Mungai Amvaa Pinda Suala La Uzee
Mbunge wa Mufindi, Joseph Mungai jana aliibua tena mjadala wa ukomo wa vipindi vya ubunge na viti maalum akieleza kuwa wanaozungumzia suala hilo, wanakwenda kinyume cha katiba inayokataza aina yoyote ya ubaguzi.
Mungai mmoja wa wabunge wenye umri mkubwa na muda mrefu katika bunge hilo, alitoa kauli hiyo juzi bungeni mjini Dodoma wakati akichangia azimio la bunge kuridhia itifaki ya jinsia na Maendeleo ya Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) ya mwaka 2008.
Hatua hiyo ya Mungai inaashiria kuwajibu wale wanaopendekeza kuwepo kwa ukomo wa vipindi vya ubunge, akiwemo aliyeibua mjadala huo, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda. Pinda alishauri ukomo wa ubunge uwe miaka 15.
Pinda aliibua mjadala huo, alipokuwa akizungumza na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari hivi karibuni jijini Dar es Salaam na kutaja mali zake.
“Yaliyo katika itifaki hii tayari yamo katika Katiba yetu na nina uhakika kabisa yamo kwa sababu nilikuwa mjumbe wa bunge maalum la Katiba lililopitisha Katiba hii, mwaka 1977, kazi tuliyoifanya kwa niaba ya wananchi wa Tanzania,” alisema Mungai.
Alifafanua katiba ya Tanzania inasisitiza haki na usawa jambo ambalo analipenda.
Akizungumza kwa mpangilio mzuri wa maneno Mungai alisema; “katika sehemu ya tatu ya katiba yetu inayohusu haki ya usawa, ninapenda kwa sababu jambo hili la usawa lipo pia katika mjadala unaoendelea hapa wa vipindi vya ubunge na vipindi vya viti maalum.
“Ninapenda katika kuunga mkono azimio hili tulipitishe, ninukuu vifungu muhimu kutoka kwenye katiba, Ibara ya 13 ya katiba yetu (2) inasema, ni marufuku kwa sheria yoyote iliyotungwa na mamlaka yoyote katika Jamhuri ya Muungano kuweka sharti lolote ambalo ni la ubaguzi ama dhahiri au wa taathira yake,” alisema Mungali akishangiliwa na wabunge wengine.
Kama hiyo, haitoshi Mungai alinukuu ibara ya nne ya katiba akisema kwamba ni marufuku kwa mtu nyoyote kubaguliwa.
Alifafanua kwamba kifungu hicho kina maana ya kwamba mwanamke ama mbunge yoyote aliyekaa vipindi viwili bungeni haruhusiwi kubaguliwa.
“Kwa madhumini ya ufafanuzi wa masharti ya ibara hii, neno kubagua maana yake ni kutimiza haja, haki au mahitaji mengineno kwa watu mbalimbali kuzingatia utaifa wao, kabila, pahala walipotokea, maoni yao kisiasa, rangi, dini, jinsi, hali yao ya maisha kwa maana inawezekana uzee,’ alisema.
Mbali na vifungu hivyo Mungai pia alinukuu Ibara ndogo ya 5 ya katiba ili kufafanua maana ya ubaguzi na kueleza kuwa hakuna sababu ya kupoteza muda kuzungumzia vipindi vya ukomo kwa wabunge wala wabunge wa viti maalum kwani kufanya hivyo ni kinyume cha katiba.
“Kwa marejeo ya Katiba, utakuta hakuna sababu yoyote ya kupoteza muda kuzungumzia vipindi vya ukomo kwa wabunge wala vipindi vya ukomo kwa wajumbe wa Bunge hili kutokana na Viti Maalum kwa sababu kufanya hivyo ni kinyume cha vifungu vya katiba nilivyovinukuu,” alisema Mungai.
(Chanzo: http://www.mwananchi.co.tz)










Weka maoni yako hapa!