Tu Kama Ng’ombe Kipofu Na Ng’ombe Aliyevunjika Mguu!
Ndugu zangu Wahehe wana msemo; Isenga imbofu na isenga indenyoofu. Kwamba ng’ombe kipofu ni sawa tu na ng’ombe aliyevunjika mguu, wote watakufa njaa. Ng’ombe kipofu hawezi kuyaona majani, na yule aliyevunjika mguu hawezi kujikokota kwenda kutafuta nyasi za kula.
Tafakuri yangu iliyopita nilimalizia kwa kuuliza swali: Je, unafikiaje uamuzi wa ama kuingia vitani, au la? Huu ni mwendelezo wa nilipoishia. Naam. Tunavyoendenda kama jamii wakati mwingine ni sawa na ng’ombe kipofu na yule aliyevunjika mguu. Unaweza kuliona hilo nyumbani kwako, katika ukoo wako na hata mahala pako pa kazi. Tumekuwa jamii ya ovyo ovyo. Tunafanya mambo ya ovyo ovyo. Ni kutoka ngazi ya familia na hata ngazi ya kitaifa.
Ona migongano ya wanasiasa wetu sasa. Ona wanavyogawanyika katika makundi yao. Hawatangulizi hata kidogo maslahi ya wengi. Wanajigawa kwenye makundi kugombania mamlaka. Nikasema huko nyuma; aliye gizani humwona aliye kwenye mwanga na aliye kwenye mwanga hamwoni aliye gizani. Na wakati mwingine, hata yule anayejiona yuko kwenye mwanga, naye pia yuko gizani. Wengi walio gizani ni watu wadogo sana. Ni wanyonge waliobakishwa gizani bila ya walio kwenye mwanga kufanya jitihada za dhati kuwatoa gizani.
Leo kuna makundi ya wanasiasa yanayopigana vita isiyo na tija kwa mtu wa kawaida. Wametafuta visingizio vya kuingia vitani. Kuna wanaodai wanapigana kuwatetea wanyonge walio gizani. Walio gizani nao wameanza kuona katika giza hilo hilo, maana wamekuwa gizani kwa muda mrefu. Wameshtuka. Wanahoji mantiki ya vita vinavyopiganwa kwa niaba yao.
Na walioamua kuingia vitani nao wanaonekana kutojiandaa vema na vita hivyo, wanaelekea kushindwa, maana wanapigana vita vya kinafiki. Na kamwe usiingie kwenye vita ambavyo hujajiandaa vema ili ushinde. Mwingine atasema vita vingine havina budi kupiganwa hata kama hujajiandaa kupigana na kushinda. Hapana, huendi vitani ili mradi tu unakwenda vitani , kama vile unakwenda harusini. Vita si lelemama.
Katika dunia hii inasemwa; chagua vita vyako. Haina maana uchague vita kama unachagua mashati ya mitumba Kariakoo. Ina maana kubwa. Pima kwanza, soma alama za nyakati. Chagua vita inayoshindika, iliyo ya muhimu kupiganwa na unayokuwa na hakika ya kuwa umejiandaa vema kulipa gharama ya ushindi.
Miaka mingi iliyopita kulikuwa na Mfalme wa Epilus aliyeitwa Pyrrhic. Mfalme huyu aliamua kuingia vitani kulikabili jeshi kubwa na lenye nguvu nyingi, ni jeshi la Warumi. Lakini kabla ya Mfalme kuingia baharini na vikosi vyake kuitafuta Italia ya Warumi, msaidizi wake wa karibu, Cineas, aliomba mazungumzo ya faragha na Mfalme. Alitaka kumwuliza maswali na kumshauri.
Cineas alimtamkia Mfalme; “ E bwana Mfalme, Warumi wanasadikika kuwa na jeshi kubwa , lenye nguvu na lenye mashujaa wengi. Ndio maana wameteka nchi nyingi. Je, Mungu akitusaidia, tukaja kuwashinda Warumi, tutafanya nini na ushindi wetu?
Mfalme akajibu: “ Mbona hilo ni swali jepesi sana. Mara ile tukiwashinda Warumi, hakutatokea jeshi kutoka mji wowote wa Italia litakaloweza kupambana nasi.”
Cineas alitulia kidogo, kisha akamwuliza Mfalme: “ Tukishaikamata Italia ya Warumi, kipi kitafuatia?”
Mfalme akajibu: Sicily ni kisiwa chenye hazina za thamani kubwa, itakuwa rahisi sana kukiteka kisiwa hicho.”
Cineas aliendelea kuuliza: “ Bwana Mfalme unaongea juu ya mambo ya kusadikika, lakini una maana kukitwaa kisiwa cha Sicily kutakuwa na maana ya kukoma kwa vita?”
Mfalme akajibu: “ Hapo tutakuwa tumeikaribia Afrika. Na tukishaikamata Afrika ni nani hapa duniani atathubutu kutukabili kivita?”
“ Hakuna” Alijibu Cineas, kisha akauliza; “ Na baada ya hapo tutafanya nini?”
Mpaka hapo Mfalme hakujua Cineas alikuwa anampeleka wapi kwa lojiki ya kifikra. Mfalme akajibu:
“ Baada ya hapo, tutapumzika, tutakula raha. Tutakula na kunywa . Tutabaki tukichekeshana na kucheka, siku nzima.”
Kama ni hivyo, alisema Cineas; “ Ni kitu gani kinachotuzuia kufanya hayo yote sasa bila kwenda vitani? Mfalme hakuielewa hoja ya Cineas. Akakaidi ushauri. Akavipeleka vikosi vyake kupambana na Warumi. Baada ya vita ngumu, jeshi la mfalme liliwashinda Warumi. Hata hivyo lilipata hasara kubwa ya kupoteza watu na kuwa na majeruhi wengi. Jeshi lake likadhohofika sana. Likajaribu kuitwaa Sparta, likashindwa vibaya sana. Mfalme aliwindwa na hatimaye akakakamatwa na kuawa kwa kupigwa mawe kwenye mitaa ya Argos. Isenga imbofu na isenga indenyoofu. Ng’ombe kipofu ni sawa tu na ng’ombe aliyevunjika mguu, wote watakufa njaa. Wanasema ndugu zangu Wahehe. Naendelea kutafakari, nawe tafakari pia.
Maggid ( Mwalimu Wa Zamu)
Iringa,
Februari 4, 2010
+255 788 111 765
http://mjengwa.blogspot.com
http://www.kwanzajamii.com










Kaka Maggid,
Makal yako ni nzuri sana,na inatoa elimu mwanana kwa wanafunzi wa filosofia.Hata hivyo,kama ilivyo ugonjwa wa wataalam wetu wa uchambuzi,haiishauri jamii ifanye nini.
Kwahiyo TUFANYEJE?Twende darasani kumsoma adui?Je itakuwaje pale tutapomaliza kisomo hicho kuhusu adui na tukawa tayari kupambana nae,tukakuta ameshakomba kila kitu?
Kweli vita si lelemama,na inataka maandalizi ya kutosha.Lakini namna unavyoizungumzia vita hiyo ni kana kwamba adui anatoa taarifa in advance kuwa anataka kukuvamia,hivyo kukupa fursa ya kufanya maandalizi.Kwa bahati mbaya katika uhalisia,mara nyingi adui hatoi taarifa lini atavamia.Laiti Nduli Idd Amini angetuhabarisha mapema basi huenda tungemkabili kabla hajafyatua risasi moja.
Tatizo la msingi zaidi katika makala yako ni pessimism unayoonyesha kuhusu “waliongia vitani” na umehitimisha kuwa “wanaelekea kushindwa maana wanapigana vita ya kinafiki”.Yani wanafalsafa mmeshahitimisha kuwa vita hiyo inaonyesha dalili za kushindikana?
Ni rahisi kusema “kamwe usiingie kwenye vita ambavyo hujajiandaa vema ili ushinde” au “Chagua vita inayoshindika” kana kwamba hali halisi inatupa fursa ya kuchagua kila tupendacho na kutuepusha na kila tuchukiacho.Hiyo fursa ya “kuchagua vita” (let alone inayoshindika) unapewa na nani?Adui anakupa fursa ya kuchagua umpige?
Hivi mkoloni,kwa mfano,alitupa fursa ya kuchagua kuondoa utawala wake?Watanganyika walipewa fursa ya kuchagua mapambano na mkoloni?Au Nduli Idd Amin alitupa fursa hiyo?
Na kama suala la kuchagua “vita yako” hudhani uamuzi wa Baba wa Taifa kuchagua vita “zisizo zetu” huko Kusini mwa Bara la Afrika kumesaidia pia kulisaidia kututengenezea majirani wema?Kuna nyakati kuna umuhimu wa kununua ugomvi ilim kujitengenezea usalama wako hususan pale ushindi wa upande mmoja katika “ugomvi usio wako” utapelekea maafa kwako.Ndio logic inayowafanya Wamarekani watumwagie misaada kuwasaidia kujilinda na maadui wao watarajiwa maeneo kama Somalia.
Kuna makupe,mchwa,walafi na wanaharamu wengine kama hao wanatafuna nchi yetu kwa kasi ya ajabu.Tuendelee kuwafanyia mchakato na mchanganuo wa namna ya kuwakabili hadi watakapomaliza “keki ya taifa”?
Mwisho,ningekushauri upatapo muda upitie maandiko kuhusu intervention japo inaweza kuwa sio relevant sana.Tukumbuke pia maneno haya ya busara: “There are risks and costs to a program of action, but they are far less than the long-range risks and costs of comfortable inaction” John Fitzgerald Kennedy (American 35th US President (1961-63), 1917-1963)
“Throughout history, it has been the inaction of those who could have acted; the indifference of those who should have known better; the silence of the voice of justice when it mattered most; that has made it possible for evil to triumph.” Haile Selassie(Ethiopian Statesman and Emperor of Ethiopia from 1930 to 1974, 1892-1975)
“Iron rusts from disuse, stagnant water loses its purity, and in cold weather becomes frozen, even so does inaction sap the vigors of the mind.” Leonardo da Vinci(Italian draftsman, Painter, Sculptor, Architect and Engineer whose genius epitomized the Renaissance humanist ideal. 1452-1519)
Maggid,
Kifilasafa, mwoga aliye hai ni bora kuliko shujaa marehemu. Lakini ni kweli pia kwamba, mwoga ufa vifo vingi tu, kabla ya kifo chenyewe.
Kwa upande mwingine, ipo hoja ya kijamii kwamba maisha ni mapambano; na, mapambano si chaguo bali ni ulazima wa mwanadamu kutumbukia kwenye kidimbwi na kujaribu kuogelea bila ujuzi wa kuogelea.
Si hilo tu, bali katika mapambano (kama yetu tuliyomo)inaweza kufikia hatua tukachagua mojawapo katika haya: kuishi daima tumepiga magoti au kufa tumesimama wima.
Ninaamini wasomaji wako watatafakari mfano ulioutoa wa mazungumzo kati ya Mfalme Pyrrhic na mpambe wake wa karibu, Cineas, katika mantiki hii.
Nawakilisha,
Ludovick
Weka maoni yako hapa!
Maoni mapya
Zinatembelewa zaidi
Makala mpya
Habari zaidi
Burudani