Alikotokea Profesa Born Again Pagan na Wenzake: (3)
Msomaji mpendwa, tumeishaona ya ujumbe mfupi uliotilia mkazo umuhimu kwa wale tuliopata nafasi ya kusomeshwa bure (au kusoma hapo mashuleni kwetu) kuweza kuanzisha alumna kwa shule zetu tulikopitia (msingi, kati na sekondari). Iatubidi tuunde uwezekano wa kuzisaidia, ikiwa ni pamoja na wastaafu wake kujitolea kufundisha, kila watembeleapo shule hizo.
Zaidi, tuliona baadhi tu ya wanafunzi waliofuzu hapo Shule ya Sekondari Bwiru (Wavulana) – 1959-1964; jinsi wenzangu na mimi tulivyowakimbia wa-Sabato (Ikizu Middle School), Musoma, East Lake Province (wakati huo); wanafunzi wenzangu walivyokatazwa kuandika Mtihani wa Darasa la 8 hapo Ikizu Middle School; kujiunga kwangu na Bwiru (Wavulana); na mchakato au mkakati wa uhuru wa kuabudu.
Kwa wale wote wanaozidi kuwasiliana nami, asanteni sana kwa maoni yenu!
Masomo
Leo tutazidi kuangalia kwa mpito ya hapo Bwiru (Wavulana) kuhusu masomo na “debating societies”; na burudani - hafla za densi (“mauno” na “milongo”), “makombora” na “wakamba”.
Niliorodhesha kufikia nambari mbili.
Tatu, Darasa la 9 lilikuwa na mitaala miwili yenye idadi ya wanafunzi 90 – kila mtaala wanafunzi 45. Mwisho wa mwaka, tulifanya mtihani wa kuchagua ni nani awekwe Darasa la 10-A au 10-B. Uteuzi ulitegemea matokeo ya mtihani huo.
Mwanafunzi wa kwanza ndiye alichaguliwa kuingia darasa la 10-A kwanza (na kuketi safu ya nyuma kwenye kona moja) na wengine kufuatia. Wanafunzi waliokuwa na maksi za chini ndio walikaa ma-deski ya safu ya kwanza - mbele ya darasa (ubao na mwalimu).
Kwa bahati nzuri nilikuwa wa kwanza darasani kuingia Darasa la 10-A. Nikawa wa kwanza kuingia na kukaa Darsa la 10-A nikifuatiwa na Phillip Mussa, Donatian Mwita, Matayo Henge, Zakayo Igenge, Charles Mashala, Amos Petro Dabana, Hussein Bakari Mbaruku, Revocatus Budodi, Isaac Chitama, Methusellah Ndaki na Julius Ndaki, na wengine wakafuata hadi kufikia wa 45.
Mwanafunzi wa 46 ndiye alikuwa wa kwanza kuingia Darasa la 10-B. Utaratibu huo huo ulitumika katika kupanga mahali pa kukaa darasani.
Kulikuwa na “quizzes” za kila siku/juma; mtihani wa kila somo mwishoni mwa mwezi na nusu muhula kabla ya mtihani wa kumaliza muhula. Wote tulichukuwa masomo bila kuchagua hadi Darasa la 11 (Arts na Sayansi/Hesabu). Tulikuwa na kitabu kimoja tu (text book) kwa kila somo: Arithmetic, Geography, Biology, Chemistry, Physics, English, Kiswahili (kila darasa na kitabu chake maalum) na Health Science!
Vitabu hivyo vilikuwa vimeandikwa kwa miktadha ya ukoloni (kasoro vya Kiswahili). Baadaye, tulipata kitabu kizuri cha somo ya Geography kilichoandikwa na wasomi wa Afrika Mashariki na kuhaririwa na Prof. Simon Ominde wa Kenya.
Vitabu vya ziada vilikuwepo hapo Maktaba yetu duni. Tulitegemea sana Maktaba ya British Council mjini Mwanza. Baadaye, British Council walitoa zawadi ya seti nzima ya Encyclopaedia Britannica –ingawa umahiri wetu wa Kiingereza uliathiiri uelewaji elimu na mafunzo yaliyokuwemo ndani ya vitabu vya seti hiyo!
Tulikuwa na timu mbili za Debating Society: Darasa la 9 na 10 (Junior Debating Society) na Darasa la 11 na 12 (Senior Debating Society). Tulishindana na shule-nyenza kwa midahalo kemu kemu: Racial Marriage is Useful, The Importance of Independence, Racially Integrated Schools Should be Encouraged, Educating Girls is More Important Than Educating Boys, East Africa Should be Integrated, na kadhalika.
Walimu walikuwa kwanza ni wa-Uingereza na wa-Matumbi wachache. Walimu wa-Ulaya wengine walikimbia baada ya uhuru. Kwa mfano, Mwalimu Pinock wa Jiografia, Mkuu wa Shule Mull na Mwalimu wa Fizikia Stenberg (?) (jina lake kidogo limenikimbia). Bwana Stenberg (?) alituambia siku moja, “I do not want to teach you because you’re now independent. I am going to teach in Kenya, which is not yet independent.”
Baada ya juma moja, hatukumuona Bwana Stenberg (?)! Tulisikia habari tu kwamba alikuwa anafundisha Thika High School, Kenya!
Nafasi za walimu wa-Uingereza zilizibwa na Mwalimu wa Kiingereza m-Pakistani akisaidiana na mkoloni mmoja, ex-District Officer. Walimu wengine walikuwa ni ma-Amerika na ma-Peace Corps (Bob Amos, Frank Mitchell, Bruce na wengineo).
Nne, kutokana na maono na uongozi bora wa Julius Kambrage Nyerere na TANU, tulipomaliza Darasa la 9 na kuingia Darasa la 10, ilitangazwa kufutwa kwa Territorial Standard Ten Examination. Mtihani huu ulikuwa kikwazo-chuja kikubwa kwa ajili ya uchache wa sekondari zenye Darasa la 11. Kufutwa kwa mtihani huo, kulituwezesha wanafunzi tulioingia Darasa la 9 kumaliza Darasa la 12, bila wasiwasi.
Tano, zaidi, kutokana na maono na uongozi bora wa Julius Kambrage Nyerere na TANU, wakati tunaingia Darasa la 11, karo ya shule iliondolewa nchini, ikiwa ni pamoja na kuacha mfumo wa “Mock Examination” wa kutoa woga kwa kujipima uwezo wa kukabili Cambridge School Certificate “Ordinary Level’.
Sita, wakati huo huo, ikatangazwa kuwa mwakani wanafunzi waliokuwa wakifanya vizuri,”academically”, wangechaguliwa mapema kuanza Darasa la 13 bila kungoja matokeo ya Cambridge School Certificate “Ordinary Level’ kutoka Uingereza mwezi Februari.
Burudani
Saba, naikumbuka Bwiru ya wakati huo kwa burudani zake. Kila mwanzo/mwisho wa mwaka tulikuwa na densi na shule ya jirani, Bwiru (Wasichana), mbali na “party” za ma-Bweni: Speke, Grant, Livingstone, Stanley na Cameron - mabweni hayo yalibadilishwa na kuitwa majina ya wazalendo – ma-Chifu wa Tanganyika waliopambana na wakoloni; kwa fano, Bweni letu la Stanley liliitwa Sina.
Ma-bweni ya Wasichana nayo yalikuwa yaki-“reciprocate” ikutukaribisha kwenye hafla za namna hiyo hapo shuleni kwao. Na wakati mwingine wasichana wa kutoka Rosary College (Nganza) walialikwa, licha ya uhasama baina ya hizo shule mbili za wasichana.
Tuliita hafla hizo “kushika mauno” au, kwa kifupi, “mauno”! hafla zilichukua muda wa saa mbili tu (toka saa mbili hadi saa nne usiku). Wakati mwingine Mwalimu aliyekuwa ameandamana na wasichana aliongeza muda wa nusu saa zaidi. Vinywaji na vitafunio vilikuwa ni soda za Fanta, Coca Cola/Pepsi na Biskuti)!
Wanafunzi wa Darasa la 9 walihimizwa kujifunza kucheza densi (rumba, chachacha, bolero na rock-n-roll/twist) ili wasiabike wakati wa hafla au kucheza na kukanyaga miguu ya ma-patna wao. Ilitubidi tuvae “milongo” (suruali) wakati wa hafla hizo; wengi tulivaa za kuazima kutoka kwa wenzetu.
Tulikuwa kila Jumamosi na Jumapili tunatumia muda wetu mwingi tukicheza densi (na pia kusikiliza taarifa za habari - Nairobi na BBC) kwa kutumia redio. Redio yetu ilikuwa aina ya Grundig isiyo na transistors - ikikamata vizuri stesheni za Kongo: Bukavu, Stanleyville (Kisangani) na Elizabethville (Lubumbashi) na za Kampala na Nairobi kuliko Dar es Salaam.
Kati ya hafla zilizotia fora, ilikuwa ni ya “Seniors” wa mwaka 1961. Kwa kawaida tulicheza muziki kutoka santuri bila spika. Lakini hafla ya mwisho ya Seniors hao walialika Bendi moja ya wa-Kongo wakimbizi iliyokuwa matembezini mjini Mwanza (kutokana na vita ya wao kwa wao – ambapo Waziri Mkuu Patrice Emergy Lumumba aliuawa ki-katili chini ya njama za wabeberu).
Bendi hiyo ilikuwa imetoka Bukavu na vyombo vya muziki wa elekroniki. Jioni/usiku huo, sisi ma-“Juniors” na baadhi ya ma-“Seniors” wengine (ambao hawakubahatika siku hiyo kupata kura ya kuchaguliwa) hatukulala! Tulizunguka Mess Hall tukishangaa kusikiliza jinsi muziki ulivyokuwa ukitoka kwa sauti nzuri na ya burudani kweli! Walimu wwa zamu walikuwa wakizunguka Mess Hall kutufukuza; lakini wapi!
Bendi hiyo ilipiga nyimbo za African Jazz: Vive Patrice Lumumba (Vicky Longomba); M.N.C. Uhuru, Table Ronde na Indépendance Tcha-Tcha (Joseph Kabasselé) ukiwasifu viongozi wa nchi huru ya Kongo (Leopoldville), Merengue Scoubidou (Docteur Nico Kassanda) na Mawonso Mpamba (Déchaud); na nyimbo nyinginezo.
Msomaji, fungua Youtube usikilize utamu wa nyimbo hizi zitakazokuchukua “vicariously” hadi enzi zetu hizo!
Nane, hakuna aliyepita Bwiru bila kujua “makombora” - barua za mapenzi kati ya wanafunzi (wavulana na wasichana)! Wasichana wa-Katoliki, waliokuwa wakija kusali kwetu Jumapili, walikuwa wakifungasha hayo “makombora”, kama walivyokuwa wavulana (wa-Inland Mission/Baptist) walioenda kusali kwa wasichana na kubeba “makombora” kutoka kwetu.
Wakati wa kukoga ni nani mwenye kupokea “makombora” mengi ulikuwa wa “roll-call” jioni ya Jumapili kabla ya mlo. “Makombora” yalikiandikwa kwenye karatasi za “airmail” na kuwekewa poda! Ufunguapo, poda ya marashi ina-“permeate” angani!
Mvulana aliyekuwa “too much obsessed with” wasichana tulimuita, “mkamba”! “Wakamba” walitumia muda wao mwingi kwenye “Valley” (Bonde linalotenganisha shule hizo mbili kuelekea ziwani). Wakati mwingine “wakamba” walipenda kujificha huko kwenye milima ya Mihama – wakati wa wikiendi wanapokosa nafasi ya ruksa ya kutembelea wasichana.
Kila baada ya majuma mawili, tuliruhusiwa kupeleka majina ya wapenzi au jamaa zetu kwa Hedmistresi ili kuwatembelea alasiri toka saa 8-10. Kama mpenzi au jamaa yako alitaka atembelewe, ruksa ilitolewa.
Tisa, mwaka 1962 Mwanza ilipata kutembelewa na ugeni maarufu wa Rais wa Guinea (Conakry) Sekou Toure. Shule za sekondari mjini Mwanza zilitayarishwa sherehe ya kumpokea mgeni huyo na kundi lake wakitoea Uwanja wa Ndege na Mwenyeji wake Rais Julius Nyerere. Waliingia mjini Mwanza ndani ya gari la wazi (convertible) - kati ya magari mawili ya namna hiyo zawadi ya uhuru kutoka serikali ya Amerika.
Baada ya kuwasili na kupumzika hapo mlimani kwa Mkuu wa Mkoa (wakati huo mtanashati Kheri Rashidi Bagdelleh), Rais Sekou Toure alihutubia mkutano wa hadhara kwenye Uwanja wa Mpira wa Nyamagana (kando ya Posta).
Rais Sekou Toure alihutubia kwa Kifaransa. Wengi tungetoka kapa, kama isingekuwa ni kwa ajili ya umahiri wa mkalimani (Kingunge Ngombale-Mwiru), ambaye alijitahidi kufuatilia na kutafsiri, “instantaneously”! Mzee Kingunge Ngombale-Mwiru katoka mbali!
Wengine siku hiyo tukaondoka kwa kukariri neno moja tu la Kifaransa, litamkwalo, puʀkwa (Pourquoi?), ambalo Rais Sekou Toure alirudia-rudia na Kingunge Ngombale-Mwiru kulitafsiri, “Kwa nini?”
Kumi, wanafunzi wengi enzi zetu tulipenda kujipa majina (au kwa lugha ya leo, user names). Bwiru (Wavulana) ya wakati huo nayo haikuachwa kwenye mataa ya kutoonekana “cool”. Yaani, kujiona umefika – kumbe fika hiyo mara nyingi huwa ni ya viini macho (the enigma of arrival) au mangazimbwe, mazigazi au sarabi (“mirage”) tu.
Kwa mifano, Walter Bgoya alijulikana kama Scott (Sir Walter Scott – m-Skoti mwandishi wa riwaya za ki-historia na mashairi); Joshua Opanga kama Watson (Thomas A. Watson, mjenzi wa meli), na Donald John (aliyekuwa mwaka mmoja na akina Silas Mayunga) alijiita Beatles.
Kwa mwaka wangu: Hussein Bakari Mbaruku kama Baker; John Williams Nyagiro kama Cameron na jina lingine Kwamy (Munsi Kwamy wa OK Jazz); Adamu Marwa kama Mujos (Mujos Mulamba wa OK Jazz); Charles Mashala kama Marshall; Reuben Matango kama Faraday (Michael Faraday – mwanasayansi m-Uingereza; na Thomas Kiboko kama Huxley (Thomas Henry Huxley – m-Uingereza – Elimu ya Viumbe).
Zaidi, Suleiman Marando kama de Albuquerque (Afonso de Albuquerque - msafiri m-Reno) na mimi nilijipachika jina la Teddy – kumbe Teddy lilikuwa ni kifupi cha Edward na huku kaka yangu mmoja alikuwa akiitwa Edward - kwahiyo, nilibadili na kujiita Salis (Nick Salis – mpigapicha.
Wengine waliotufuatia nao waliendeleza tabia hiyo. Kwa mfano, Josephia Fanuel Muindi kama Ringo (Ringo Star wa Beatles).
Oh boy, those were, indeed, the days!
Msomaji mpendwa, tutaendelea kuangalia ya mgomo wa tatu nilioshiriki (mgomo wa kwanza ulikuwa ni kukataa kuendelea na masomo ya sekondari katika shule za wa-Sabato na wa pili ulikuwa ni kukataa kubatizwa hapo Ikizu Middle School); harakati za kudhibiti uchumi na siasa hapo Mwanza; na mwanafunzi wa Bwiru (Wavulana) alivyoshinda Brooke Bond Tea Literary Competition na kutembelea Uingereza kwa muda wa mwezi mmoja.
E-mail: romuinja@yahoo.com










Asante sana kwa historia nzuri ya kupendeza enzi zenu hizo zilikua za kupendeza hasa masuala ya elimu yalionekana kupata mkazo mzuri hongera. Shaibu Mwambungu -Mbinga,Ruvuma
mimi twalib abdul hussein niko oxford uingereza,ooh nimefurahishwa sana na flash back ya profesa mimi ni mzaliwa wa mwanza nyegez,kwahiyo flash back imenifanya nikumbuke hadith nying ambazo mzee wangu alikuwa akinipatia kwani yeye amesoma butimba primary school,kwa hiyo nimekuwa nikikumbuka nyumbani na wazee na maisha ambavyo waliyokuwa wanaish ambayo ni nadra sana kwa sasa kuyapata japo walikuwa hawana facility kama tulizo nazo, ooh i cant wait for another chapter,nna ham ya kutaka kujua iliendeleaje, asante sana profesa mimi ni ku wish afya njema ulipo na familia yako,kwa kazi nzuri.
Ahsante kwa historia nzuri Prof. Lakin umewahi hata tembelea Bwiru boys miaka ya karibuni? Habari hii imenifungua macho sana. Mimi nimesomea Tabors Boys na kuhitimu kidato cha sita mwaka 2000. Nakumbuka enzi hizo vyoo vilikua na hali mbaya ukiingia yabidi uvue nguo harufu. Watu walikua wanaweka magodoro sakafoni. Maji km2 mbili kupitia Tabora girls na chemchem ilikua yaitwa Tukutuku. Aibu toka nihitimu sijawahi angalia nyuma. Nimeona haja ya kutembelea shule yangu na kupeleka walau mipira mitano ya mazoezi na kubadilishana mawazo na walimu na wanafunzi na hata changia Tabora School Alumni. Ambayo ipo miaka mingi na enzi twasoma ashukuriwe Nd. Pius Ng’wandu na Juma Kapuya maana walikua wakitumbelea sana na kutupa motisha maana boys ilikua yaitwa kichwa cha Tanzania enzi hizo.
Majid ahsante sana kwa Juhudi zako za kutuamsha na ubarikiwe.
Shukrani.
Jibaulanya
Weka maoni yako hapa!
Maoni mapya
Zinatembelewa zaidi
Makala mpya
Habari zaidi
Burudani