Namtetea Profesa Joseph Mbele
Namtetea Profesa Joseph Mbele
Niliona humu ukumbini ( JF) yametundikwa mawazo ya Profesa Mbele. “ Wengi Waanza Kuona Ubora Wa JK”. Yalikuwa ni maoni binafsi ya Profesa Mbele. Wengi wamechangia na wanaendelea kuchangia. Nami nitachangia pia. Nimepata bahati ya kukutana na kuongea na Profesa Mbele kwa simu na ana kwa ana . Ni pale aliporudi nyumbani Tanzania mwaka jana.
Naweza kusema nimemfahamu Profesa Mbele kupitia maandiko yake kwa maana ya makala zake anazozituma KWANZA JAMII na pia nilipoongea nae na kumsikia anavyoelezea mitazamo yake juu ya masuala mbali mbali ya nchi aliyozaliwa, Tanzania. Kwamba Profesa Mbele ni mtaalamu wa lugha ya Kiingereza haina maana hana anachokijua kuhusiana na nchi yake Tanzania na ulimwengu kwa ujumla.
Ni dhahiri kuna wanaotishika wanaposikia mtu anaitwa ‘ Profesa fulani’. Na kuna anayejisikia raha anaporudi nyumbani na kumwambia mumewe au mkewe; “ Kuna jamaa kule JF anaitwa Profesa Mbele, kaja na hoja zake za kipumbavu, nimempa maneno yake, mpuuzi mkubwa!”
Aliyempa Profesa Mbele ‘maneno yake’ huenda ana hitaji la kupunguza hasira zake, msongo wake wa mawazo. Kama hilo linamsaidia ni jambo la heri. Lakini bahati mbaya si wengi wako kama Profesa Mbele. Yeye atasoma na atalifahamu hilo, wala hutamwona akirudi na kujibu kwa hasira.
Ukikutana na Profesa Mbele huwezi kumsikia akitamka neno ‘Profesa’. Kwa Profesa Mbele ‘ sina hata ya kujisikia kuwa mimi ni sawa na ‘Mwalimu wa Zamu’ Shule ya Sekondari Changanyikeni. Profesa Mbele hana makuu. Ni mwalimu na bado ana kiu ya kujifunza. Anajiamini. Si mwanachama wa chama cha siasa hapa Tanzania. Anaipenda Tanzania na anajisikia huru kuchangia fikra zake. Hana sababu za kuficha jina lake. Na katika hilo, Profesa Mbele na mimi tuna mitazamo sawa. Binafsi sioni tatizo kuandika maoni yangu. Naandika kwa uhuru . Sina chama na sina sababu ya kuficha jina langu kwa fikra zangu ninazozitoa hadharani. Mwenye kuzipinga, ruksa, azipinge kwa hoja, ni muhimu. Na mengine niandikayo yaweza kuwa ya kipuuzi, najua, maana mimi si malaika. Kuna watakayekubaliana na hoja zangu, na kuna watakaosema; “ Sasa mshenzi huyu atakiona cha mtema kuni”. Watanishambulia mimi binafsi hata kwa matusi ya nguoni. Nimeshazoea. Ukichagua mchezo wa masumbwi, usiogope ngumi za usoni!
Tujitahidi kujenga mazoea ya kuikabili hoja inayowasilishwa na si kumkabili mwasilisha hoja. Mathalan, Profesa Mbele yeye kwa mtazamo wake anaona kuwa JK ameonyesha ubora kama kiongozi. Ni mtazamo wake. Wengine tuje na mitazamo yetu kwa kupinga au kuunga mkono hoja zake. Si busara kuanza kumvamia Profesa Mbele na kwa kutumia lugha zisizo za kiungwana . Na wanaofanya hivyo baadhi yao ni waoga kwa vile hawatumii hata majina yao halisi.
Daima tupiganie ‘ Neno huru’. Uhuru wa kila mmoja wetu kutoa maoni yake. Tujiadhari tusije tukatumia majukwaa haya kukandamiza fikra huru. Si kwa bastola na pingu, bali kwa kalamu zetu. Tujiulize; ni Maprofesa wangapi wa Kitanzania wanaojitokeza kwa majina yao kuchangia fikra zao katika majukwaa ya wazi ya kijamii?
Na kama asememavyo Profesa Mbele Mwenyewe; “ Kuona mazuri ya JK kama kiongozi, kwa upande wangu, si sawa na kuipigia debe CCM. Tangu CCM ianze, nimekuwa nikiishutumu kwa namna mbali mbali, tena kimaandishi, ili kila mtu asome. Nimechapisha hata kitabu, wiki chache zilizopita, ambamo nimeendelea kuishutumu CCM.
Tatizo la waTanzania wengi ni ufinyu wa mawazo. Kwa vile wamezama mno katika siasa za vyama, wanayachukulia masuala kwa mtazamo wa kichama. Ukisema hivi, wanaangalia unaunga mkono chama gani. Ukisema vile, wanaangalia kwa mtazamo wa chama fulani. Ukweli ni kuwa mimi si mwanachama wa chama chochote. Nina uhuru wa kusema chochote ninachofikiri, hata kama kinawaudhi watu wa chama fulani. Shauri lao na siasa zao za ufinyu na ukandamizaji wa fikra kwa maslahi ya chama.” Profesa Mbele.
Nawasilisha.
Maggid
‘ Mwalimu Wa Zamu’.
Tembelea: http://mjengwa.blogspot.com










Maggid nakubaliana na wewe,tunapaswa kuheshimu
mawazo ya wengine na hata pale tunapotofautiana nao
tuwajibu kwa namna ambayo haiwezi kuwakera.
Binafsi namuheshimu sana Profesa Mbele kutokana
na mawazo yake anayoyatoa katika blog mbalimbali na
katika gazeti letu la kwanza jamii na nitumie fursa
hii kumshukuru kwa jitihada zake za kutafuta maarifa
na kuyagawa kwa wengine.
Ndugu Maggid,
Awali niliposoma kichwa cha habari kuwa unamtetea Profesa Mbele nilidhani utakwenda moja kwa moja kwenye hoja iliyofanya baadhi ya wana-JF wapingane nae in the first place.Lakini kwa bahati mbaya,au makusudi,umeamua kukumbatia utamaduni wa kuangalia haiba ya mtu badala ya hoja husika.
Naomba pia kutokubaliana nawe katika hoja yako kuwa “tatizo la Watanzania wengi ni ufinyu wa mawazo”.Hivi una takwimu zozote za kusapoti hitimisho hilo?Ufinyu huo ni pale wanapokosolewa akina Profesa mbele pekee au kwenye kila suala?Hivi pale Jamii Forums,michango ya maana inayotolewa pale inawekwa na wageni au Watanzania hao “wengi wenye ufinyu wa mawazo”?Na pengine la muhimu zaidi,inakuwaje akina Mjengwa na Profesa Mbele ambao ni Watanzania wenzetu hawako kwenye kundi hilo la wenye ufinyu wa mawazo?
Unatetea uhuru wa Profesa Mbele kutoa mawazo yake halafu wakati huohuo unakwaza uhuru wa wasioafikiana na mtizamo wake.Naamini kabisa kuwa laiti Profesa Mbele angeungwa mkono usingekuja na hitimisho la “dharau” kuwa Watanzania wengi wana ufinyu wa mawazo.
Pengine kabla ya kukimbilia kumtetea “rafiki yako Profesa Mbele” ungefanya utafiti mdogo tu kwanini kumejitokeza upinzani kwenye hoja yake kuhusu JK.Kukurahishia,ukweli ni kwamba hoja yake sio tu unpopular bali ilikosa hoja za msingi zinazotarajiwa kutoka kwa mwanazuoni kama yeye.Pale JK kuna baadhi ya wana-forums wanaotoa hoja za ajabu kabisa lakini mara nyingi zinaishia kupuuzwa na wachache.Sababu ya kupuuzwa huko au kupingwa na wachache ni ukweli kuwa wana-forums hawajua uwezo wa akili na kiuchambuzi wa mwandishi husika.Ila kwa Profesa Mbele,sote tunafahamu kuwa ni mwanazuoni aliyebobea,na tuna matarajio makubwa kutoka kwake.
Wana-JF waliohoji usomi wa Profesa Mbele walikuwa na haki na uhuru wa kufanya hivyo kama ilivyokuwa kwa Profesa Mbele kutoa hoja yake hiyo unpopular.Tukienda mbele zaidi ya suala la haki na uhuru,ni dhahiri kuwa laiti hoja ya Profesa ingeendana na hali halisi basi kusingekuwa na ukosoaji uliojitokeza.
Na wakati unawakosoa wakosoaji wa Profesa Mbele unasahau kuwa Profesa nae ni mahiri wa kuwakosoa Watanzania wenzake kuhusu “uvivu wa kufikiri” au “ufinyu wa mawazo” (angalau wewe umesema “Watanzania wengi” badala ya kusema “Watanzania” ikimaanisha “wote”).Uhuru ni sawa na barabara yenye pande mbili: heshimu uhuru wangu,nami nimeshimu wako.
Mwisho,mnapoamua kuweka mawazo yenu hadharani msitarajie kuungwa mkono pekee.Hata kama mawazo yenu yangekuwa sahihi kila wakati bado kungewepo uwezekano wa baadhi ya wasomaji kutoafikiana nanyi.Ndio wanasayansi wa jamii wanachoita point of view.Atakayeafikiana nanyi atawaunga mkono na hata kuwapongeza,atakaetofautiana nanyi atawapinga au kuwakosoa.Hilo la kujadili mtu badala ya hoja si mwafaka lakini si la ajabu kwa vile hata waandishi mahiri kama wewe Mjengwa umeangukia kwenye mtego huohuo wa kuwashutumu watu (Watanzania wengi wenye ufinyu wa mawazo) badala ya kuangalia mantiki ya hoja zao.Na badala ya kuangalia kwanini “wenye ufinyu wa mawazo” wamempinga Porfesa mbele,mwenzetu unatuletea habari za haiba ya Profesa Mbele!
Mwenyekiti,
Inaelekea nawe una matatizo ya kulalia upande mmoja. Unazungumzia uhuru wa kila mtu kutoa maoni yake na wakati huo huo hutaki watu wamkosoe Profesa. Katika makala yake Profesa hakuweza kuainisha mazuri ya JK zaidi ya zira zake za kuitangaza Tanzania nje ya nchi. Kuna matatizo mengi ya msingi hapa nyumbani ambayo kama JK angeamua kuyavalia njuga, hakika hali ingekuwa bora zaidi kuliko ilivyo sasa ambapo longolongo ni nyingi kuliko vitendo. Nchi inaendeshwa kisiasa zaidi kuliko kitaalamu!
Unaungana na Profesa kuwa tatizo la waTanzania wengi ni “ufinyu wa mawazo”. Kauli hii kutoka kwa mwanafalsafa kama wewe inaonyesha wazi jinsi ambavyo umefilisika kimawazo hasa linapokuja suala la watu kuonyesha msimamo tofauti dhidi ya swahiba yako.
Unadai kuwa “Ukikutana na Profesa Mbele huwezi kumsikia akitamka neno ‘Profesa’.” Kwa taarifa yako nchini marekani ni nadra sana kusikia walimu wa vyuo ambao ni PhD holders na hata maProfesa kujiita kwa title zao hivyo haishangazi kwa Profesa Mbele kutojiita hivyo kwani ataonekana kituko. Huku mara nyingi watu huitwa kwa majina yao - vyeo havitumiki sana.
Mjengwa, hoja hujibiwa kwa hoja…hoja uliyokuja nayo kumtetea Profesa Mbele ni dhaifu mno.
Maggid,
Lazima utambue ya kuwa uhuru ambao umekuwezesha wewe na Profesa Mbele kuwalabel watanzania kama wavivu wa kufikiri, ndio uhuru huo huo uliowawezesha think tanks wa ukumbini (JF) kuita hoja za Profesa Mbele za kipumbavu. Mimi binafsi nimechukizwa sana na kauli za Prof Mbele za kumsifia JK. Haiingii akilini kabisa kwa Profesa kumjaji Rais kwa vigezo vya kusafiri nje na kupitisha kwa mswada wa uraia wa nchi mbili. Hii inaonyesha dhahiri ya kuwa Profesa mbele ni mbinafsi, na ameweka maslahi binafsi mbele.
Watu walitegemea Profesa angejenga sababu zenye ushawishi , na sio kusema tuu kama yuko kwenye kilabu. Ni kitu gani haswa ambacho KIKWETE amefanikisha mpaka sasa ?
Naniamewapa JF cheo cha “Think Tank”? Kwa hiyo kila kinahoongelewa huko JF mnafikiria kwa niaba yetu sio. Kama ni think tank nafikiri ni ya Chadema na si ya kila Mtanzania.
Sikatai nyie Chadema na JF yenu mna haki ya kupingana na mawazo ya Prof. Mbele lakini kwa mujibu wa hoja si matusi na kumbananga eti ni Prof uchwara awaachie nyie ulingo wa siasa. Nani amewaambia kuwa kwa kuwa nyie mnatoa mawazo yenu huko JF basi kila mtu lazima akubaliane na mawazo yenu? Wengine sisi huko JF hatuingii kabisa kwa sababu ya hiyo hiyo ya kujiona kuwa nyie mnajua kila kitu na ni wasomi kuliko wengine. Leteni hoja za hoja si kumtukana mtu kwa kutoa mawazo yake.
Kimsingi mimi nakubaliana na hoja alizotoa Prof. Mbele, Mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni.
Mwenyekiti
Hoja zangu zitaingiaje vichwani mwa watu wenye akili finyu, wasiojiamini, ambao hata kujitambulisha hawajitambulishi?
Ufinyu wa mawazo unajitokeza hapo watu wanapodhani kuwa kazi ya kujenga nchi ni ya rais, wanapokaa vijiweni na kungojea Kikwete afanikishe malengo ya Taifa. Ukiachilia mbali akina mama huko vijijini ambao wanafanya kazi sana, na baadhi ya watu mijini, mamilioni ya Watanzania wanakaa vijiweni wakisogoa badala ya kufanya kazi.
Watanzania wengi wanakaa vijiweni, kwenye baa, kwenye sherehe, badala ya kuwajibika kazini. Hata maofisi yameshakuwa vijiwe. Ni nchi gani inayoweza kusonga mbele na wananchi wa aina hiyo, hata kama kiongozi ni makini sana? Ufinyu wa mawazo ndio unawafanya watu wasione hilo, na badala yake wawe wanamshambulia rais. Jishambulieni pia nyinyi wenyewe.
Sasa pamoja na ufinyu huo, hao ndio wanaodai kuwa wataweza kushindana katika dunia hii wakishapata uraia wa nchi mbili. Mtashindana na nani kama ni waoga namna hiyo, msiojiamini? Mpewe hata uraia wa nchi kumi, mwone kama mtaiweza dunia hii inayohitaji elimu, maarifa na ujuzi.
Inafahamika wazi, na imefahamika kwa miaka mingi, kuwa waTanzania wanapata shida hata kujieleza. Lugha inawashinda, iwe ni ki-Swahili au ki-Ingereza. Vyuoni, inabidi mwalimu anapofundisha atumie maneno ya ki-Ingereza na kiSwahili, kwani lugha ya kufundishia, yaani ki-Ingereza, haifahamiki vizuri. Na bado watu mnaamini kuwa, pamoja na uzembe wote huu, mkipata uraia wa nchi mbili mtaweza kushindana ulimwenguni.
Huku Marekani, kuna nafasi za kufundisha ki-Swahili katika vyuo mbali mbali. Ajabu ni kuwa wa-Kenya ndio wengi wanaochukua nafasi hizo. Watanzania bado wako vijiweni, hawasikii la mtu.
Daima nimewaambia wa-Tanzania kuwa tujizatiti kielimu, na tujielimishe kweli. Na ninajaribu kutoa mchango wangu kwa upande huo. Sio siri, hata vitabu nimewawekea huko huko Tanzania. Lakini wa-Tanzania ndio hao, maneno na maringo yasiyo na maana. Shuleni wanatafuta dezo, na wengine wanaghushi vyeti. Wako wanaodhani watafanikiwa kwa kutumia ngozi za binadamu, viungo vya albino, bahati nasibu za makampuni ya simu au bia, uraia wa nchi mbili, na kadhalika.
Huku ni kujidanganya. Inabidi Watanzania mtambue kuwa leo kinachoongelewa ni uchumi unaoendeshwa na ujuzi, elimu, na maarifa. kwa kiIngereza wanaita “knowledge economy.” Tujitazititi kielimu. Bila kujizatiti namna hiyo, hata mkipata uraia wa nchi kumi haitawasaidia, kwani mtashindana na watu wa dunia yote waliojizatiti ipasavyo.
Nitakuja Tanzania mwaka huu kuendesha warsha, na ratiba mtaipata. Njooni tukutane, kama mnajiamini. Lakini vile vile, njooni tuelimishane, kama mnataka kujiandaa kweli kwa ushindani wa dunia hii ya utandawazi. Warsha moja imeshapangwa tayari. Itafanyika Arusha Community Center, tarehe 3 Julai, kuanzia saa 4 asubuhi.
Dr Mbele: mimi nathibitisha nitakuwapo. Ikiwa kuna wananet wanaisho DSM watataka kuja nami nina nafasi 3 kwenye gari yangu. Naomba tu Dr Makundi wa Roma na yeye aje kwenye warsha, na wewe nakuomba uruhus Q&A mwishoni.
Mukulu,
Taarifa tulizonazo ni kwamba unaponda UDUO kwa sababu huna sifa za kupata uraia wa Marekani. Utafiti tuliyofanya unaonyesha ukijaribu tu kuomba UDUO report zako zitaonekana na ukikataliwa ndiyo na green card inaota mabawa. Kwa maana nyingine itabidi urudi hapa uanze kubangaiza kama sisi. Kwa hiyo kupinga kwako UDUO siyo kwa dhati bali kwa vile wewe huna sifa za uraia wa Marekani umeona umharibie kila mtu!
Venance, usiwe na wasi wasi. Warsha zangu, ambazo nilianza kufanya mwaka juzi Arusha, halafu mwaka jana nikafanya Tanga na Dar es Salaam, zina muda mwingi sana wa masuali na majibu. Tunaongea na kujibizana hadi tunachoka, na ndipo tunaagana.
Kama uraia wa ugenini ni bora, si bora muombe huo uraia mpewe muishi maisha ya raha kwenye nchi za maziwa na asali? Kama ishu ni kuwekeza mbona wageni wanawekeza Tanzania na wanapata vivutio kibao bila ya kuwa raia wa Tanzania, nyinyi kinachowashinda kuwekeza Tanzania ni nini kama sio ukosefu wa mitaji?
Tusidanganyane hapa, watanzania wengi waliopo nje hawana mitaji ya kushindana na wageni, mfano mdogo ni jinsi wanavyolalamika kila siku kupanda kwa bei ya ardhi Tanzania, hawajui kuwa tangu serikali ilipotoa ruhusa kuuzwa kwa ardhi kama commodity bei yake imekuwa ikipaa kila siku kwa sababu wapo wanunuzi walio tayari kulipa hizo bei. Na ni wanunuzi wapangao bei na hawa ni watanzania wanaoishi Tanzania wakifanya biashara Tanzania na shughuli nyingine za kiuchumi. Nyie watanzania wageni kaeni huko kila siku mkiwaza nchi iko ’static’ kama mlivyoiacha, bado iko kwenye ‘ujamaa’ wakati sasa hivi ni ubepari kwa kwenda mbele, hakuna kiwanja cha bure, mwenye kuweza kuinvest peke yake haya, mwenye kushirikiana na wageni haya, na hata hamtaweza kufit kwenye middle class ya Tanzania.Matabakia kuilaumu serikali na kusubiri iwafanyie kila kitu.
Kuna siku Mihayo alitoa makala kuonyesha jinsi wageni wanavyopewa upendeleo kwenye uwekezaji, kuliko wazawa, na wengi wenu mlimuunga mkono, sasa na nyie mshakuwa wageni kinachowashinda kuwekeza ni nini? Au mko kama popo huko mliko uraia hamjapata, nyumbani uraia hamna?
Weka maoni yako hapa!
Maoni mapya
Zinatembelewa zaidi
Makala mpya
Habari zaidi
Burudani
Makala mpya
Zenye maoni mengi
Zinazotembelewa zaidi
Counter:347,180
Maintained by Daima Solutions | Log in | Entries (RSS) | Comments (RSS) |