Home » Featured, Habari, Headline

Alikotokea Profesa Born Again Pagan na Wenzake: Bwiru Sekondari (Wavulana) 1960-1963 (4)

5 March 2010 578 views One Comment

Shukrani zangu za dhati kwa wasomaji wote wanaoniletea e-mails zao kuhusu hadithi hii inayoendelea.

Stori, kama hii niandikayo, inatufanya tukumbushane mada (themes) sawa lakini kwa miaka na michakato tofauti. Kuna wengi wapendao sana kujua ya mazingira, raha, taabu na mambo mengine yaliyotokea zamani. Kwa mfano, msomaji mmoja amenitaka nitoe maelezo binafsi ya marehemu mzazi wake aliyewahi naye kupita hapo Bwiru (Wavulana), endapo nilimfahamu,

Msomaji mwingine, akitoa mfano wa shule ya Tabora (Wavulana) mwaka 2000: uchafu wa vyoo, ukosefu wa maji na uhaba wa nafasi ya kulala wanafunzi (kiasi cha wanafunzi wengine kulala sakafuni), alitaka kujua endapo nimewahi kuitembelea shule ya Bwiru (Wavulana) hivi majuzi ili kupima hali yake ilivyo. Pengine ni vizuri kuipima Bwiru (Wavulana) katika muktadha wa sasa kuliko kutumia “macho” ya mwaka 1960-63!

Wakati wetu hatukuwa na msongamano, kama mfano huo wa Tabora (Wavulana) kwa baadhi ya wanafunzi kuweka magodoro sakafuni mabwenini! Kwa mifano, kutokana na mwaka wetu kuanza mitaala miwili, “Senior Recreation Room” ilifutwa na kufanywa Library tukiwa darsa la 10. Wakati huo huo, Mess Hall mpya ilianza kujengwa na Mess Halls za zamani moja ikabadlishwa kuwa Library na nyingine pembeni ikawa Geography Room.

Baadaye, ili kukidhi nafasi kwa ma-Darasa 12-A na 12-B jengo jeupe lilijengwa (ingawa liliezekwa kwa vigae vya “asbestos”), ambalo tuliliita, “White House”.

Shule zote za Bwiru (Msingi, Kati na Sekondari) zilikuwa na mashini yake ya kuvuta. Hata hivyo, hapo Bwiru (Wavulana) mazingira ya vyoo hayakuwa mazuri kwa sababu ya kungoja matanki ya maji ya kuvuta (“cistern”) yajae”. Na wakati wa “heavy traffick”, mifereji iliziba; na wakati mwingine maji machafu yalijaa na kufurika siku kadhaa kabla ya kuwasili kwa gari la kufyonza uchafu (cesspit emptier) huo. Mazingira ya shule yalinukwa kwa harufu mabaya. Gari lilimwaga uchafu huo popote hapo milimani!

Inafaa sana izingatiwe kuwa niyaandikayo sana sana ni ya kati ya mwaka 1960 na kumalizikia mwaka 1963 hapo Bwiru (Wavulana) – sizungumzii kwa ujumla ya shule zote za serikali. Hata ya miaka ya nyuma au baadaye hapo Bwiru (Wavulana) ni “outside the scope” ya hadithi hii; nawaachia wengine wayaandike, wakitaka. Ila katika hadithi itakayofuata nitamalizia na ya Tabora (Wavulana) ya wakati wangu.

Ingawa sijaenda Bwiru (Wavulana) kwa muda mrefu, katika kuandika hadithi hii, simaanishi kuwa enzi zetu tuliishi katika “paradisiacal” mazingira. La hasha! Pamoja na mapungufu ya Bwiru (Wavulana), kama hadithi hii itakavyozidi kuelezea hapo baadaye, tulikazana sana tufaulu na kufuzu.

Wakati huo, shule ilikuwa haishindani na mazingira mengine ya “vya usasa” katika kuleta mabadiliko maishani. Pengine hili linahitaji mada tofauti, na niliwahi kulizungumzia katika mfululizo wa maandishi yangu juu ya Kuporomoka kwa Maadili Mema kwa Vijana Wetu (gazeti la KwanzaJamii lililokufa).

Msomaji, ni matumani yangu kuwa waendelea kufurahia “excursionary travelogue” hapo Bwiru (Wavulana) ya wakati wangu (1960-63). Leo tutaendelea kuangalia mambo matano: Mosi, dereva, wapishi na mlinzi wetu wa usiku. Pili, ya “The Oliver Twist School” - mgomo wa tatu nilioshiriki. Mgomo wa kwanza ulikuwa ni hapo Ikizu Middle School wakati wanafunzi kumi tulipogoma kuendelea na masomo ya sekondari katika shule za wa-Sabato. Mgomo wa pili ulikuw nilikataa kubatizwa. Tatu, harakati za kudhibiti siasa na uchumi hapo Mwanza. Nne, mwanafunzi wa Bwiru (Wavulana) alivyoshinda Brooke Bond Tea Literary Competition na kutembelea Uingereza kwa muda wa mwezi mmoja. Tano, Bwiru (Wavulana) daima itamkumbuka Mwalimu Frank Mitchell.

Katika orodha yetu, tulimalizia na nambari kumi.

Kumi na moja, kidogo, nisimulie ya dereva, wapishi na mlinzi wetu wa usiku. Bwiru (Wavulana) ilikuwa na dereva wetu mashuhuri, Bwana Manugwa, ambaye tulimpenda kwa umahiri wa kuendesha ki-gari chetu kidogo kizee cha “van” (rangi ya kijani – kama yalivyokuwa magari yote ya serikali) kilichokuwa wazi, kabla ya shule kuletewa lori kubwa, kama walilokuwa nalo Bwiru (Wasichana). Dereva Manungwa hakuwa mtanashati, kama alivyokuwa mwenzake, Adam wa Bwiru, wa Bwiru (Wasichana).

Dereva Manugwa alitupeleka kwenye vituo vya mabasi, bandari ya meli na stesheni ya treni wakati wa kwenda likizo au kutuchukua kutoka likizoni; kupeleka wagonjwa Hospitalini; kupeleka wachezaji michezoni na kwenye makomangano mjini Mwanza na vitongoji vyake.

Wakati mwingine dereva Manugwa alipuuzia alama za trafiki na sheria zake bila kukamatwa. Nafikiri, aliujua uzembe wa ma-Afisa wa Trafik, kwa upande mmoja. Alipuuzia pia kutokana na gari hilo kubeba wanafunzi wa shule ya serikali, kwa upande mwingine. Dereva Manungwa alikuwa akihatarisha maisha yetu. lkini hatukujali!

kwa mfano, kama kulikuwa na gari lingine mbele, hasa la Bwiru (Wasichana), tulimchokoza, “Potea Manungwa”! Aliweza kupotea kwa mwendo wa kasi na kuyaacha magari mengine mavumbini huko kwenye barabara ya Bwiru mlimani na ya lami – Makongoro Road (Kiwanja cha Ndege-Mwanza Mjini) au Tabora Road kuelekea sehemu za Butimba TTC, Nyegezi Seminary, Rosary College na Nsumba Sekondari.

Tulikuwa na wapishi kama wanne hivi – maarufu walikuwa wazee Ndege na Reli. Wapishi wote walikuwa wanywa gongo na “mapuya” sana. Licha ya ulevi huo, walikuwa ni “very fatherly.” Na mara nyingine walikuwa wakilala katika stoo ya vyakula ili wasichelewe kuandaa ujiwa asubuhi.

Mwenye machachari na ukali alikuwa ni mlinzi wetu wa usiku – mzee m-Kuria, mnywa gongo kama maji! Tulimpachika jina la “Kukuru Kakara”, kaulimbiu aliyopenda sana kuitumia wakati akiwa kazini. wakati wa kuzima taa (“lights out”), alisika akiungunguruma saa nne za usiku, “Kukuru kakara, saa ya kurara sasa!”

Wakati mwingine “Kukuru Kakara” alipenda kufukuza wanafunzi waliokuwa wamezoea kuamka kwa siri usiku saa tisa na nusu hivi kujisomea madarasani kwa mwanga wa vibatari/vikoroboi, hususan wakati wa mtihani ukaribiapo.

“The Oliver Twist School”

Kumi na mbili, kulikuwa na “Bwiru” nyingi: toka Darasa la 1 hadi 12 (wavulana na wasichana). Mtoto aliyezaliwa hapo Bwiru aliweza kumaliza Darasa la 12 akingali katika mazingira ya Bwiru.

Mwaka 1962, moja ya hizo “Bwiru” - Bwiru (Wavulana) - tuligomea chakula. Gazeti la Kiingereza (The Tanganyika Standard) lilituhurumia na kuandika habari za mgomo huo kwa kichwa cha habari, “The Oliver Twist School’, kuufananisha na hadithi ya Oliver Twist iliyoandikwa na Charles Dinkens – juu ya mustakabali wa watoto yatima na masikini walivyokinyanyaswa, kuchapwa viboko na kuteswa katika mazingira magumu ya mapinduzi viwandani huko Uingereza.

Katika hadithi hiyo, huku akitetemeka na kushikilia bakuli lake la chakula, mtoto Oliver alimwendea Mkuu wa Shule kuomba aongezewe chakula: “Please, sir, I want some more.”

Tuliandaa mgomo kwa sababu kiasi cha chakula - uji, ugali na maharage, nyama, samaki na wali (“kitee”) na “la juu” (mafuta ya mawese) - tulichokuwa tumezoea kukipata kilianza kupungua sana. Uongozi wa shule haukutuarifu kwa nini kulikuwa na uhaba wa chakula; hivyo, tukagoma, mithili ya Oliver, “Please, sir, we want some more.”

Nafikiri sababu ya kupunguka kiasi cha chakula ilitokana na kuongezeka kwa mitaala miwili miwili tangu Darasa la 9 (1960) bila kuongeza mapesa. Kwani sio Bwiru (Wavulana) tu iliyogoma mwaka huo; shule za sekondari nyingine (Old Moshi na Tosamaganga) nazo ziligoma, kama sikukosea.

Ma-Prefekti wa zamu siku hiyo ya mgomo, ambamo kila mwanafunzi alishiriki, walikuwa kutoka Speke House: Silas Mayunga na Msaidizi wake Ali Hussein Magomasi. Badala ya kwenda mstarini kukaguliwa (kabla ya kuingia madarasani), tulielekea upande mwingine karibu na Mess Hall na wengine kupotea milimani. Mwalimu wa Zamu aliduwaa tu kutuona tunazila ukaguzi, kabla ya Hedi Prefekti Pamba Masyole (m-Kerewe) kumtaarifu juu ya mgomo.

Mkuu wa Shule A.R. Thompson, aliyeshika nafasi ya Bwana Mull, alitaarifiwa na kuitisha mkutano wa walimu mara moja. Kuona walimu wanajifungia mkutanoni, tulianza kutembea kuelekea mjini ili kutoa kilio chetu mbele ya Mkuu wa Mkoa (Elimu).

Baada ya mwendo wa kama nusu saa hivi, walimu wa-Matumbi wawili (Venables B. Mtabi na Methuselah Kishosha) walitufuata ndani ya gari dogo aina ya Popular la Mwalimu m-Amerika Frank Mitchell. Walitupita; na mara wakasimama. (Nitasimulia msaada wa baadaye wa Mwalimu Frank Mitchellkwa shule yake hiyo ya zamani mwishoni).

Mwalimu Methuselah Kishosha alitusihi turudi shuleni kuyazungumza. Ubishi ukawaka moto. Kitambo, Hedi Prefekti akatusihi tuwatii hao walimu wetu wa-Matumbi. Tukarudi shuleni.

Kurudi shuleni, tuliambiwa kukaa hapo shuleni bila kufanya fujo bila kubaini kuwa Mkuu wa alikuwa ameishamwarifu Mkuu wa Mkoa (Elimu), ambaye alimpa maagizo ya kuturudisha shuleni hadi tusikie kutoka kwa Waziri wa Elimu (Waziri Solomon Nkya Eliufoo, MP) na Kamishina wa Elimu (Bwana Dunstan Omari), Dar es Salaam!

Mara ujumbe ukafika. Akizingatia kuwa huo mgomo haukumlenga yeye (Bwana Thompson, kama Mkuu wa Shule) bali ulilenga serikali yetu huru, Mkuu wa Shule aliitisha mkutano na kutamka maneno makali, mithili ya mbogo mkali, kama ifuatavyo:

“You have decided to go against your own government. The warning message from your government is that you will all be sent home; and home you will go, immediately! Your warrants are being prepared. Go and pack your belongings ready to go home!”

Huo ujumbe haukuingia vizuri ndani ya masikio ya baadhi yetu na kusababisha Mkuu wa Shule kurudia kwa ukali:

“Disperse to your dorms to pack up your belongings! After packing, you must all come to the Office for your return travel warrants to your respective homes! The school is closed until the start of the next term!”

Tulitawanyika kama vifaranga kwa unyonge mkubwa! Tulikuwa tumebakiza mwezi mmoja wa kumaliza nusu muhula wa shule. Tulipewa hizo “return travel warrants” na kujipa moyo kuwa wote tutarudishwa.

Kwa kawaida sisi kutoka Mkoa wa Mara tulikuwa tukisafiri kwa meli - wakati huo meli mpya kabisa ya MV Victoria. Lakini siku hiyo sisi kutoka Mkoa wa Mara tulisafirishwa kwa njia ya basi la kampuni ya Tanganyika Bus Services hadi mjini Musoma, na hapo baadaye, kujipakia kwa mabasi yaliyotupeleka hadi nyumbani kwetu. Na wa kuelekea sehemu za Kwimba na Shinyanga walikuwa wakisafiri kwa treni. Siku hiyo walipelekwa kwenye stesheni kupanda treni lililokuwa lisafiri siku hiyo, na hapo baadaye wapande mabasi hadi majumbani kwao.

Wazazi wangu walishangaa kuniona nimewahi kuja nyumbani. Kabla ya kuniuliza kisa cha kuwahi, nilidakia kuwaambia kisa chenyewe. Kumbe walikuwa tayari wamepata habari kupitia redio juu ya kufukuzwa kwetu.

Kwa ukali, Mama alinijibu, “Tulikupeleka Bwiru kusoma; sio kugoma”!

Nilikaa hapo nyumbani kwa mapumziko marefu ya miezi miwili (“likizo ya kufukuzwa”) na kurudi shuleni kumalizia muhula uliobakia na mwisho wa mwaka. Chakula kili-“improve” sana baada ya huo mgomo!

Kumi na tatu, mwaka ulioanza, m-Matumbi wa kwanza Bwana Venables B. Mtabi alichaguliwa kuwa Mkuu wa Shule badala ya Bwana A.R. Thompson aliyepewa uhamisho kwenda Makao Makuu ya Wizara ya Elimu, ambako alishughulikia suala la kutunga muhtasari wa kufundisha Historia (Mafunzo ya Ualimu).

(Tulimkuta Bwana A.R. Thompson mwaka 1966 Institute of Education, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, akifundisha jinsi ya kufundisha Somo la Historia kabla ya kufunga virago vyake na kurudi kwao Uingereza.)

Kumi na nne, niliona michezo ya maajabu ya sarakasi kwa mara ya kwanza hapo Mwanza (1960). Kundi la Circo Brasil lilikuja kutumbuiza hapo kwenye sehemu ya Kirumba (Uwanja wa Mpira wa sasa): mapikipiki ya kasi ndani ya tufe la chuma, temb waigizaji, na kadhalika. Kila mara Circo Brasil iliwatumbuiza watazamaji kwa nyimbo mbalimbali. Wimbo uliotia fora ulikuwa ni ule wa Marina (fungua Youtube uusikie).

Kumi na tano, Mwanza ilivuma wakati huo, ki-siasa na ki-uchumi. Sana sana, ki-siasa kati ya Tanganyika African National Union (TANU) ya Julius Kambarage Nyerere (siasa za utaifa wa Mseto) na African National Congress (ANC) ya Zuberi Mwinshehe Manga Mtemvu na mzee mmoja kwa jina Saidi Chamwenyewe (siasa za u-taifa wa Mwafrika), ambao walikuja kwa nyakati tofauti kuhutumbia wananchi wa mji wa Mwanza hapo kwenye Uwanja wa Kirumba; na siasa kali za u-Temi kujiunga na siasa mpya au hapana wakati wa-Koloni wakiwa na njama zao za kuunda Temi kubwa kupitia sera ya kuwa na Paramount Chief huko u-Sukumani, kama walivyofanya huko u-Chaggani.

Zaidi, ushirikiano kati ya siasa na vyama vya ushirika na jinsi TANU ilivyopiku wanachama wa Chama cha Ushirika cha Victoria Federation of Cooperative Unions (VFCU) - vyote vikajikuta vinakabiliana na adui mmoja (kisiasa na ki-uchumi); kuzuka kwa chama kingine cha siasa kilichoanza kama cha ushirika kupambana na VFCU; siasa kali za TANU huko Geita zilizoleteleza FFU kuingilia kati, mbali ya woga wa “Mau Mau” mpya; na siasa za mfumo wa ui-ubaguzi (“tripartite system”): wa-Ulaya (thamani 3); wa-Hindi (thamani 2) na wa-Matumbi (thamani 1).

Hakuna utafiti wenye kuelezea mchakato huo wa siasa na uchumi kama wa G. Andrew Maquire, ambaye alifanya utafiti huo tukiwa Darasa la 10 na kuwahi kututembelea kwa mwaliko wa Mwalimu Bob Amos, m-Amerika mwenzake. Baadaye, Bwana Maguire aliandika utafiti huo kama kitabu, Towards Uhuru in Tanganyika: The Politics of Participation (Cambridge University Press, 1969).

Ki-uchumi (retai trade – dukawalla), Mwanza ilikuwa ya wa-Hindi, kwa mifano, familia za Patel, Chopra na wengineo. Familia ya Chopra ilikoga na kuranda barabara za Mwanza kwa magari mawili ya fahari aina ya Royce-Rolls pamoja na moja la Mzungu wa Schumann’s Garage. Wengi wa wa-Hindi matajiri wa Tanganyika ya wakati huo walijiunga na TANU na kukisaidia kwa mapesa: Chopra na Patel (wa Mwanza), Amir Habib Jamal, Mahmoud Rattansey, Karimjee Jivanjee, Sophia Mustafa, Alnoor Kassam, Sir Chande (wa Tanga/Dar es Salaam), na familia nyinginezo.

Mwanza ilikuwa pia ya wa-Ulaya wa migodi wakitokea Shinyanga, Geita na Kiabakari/Buhemba, Musoma. Wengine walifanya kazi East African Common Services Organisation iliyokuwa na Makao Makuu ya Utafiti wa Tiba, hasa kichocho (schistosomiasis).

Nakumbuka wanafunzi kutoka sehemu za Usukumani wa Middle School na hapo shuleni kwetu walipimwa na kukutwa na kichocho. Walichaguliwa kupewa tiba-tafiti kwa kudungwa sindano. Matokeo yake wakaugua hoi kwa muda wa siku mbili hivi, hadi shule ikasimamisha tiba-tafiti hiyo!

Wa-Ulaya waliishi hapo Capri Point, Bwiru Hills na sehemu ya Isamilo. Kulikuwa na vilima vya Pisii na Disii; nyumba zao zilijengwa hapo vileleni.

Kumi na sita, wakati huo kusikia kuwa mtu kapigwa bunduki na kufa lilikuwa ni tukio la kutisha sana. Hata hivyo, mwaka 1960 huko sehemu za Malampaka, askari koplo mmoja wa Relwe mwendwazimu aliua watu watatu kwa bunduki ya Askari Jela wa wakati huo.

Askari wa FFU wa West Lake, Mwanza, East Lake, Arusha na Western Province walijipanga kumsaka mtuhumiwa, Ambale Sichenga - m-Luhya wa Kenya – askari wa Relwe. Wakati huo Askari Polisi wa Relwe walikuwa wa Afrika Mashariki – waliweza kupelekwa kufanya kazi popote Afrika Mashariki.

Shule ilitahadharishwa na kuomba kutoa habari mara moja kwa Polisi endapo mtuhumiwa angeonekana. Alionekana kajificha mstuni huko Malampaka; mapambano yakawaka moto. Mtuhumiwa alikamatwa baada ya kuishiwa risasi. Hofu ikaisha! Koplo Ambale Sichenga alihukumiwa kunyongwa.

Brooke Bond Tea Literary Competition

Kumi na saba, kila mwaka, Kampuni ya Chai nchini (Tanganyika Brooke Bond Tea Company) ilikuwa ikitayarisha mashindano ya kuandika insha kwa Kiingereza kwa Darasa la 11. Na kampuni–dada za Brooke Bond Tea nchini Kenya, Uganda na Zanzibar nazo zilikuwa zikitayarisha mashindano ya namna hiyo. Mshindi kutoka kila nchi alikuwa akipewa zawadi, zikiwa ni pamoja na safari ya kwenda Uingereza kwa utalii wa mwezi mmoja akiandamana na Mwalimu-Msindikizaji kutoka shuleni kwake.

Mwaka wetu (Darasa la 11) tuliambiwa kuandika insha yenye kichwa, “The Importance of Drinking Tea” (yenye maneno yasiyopungua 500). Insha zetu zilisahihishwa kwanza hapo shuleni. Insha ya Kidollah Makani ilipata ushindi wa kwanza. Kidollah alizidi kuinoa kazi yake; na shule iliwasilisha insha-nolewa mbele ya Tanganyika Brooke Bond Tea Company na kushinda zawadi ya kwanza nchini Tanganyika mwaka huo.

Ushindi wa Kiodollah Makani ukawa ni wa Darasa la 11 - Mwaka 1962 Bwiru (Wavulana)! Ushindi kwa Bwiru (Wavulana) Mwaka 1962! Ushindi kwa Mkoa wa Mwanza Mwaka 1962! Kwa muda wa miaka mingi, Tabora (Wavulana) ndio ilikuwa inaongoza kwa ushindi.

Kidollah Makani na Mwalimu wa Hesabu Venables B. Mtabi (Mkuu wa Shule Msaidizi) waliongozana hadi Uingereza na kurudi kutusimulia ya safari yao.

Bwiru (Wavulana) Daima Itamkumbuka Frank Mitchell

Napenda kuhitimisha kwa mchango wa Mwalimu Frank Mitchell kwa Bwiru (Wavulana), shule yake ya zamani. Nilipofika hapa Amerika (1975), nilijitahidi kuwatafuta hao walimu wetu wa-Amerika waliotufundisha enzi hizo hapo Bwiru (Wavulana). Wawili walikuwa ni wa kundi la “Teachers of East Africa” : Bob Amos na Frank Mitchel. Wengine walikuwa ni wa kundi la US Peace-Corps: Bruce Levine, Berkowitz na wengineo.

Nilifanikiwa kuwasiliana na kukutana na mwalimu wangu wa zamani, Frank Mitchell (aliyekuwa Mwalimu Biolojia). Alikuwa akifundisha hapo Ohio State University. Mwalimu Frank alifurahi sana kukutana nami. Tulibadilishana ya maisha ikiwa ni pamoja na kumtaarifu kuwa mmoja wa wanafunzi wake (Mwalimu Phillip Mussa) ndiye alikuwa Mkuu wa Shule. Mwalimu Frank aliahidi kuitembelea shule yake hiyo ya zamani.

Zaidi, tulijadili jinsi ya kuisaidia Bwiru (Wavulana) kwa kuipatia vifaa vya komputa na kuiunganisha shule yetu hiyo ya zamani kwa Internet. Niliwasiliana na (na kupata ushirikiano wa) Mkuu wa Shule Mwalimu Phillip Mussa (tuliyekuwa naye darasa moja) kumweleza juu ya ka-projekti hako na jinsi ya kukafanikisha kwa kuingiza vifaa vya komputa bila ushuru.

Kutokana na habari kutoka kwa Frank, mpango huo ulifanikiwa mwaka 2005 wakati alipotembelea shule yake hiyo ya zamani na kutoa zawadi za komputa na “internet connection” kwa Mkuu wa Shule - wakati huo, Mr. Elia Kissuu. Lakini sijui sasa mambo yakoje!)

Picha zifuatazo (zinapatikana http://www.tea-a.org/ - angalia upande wa Schools/Tanzania) ni kutokana na juhudi za kukutana kwangu na Mwalimu Frank Mitchell:

Bwiru Boys: Mr. Frank Internet Cafe

Din webbläsare kanske inte stöder visning av den här bilden.

Mipangoni: Frank na Hedimasta Elia Kissuu

Din webbläsare kanske inte stöder visning av den här bilden.

Ujenzi wa Mapokezi ya Internet (Communication Tower)

Din webbläsare kanske inte stöder visning av den här bilden.

Mwalimu Frank Mitchell anabadilishana mawaidha na baadhi ya wananchi

Din webbläsare kanske inte stöder visning av den här bilden.

Wanafunzi wanafundishana ujuzi wa Internet

Din webbläsare kanske inte stöder visning av den här bilden.

Mwalimu gwiji anakagua baadhi ya kumputa zilizotolewa zawadi tayari kwa kazi

Asante sana Mwalimu Frank Mitchell!

Msomaji mpendwa, karibu tunafikia mwisho wa safari. “Leg” yetu ya mwisho itaangalia ya “utoto” – wakati mwingine wanafunzi tunatenda vi-ji-mambo vya ajabu ajabu tu, kama watoto wadogo; mwenzetu alivyopata skolashipu kusomea u-Daktari Algeria; Mtihanii wa Cambridge School Certificate “Ordinary Level” wa Kumaliza Darasa la 12 na uteuzi wa kuingia Darasa la 13 bila majibu kutoka Cambridge; na ya kujiunga na kuhitimu Tabora (Wavulana), kwa kifupi tu.

E-mail: romuinja@yahoo.com

One Comment »

  • Born Again Pagan said:

    Msomaji, kunradhi, picha za Bwiru za mradi wa komputa zawadi kutoka kwa Mwalimu Frank Mitchell hazikutokea.

    Hata hivyo, picha zenyewe zapatikana: http://www.tea-a.org/ (kama nilivyodokea).

    BAP

Weka maoni yako hapa!

Add your comment below, or trackback from your own site. You can also subscribe to these comments via RSS.

Be nice. Keep it clean. Stay on topic. No spam.

You can use these tags:
<a href="" title=""> <abbr title=""> <acronym title=""> <b> <blockquote cite=""> <cite> <code> <del datetime=""> <em> <i> <q cite=""> <strike> <strong>

This is a Gravatar-enabled weblog. To get your own globally-recognized-avatar, please register at Gravatar.