Home » Featured, Habari, Headline

Woga Wa Mgombea Binafsi Katika Uchaguzi Unatoka Wapi?

25 February 2010 174 views No Comment

WIKI iliyopita nilijadili jinsi ambavyo chama tawala cha (CCM) kilivyowapora wananchi haki ya kujua hatima ya watuhumiwa wa kashfa ya Richmond kwa mtindo wa ‘funika kombe mwanaharamu apite’.

Watu wengi walinipigia simu na kushiriki katika mjadala huu wengi walionyesha masikitiko makubwa jinsi mjadala huo wa Richmond ulivyofungwa kibabe na Bunge na hata wengine kufikia mahali kuhoji uzalendo wa viongozi wetu.

Vilio vya wasomaji wangu hawa wanaolalamikia utendaji wa serikali vinatoa picha kwamba, sasa wananchi wengi nchini wamechoshwa na jinsi serikali inavyoendesha mambo yake. Sio jambo la ajabu leo ukipita mitaa ya watu wa kipato cha chini kuanzia kwenye daladala hadi mitaani utasikia watu wakilalamika juu ya maisha magumu.

Wapo ambao wanalalamika juu ya wizi wa mali za umma unaofanywa na baadhi ya viongozi, wapo wanaolalamikia tabia ya viongozi wetu kulindana pale mwenzao anapoingia katika kashfa na wengine wakishangaa kuona namna viongozi wanavyowafanyia usanii kutekeleza mambo ambayo waliahidi kuyafanya wakati wakingia madarakani. Ingawa wanalia bila ya kutoa machozi, lakini nyuso zao zinaonyesha alama ya kukata tamaa huku wakihoji kwa nini Tanzania iendelee kuwa maskini ilhali ina rasilimali lukuki?

Wananchi hawa wanaendelea kulalamika kuwa serikali imekuwa ikiwafanyia mchezo mchafu wa kuwanyima haki yao ya msingi ya kupata mgombea binafsi, ili waachane na kulazimika kupitia vyama vya siasa, hususan CCM. Wengine bado wanakumbuka rafu waliyochezewa kupitia Bunge la Jamhuri ya Muungano ya kuzima hoja ya kashfa ya Richmond na huenda kashfa nyingi zitakufa hivyo hivyo ili kuilinda CCM. Lakini, ninajiuliza kwa nini Watanzania hawa wanalia wakati viongozi hao hao, wanaowalaumu ndio wamekuwa wakiwachagua kila uchaguzi mkuu unapofanyika na kuwarejesha tena madarakani?

Katika nchi nyingine, wananchi hutumia kura kama fimbo ya kuwapigia viongozi wabaya na kutowapa ridhaa ya kuongoza tena na hii huwapa funzo kubwa viongozi wanaochukua madaraka kwamba uongozi ni dhamana ukiharibu unaondoka. Sasa tujiulize kwa nini wananchi walio wengi nchini wanakubali tuendelee kuongozwa na watu hawa?

Inawezekana kabisa kwamba, uchaguzi wetu katika baadhi ya maeneo unagubikwa na vitendo vya ukiukwaji wa taratibu za uchaguzi kwa lengo la kunufaisha mtu fulani au chama tawala, lakini hii haiwezi kuwa sababu kama watanzania wengi watakuwa wamepata mwamko wa kujitambua.

Tatizo kubwa la Watanzania walio wengi ni kushindwa kuchambua vitendo na maneno ambayo yanasemwa jukwaani na viongozi wetu. Kwa bahati mbaya kabisa hata wakiteseka miaka yote, lakini ikifika uchaguzi maneno matamu ya ulaghai na takrima za pilau na fulana zinawafanya wasahau maisha magumu ya miaka mingi waliyoishi. Tatizo letu ni nini sasa? Tunahitaji mapinduzi ya fikra. Kama hakuna mapinduzi ya fikra si rahisi kufanyika mabadiliko yoyote ya manufaa.

Leo hii tujiulize ni wananchi wangapi vijijini na mijini, wasomi na wale wasiokuwa wasomi ambao wanajua thamani ya kura yao? Ni wananchi wangapi wanaojua kuwa kura yake ikichanganywa na kura za wenzake inaweza kuondoa kuendelea kuwepo kwa mikataba mibaya ya kuuza madini yetu inayosainiwa kwa siri nje ya nchi?

Ni wananchi wangapi wanaojua kuwa kura yake ina thamani ya mamilioni ya dola na shilingi na inaweza kujenga barabara ambazo zimeshindikana tangu nchi ipate uhuru jimboni kwake? Katika mwendelezo huo huo, leo hii serikali kwa makusudi imeamua kukaidi kuruhusu mfumo wa kidemokrasia wa mgombea binafsi katika uchaguzi. Kisa ni kuilinda CCM isianguke.

Wanajua wazi kuwa wagombea binafsi wakiruhusiwa wapo watu wengi waliopo ndani ya bunge wanaweza kuamua kusimama katika majimbo kama wagombea binafsi wakashinda na hivyo kupunguza idadi ya wabunge wao bungeni. Ingawa kihistoria mgombea binafsi kushinda ni vigumu katika nchi nyingi zilizo na mfumo huu; watanzania waachwe waingie kupimana ubavu na wagombea wengine wa urais na wabunge akiwemo Rais Jakaya Kikwete.

Hiyo ndiyo demokrasia. Suala la mgombea binafsi siyo geni nchini, lilishafanyiwa utafiti na kuzungumziwa katika Ripoti ya Jaji Robert Kisanga na Tume ya Jaji Francis Nyalali hata Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere wote waliafiki kuwepo kwa mgombea binafsi ili kupanua demokrasia nchini.

Sasa woga huu wa serikali ya CCM kuwepo kwa mgombea binafsi unatoka wapi? Kama CCM inaweza kusimamisha wagombea wazuri kuanzia urais hata ubunge wanaokubalika, kwa nini iwe na wasiwasi na hawa watakaosimama peke yao ambao nafasi yao ni finyu kwa vile wanategemea kuchaguliwa na masalia (wananchi wasio na chama )?
(chanzo:http://mwananchi.co.tz)

Weka maoni yako hapa!

Add your comment below, or trackback from your own site. You can also subscribe to these comments via RSS.

Be nice. Keep it clean. Stay on topic. No spam.

You can use these tags:
<a href="" title=""> <abbr title=""> <acronym title=""> <b> <blockquote cite=""> <cite> <code> <del datetime=""> <em> <i> <q cite=""> <strike> <strong>

This is a Gravatar-enabled weblog. To get your own globally-recognized-avatar, please register at Gravatar.