi inachangia sana kuturudisha nyuma watanzania. Mfano wenzetu wengine wanapata nafasi wizarani kabisa na katika idara nyeti ambako wananafasi kubwa ya kufanya mabadliko lakini wakifika wanatulia na kuacha kila kitu kiende kama kilivyo ili mradi pengine haiwagusi sana wao na familia zao. Si hao tu hata sisi wengine Mungu ametupa nafasi ya kusoma tusaidie jamii lakini maisha yetu yote tunajifikiria wenyewe na familia zetu na kusahau yaliyotutesa sisi ili vizazi vijavyo visipite humohumo.
    Kweli changamoto tunayo ,hivi sasa tunajivuna kuwa kila kata ina shule yake lakini ukifuatilia shule hizo hasa za vijijini na hatari tupu,hazina viwango ,walimu haba nk.
    Let us keep on pressing ,hasa tulio na influence kwenye vyombo vya serikali tatafika tu.

  • Wilfred said:

    nimesoma mawazo hayo kuhusu elimu, ni kweli elimu yetu imekuwa ya kuaandaa watoto kupata A’s maana bila hizo hupati mkopo kusoma chuo kikuu na hata admission ya chuo kikuu inakuwa shida.lakini hasara yake imekuwa kubwa sana, wimbi la vyeti vya kufoji limezidi na ubunifu umepungua kabisa miongoni mwa wahitimu wa vyuo

    elimu ikiendana na uhalisia wa unachokisoma inakuwa elimu barabara inayochochea ubunifu ndani ya mtu. mi nashauri elimu kwa vitendo ipewe kipaumbele toka ngazi za chini za elimu.

  • jose said:

    kichwa cha habari na makala havioani. lengo la makala ni showing off kuh uingereza .

Weka maoni yako hapa!

Add your comment below, or trackback from your own site. You can also subscribe to these comments via RSS.

Be nice. Keep it clean. Stay on topic. No spam.

You can use these tags:
<a href="" title=""> <abbr title=""> <acronym title=""> <b> <blockquote cite=""> <cite> <code> <del datetime=""> <em> <i> <q cite=""> <strike> <strong>

This is a Gravatar-enabled weblog. To get your own globally-recognized-avatar, please register at Gravatar.