Home » Featured, Habari, Headline

Abdul Mbashiri: Ni Nini Hasa Nia Ya Butiku Na Wenzake?

7 December 2009 1,193 views 19 Comments

Mbashiri said:

Mchomeko;

Ni nini hasa nia ya Butiku na wenzake?

Na Abdul Mbashiri wa Mbashiri

KWA watu walioshikilia madaraka, tena kwa miaka mingi, wakayatumia kama walivyopenda, wakitamba na hata kuonea watu lakini wakayapoteza madaraka hayo ghafla na wasijue jinsi ya kuyapata tena, siyo jambo la ajabu wala la kushangaza kusikia na kuona watu hao wakitapatapa kwa kauli zisizo za msingi dhidi ya utawala ulioko madarakani sasa.

Wakubwa hawa wanadai kuwa nchi inakwenda ovyo. Kwamba nchi imejaa rushwa (wenyewe wamepata neno jipya la ufisadi). Kwamba nchi imegawanyika vipande vipande. Kwamba inafaa kurudisha Azimio la Arusha. Kwamba nchi inaharibiwa na Mtandao. Kwamba Rais Jakaya Kikwete amezungukwa na “majizi”.

Hakuna namna bora zaidi ya kuzielezea kauli hizi zinazotolewa na watu ambao wamepata kuwa viongozi, tena wakubwa Serikalini, ila kusema kuwa kauli hizi ni kauli za hatari kwa uhai na usalama wa nchi, na kwa kweli ni ushahidi halisi za watu wanaotahayari baada ya kupoteza madaraka hata kama wanaendelea kuyasaka kwa udi na uvumba kwa njia nyingine.

Pamoja na uhatari wake, hizo ndizo baadhi ya kauli zilizotawala Mjadala wa Kongamano la Miaka 10 ya Kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, lililofanyika majuzi mjini Dar Es Salaam kwa kuandaliwa na Mfuko wa Mwalimu Nyerere (Nyerere Foundation).

Hakuna shaka, hata kidogo, kuwa kongamano hili lilikuwa zuri na muhimu kumuenzi Baba wa Taifa, kiongozi ambaye pamoja na kwamba utawala wake haukuwa kamilifu hasa katika maeneo kama ya uchumi na utawala bora, bado alikuwa na anabakia kuwa nguzo kuu la Taifa la Tanzania, na nyota iliyong’ara na inaendelea kung’ara katika Bara la Afrika.

Mwalimu Nyerere anabakia kiongozi ambaye amelijenga Taifa Huru la Tanzania, atabakia kiongozi mfano wa uadilifu, hasa wa mali. Waliomharibia wakati wa utawala wake na pengine wanaoendelea kuharibu jina lake kwa kulitumia vibaya jina hilo ni hawa akina Joseph Butiku, Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Mwalimu Nyerere - Nyerere Foundation na wenzake ndani na nje ya taasisi hiyo.

Hakuna njia mbaya zaidi ya kumuezi Mwalimu Nyerere kama wanavyofanya akina Butiku kwa kutumia jina la Mwalimu kama kichaka cha kuficha tamaa na laghai zao kwa wananchi na kuendeleza maslahi, mahitaji na matakwa yao binafsi.

Kuna mambo kadhaa yanayostahili kuwekwa wazi mapema ili kufuatilia vizuri makala hii na zile zitakazofuatia. La kwanza ni kujua shahaba kuu ya kuanzishwa kwa Nyerere Foundation. La pili kujiuliza ni kwa nini mashambulizi haya yanazushwa sasa hivi. La tatu ni kujiuliza mashambulizi hayo yanamlenga nani hasa - Serikali, nchi ama kiongozi wa vyote viwili na mwisho ni kujiuliza nini hasa nia ya akina Butiku na wenzake. Nini kinawasukuma kuwa katika mstari wa mbele kabisa kuushambulia uongozi wa sasa wa Tanzania.

Tuanze na la kwanza. Nyerere Foundation inazo shabaha kadhaa, lakini kubwa kuliko zote ni kwamba huu ni Mfuko ulioanzishwa kwa nia kuu ya kuendeleza yale makuu ambayo aliyaanzisha, akayasimamia na kuyaenzi Mwalimu wakati wa uhai wake wote, ndani ama nje ya madaraka ya uongozi.

Na moja kubwa katika hayo ni nia ya dhati, iliyoungwa mkono na vitendo vya dhahiri kabisa ni jitihada zake kubwa kujenga Taifa la Tanzania, kuleta Umoja wa Tanzania, na kuhakikisha kuwa nchi hii inaendelea kuwa na utulivu na amani katika eneo la dunia ambako mambo hayo mawili ni tunu kubwa.

Ni dhahiri kuwa kauli za akina Butiku zinavunja kabisa msingi huu mkubwa wa Mwalimu, na hivyo nia ya watoa kauli hizo, haiwezi kuwa wanalenga kumuenzi Mwalimu, bali ni kutumia jina lake vibaya tu, na kama kichocheo cha kuendeleza chuki na ajenda zao binafsi.

Mashambulizi haya ya wakubwa hawa yasiyoisha dhidi ya uongozi wa sasa hayalengi kujenga taifa lenye Umoja, bali yanajaribu kubomoa Umoja wa Taifa letu kwa kuwarubuni wananchi waamini kuwa uongozi wa sasa siyo makini na haustahili kuwa madarakani. Ni aina ya hatari ambayo tumeishuhudia ikiziingiza nchi nyingi za Afrika katika zahama kubwa.

Kauli hizi za uchochezi za akina Butiku, ikitokea zikasababisha vurugu, uvunjwaji wa amani na upotevu wa maisha na mali katika nchi, ni dhahiri kuwa katika dunia ya sasa, Butiku na wenzake wanahusika na kuwajibishwa moja kwa moja, siyo tu na vyombo vya Tanzania tu, bali hata vile vya kimataifa.

Mfano halisi ni jirani zetu wa Kenya ambako viongozi waliohusika na machafuko, mauaji na upoteza wa maisha na mali baada ya Uchaguzi Mkuu wa Desemba 2007, sasa wanahaha kujinasua katika ndoani ya Mahakama ya Kimataifa ya Uharifu (ICC) na mwendeshaji wa mashitaka ya Mahakama hiyo, Bwana Luis Moreno Ocampo.

Akina Butiku wanasahau hata sifa kuu za uongozi. Moja ya sifa kubwa ya kiongozi mzuri ni kujua nini la kusema na wakati gani. Kiongozi hawezi kuwa mropokaji, tena hadharani, juu ya mambo ambayo yangeweze kusemwa kwa busara zaidi kwa kuyaelekeza kwa wanaohusika moja kwa moja bila kutumia jukwaa la kisiasa. Na basi ni vyema mtu kuropoka ukijiaminisha kuwa mtu safi ambaye hana madoa makubwa na ya dhahiri kabisa katika uongozi.

Hoja ya pili na ya tatu hapo juu zinaweza kujibiwa kwa pamoja na kwa maelezo mafupi. Mashambulizi haya yanazuka sasa kwa sababu wenye kuyaendesha wanahisi kuwa baada ya kuwa wamejaribu na kushindwa huko nyuma, sasa ndiyo wakati mwafaka wakati nchi inajiandaa kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa mwakani.

Na kwa kweli hii ndiyo nafsi yao ya mwisho kujaribu kuwashawishi wananchi kwa propaganda zao dhaifu na zisizo kweli. Wanaamini kuwa propaganda hizo zikifanikiwa wanaweza kujaribu tena kumpamba na kumwingiza mgombea wao katika kinyanganyiro cha uchaguzi mkuu wa mwakani.

Tatu ni kwamba mashambulizi ya sasa, hata kama waendeshaji mashambulizi hayo wanajificha vipi, yanamlenga moja kwa moja kiongozi wa sasa wa Serikali na taifa la Tanzania, yaani Rais Jakaya Mrisho Kikwete. Haya siyo aina ya mashambulizi yanayomlenga mtu mwingine yoyote wa chini ya Rais.

Mwisho ni kwa nini akina Butiku wanamlenga Rais Kikwete? Nini nia ya akiba Butiku na wenzake? Nini kinasukuma wazee hawa kumshambulia kijana ambaye walimlea wenyewe katika uongozi, kwa miaka mingi.

Kubwa la kwanza ni kwamba tokea mwanzo, kundi hili la wazee halikumtaka Jakaya Mrisho Kikwete kuwa Rais wa Tanzania. Na wala halijapata kumkubali ama hata kumsamehe Kiongozi huyo kwa kuweza kuwashinda wakati wa mchakato wa kuwania uongozi mwaka 2005.

Na ndiyo maana zinajegwa hoja zinazodiriki kuhoji hata ni kwa namna gani aliingia madarakani, wakisahau kuwa ni wananchi wenyewe wa Tanzania katika hatua mbali mbali waliomwingiza Rais Kikwete madarakani, tena kwa kumwuunga mkono kwa wingi wa kushangaza sana.

Na siyo tu kwamba aliwashinda kuweza kuingia madarakani. Lakini pia wanahisi kuwa kuwapo kwake madarakani kunafunga milango ya maslahi na matakwa yao kuweza kutumikiwa vizuri na utawala wake. Kwa namna nyingine pia wana hofu kuwa udhaifu wao na uongozi na uchafu wa baadhi yao walipokuwa madarakani unaweza kuanikwa hadharani.

Hivyo, wanatumia janja tu ya jukwaa la kumuenzi Mwalimu Nyerere kujitafutia umaarufu binafsi na kutaka waenziwe wao. Na wako tayari kulifanya hili kwa gharama zote zote ikiwa ni pamoja na kutumia siri za vikao

Ni sababu hiyo ya msingi ambayo siku zote imewasukuma viongozi hao kuushambulia moja kwa moja uongozi wake. Wamekuwa wanashindwa kumshambulia yeye moja kwa moja kwa jina na cheto chake kwa sababu wanaogopa hasira ya wananchi, lakini baada ya mashambulizi ya Kongamano la majuzi ni dhahiri kuwa sasa wanajiandaa kuianza kazi hiyo kwa ari mpya, nguvu mpya na kasi mpya. Na wala wananchi wasije kushangazwa na hili.

(Makala hii itaendelea)

19 Comments »

  • CNBM said:

    Kwani wazee wameongea kipi ambacho watu hawakijui? Wametoa maoni yao na ni wazi watatanzania wnegi hawariziki na utendaji wa serikali..tusianze kutishana

  • Kaka Trio said:

    Mwanindishi amejitahidi kiasi chake kuchambua na kuhoji uhalali wa akina Butiku kutoa maoni. Kwa upande wangu sioni ubaya wowote kwa kina Bitiku na wenzake ambao hawakutajwa kutoa maoni aidha kwa kupitia Mwl Nyerere foundation au njia zingine.

    Akina Butiku na wenzie wana haki kama ile aliyonayo mwandishi wa makala hii kutoa maoni yao kadri wanavyoona inawezesha kuendeleza taifa letu. Kama Butiku na wenzake wameona hio ndio njia ya kutoa maoni yao basi na waachwe watoe.

    ni ukweli usiopingika kwamba kila serikali popote duniani inatenda mabaya na mazuri ktk muda wa utawala wao. Kuna mambo mema serikali ya mwl na akina Butiku waliyatenda na kuna mabaya pia yalitendeka kwa bahati mbaya au kwa makusudi. Ktk serikali ya Kikwete pia kuna mema yanatendeka na kuna mabaya yanatendeka vile vile. Kwa yale yaliyo mabaya hakuna ubaya wowote yakikemewa na Butiku na wenzake au na mwananchi mwengine. Kwani ni siri kuwa hakuna ufisadi umetokea? kwa hata Kikwete halijui hilo? kwani hakuna watu wamefikishwa mahakamani na kesi bado zinaendelea? kwani kulikuwa haku skandali ya Richmond? kama ni jibu ni ndiyo, sasa kuna ubaya gani Butiku na wenzake wakisema akisema mambo yanakwenda mrama kwenye Tanzania yetu? au tuseme watu waliokwishafanya kazi ktk serikali za awamu zilizopita hawana haki ya kuchangia mistakabali mbali mbali ktk taifa la Tanzania?.

    Cha msingi mie naona si kumlaumu Butiko au mtu yeoyote anayejaribu kukemea au kunyoosha kidole kwa kibaya au kizuri kinafanyika nchini, kila Mtanzania ana haki ya kuchangia maendeleo ya aina zote nchini, bila shaka Kikwete pia hapendi watu wampake mafuta kwa mgongo wa chupa, nadhani Kikwete anafurahi sana anapoona wananchi wa kawaida na wale waliowahi kuwa viongozi wanajishirikisha ktk mijadala mbali mbali inayohusu nchi yetu kwani anajua wanaitakia nchi mema pia anajua wanamchangamsha pale ambapo labda anakuwa kwa kiasi fulani hajafuatilia jambo fulani ipaswavyo.

  • bwenge said:

    Ninaomba kutofautiana kidogo na Bw Mbashiri wa Mbashiri. Hakuna watu muafaka wa kuona uchafu wa jikoni zaidi ya wale waliowahi kuwa wapishi. Inawezekana kabisa kuwa akina Butiku (wakati wakiwa jikoni) walitumia madaraka yao vibaya (hatuna ushahidi). Lakini ni nafasi hiyo hiyo waliyowahi kuwa nayo inayowawezesha kuona vizuri jinsi waliowarithi wanavyotumia vibaya madaraka. Na tutakuwa wajinga wa mwisho kukubali kwamba kwa vile akina Butiku walitumia vibaya madaraka, basi hawana uhalali wa kukemea watawala wa sasa pindi wanapoona ‘uchafu ule ule’ waliokuwa wakifanya . Kama kweli wewe ni mtu unayependa kuona maisha bora kwa kila mtanzania kwa dhati na sio kwa chati, basi watu aina ya akina Butiku ni hazina, ni waungwana (pengine ndio njia mojawapo ya kutubu mbele ya umma, na kwa hiyo kutubu kwao ni faida kwetu). Kwa mfano, kama mimi ningekuwa Rais JK (nikiamini kuwa anaposema maisha bora kwa kila mtanzania anasema kwa dhati - kama kaulimbiu hiyo bado iko hai, sijui!), ningemteua Mhe Rais Mstaafu, William Mkapa kuzungungukia nchi nzima akilaani ufisadi. Ndugu Mbashiri wa Mbashiri, ufisadi upo kweli unatafuna nchi na kama hauko upande wa mafisadi, ninaamini utaunga jitihada yo yote ile ya kulaani ufisadi(iwe inafanywa na waliowahi kushika madaraka au la).

  • Kuku said:

    Wewe umekuwa very one sided. Pamoja na ukweli kuwa wale waliomshambulia raisi waliwahi kwa nyakati tofauti kuwa viongozi bila mafanikio, bado walichozungumza nui ukweli. Kikwete ni kiongozi dhaifu anaeendeshwa na mafisadi haijalishi nani anasema hayo bado ni ukweli mtupu. Ama unajipendekeza kwa raisi au hujui mantiki ya kiuongozi. Nchi imeharibika kila kitu kinayumba. Kikwete, makamu wake pamoja na waziri mkuu wote ni viongozi dhaifu wasioweza kuwakabili watu kama Lowassa. Nchi hii itaendelea kuporomoka mpaka atakapokuja kiongozi kamili 2015. Wakati mwingine nasema ni afadhali Lowasa angekuwa raisi maana angeiba bna kuendesha nchi vizuri kama Mkapa alivyofanya. Huyu jamaa hafanyi lolote la maana.

  • K. L. M said:

    Ndugu mwandishi wa Makala hii, umeongea hukuelimisha.

    \rudia yale mabango makubwa kunako barabara za nchi hii. “Rais Tunaimani kubwa na wewe”

    Je! IMANI bado unayo ?

    Ukianza ubaguzi, ni sawa na kula nyama ya mtu, hii mitandao ni ubaguzi na sasa ndiyo inatafuna nchi.

    Kikwete asimame kama Rais akemee na aadhibu wote wanaofanya uzembe.

    MZAZI HATAKIWI KUMNYIMA MTOTO FIMBO

  • Anonymous said:

    Hakuna ubaya kwa Akina Butiku kukosoa Utawala wa Jakaya Kikwete lakini mbona kipindi cha Mkapa hawakuwa na mikongamano ya namna hiyo?Na kama wana nia njema na serikali ya Kikwete kwa nini wajadili mapungufu tu?Hivi hakuna hata jema moja amelifanya kikwete?
    Ilikuwa katika kongamano hilo waelezee hata mafanikio fulani yaliyofanyika katika serikali ya kikwete,wangesema pamoja na mafanikio fulani lakini bado kuna mapungufu haya yarekebishwe!
    Mie kwa mtazamao wangu tayari naichukilia hii taasisi ya Mwalimu Nyerere ni kama chama cha siasa!
    Ni vyema hao akina Butiku na genge lake waanzishe chama chao cha siasa badala ya kutumia mgongo wa taasisi ya Mwalimu Nyerere kuleta upinzani wao wa kisiasa!
    Kama mtu alipigwa chini kupitia CCM na wanamtaka awe Rais ni bora wamtafutie chama agombee urais kuliko kubweteka na kuleta siasa za kijinga!

  • isack Elias said:

    Unashangaa nini ? nchi inakwenda kubaya wewe washangaa wanaosema kiasa waliwahi kuwa katika uongozi wa nchi hii. Walimnyamazia mda mrefu wamemchoka.

    Unataka kutuambia Tz mambo ni mazuri? Rushwa haipo? Umaskini umekwisha? Kagoda imeshashughulikiwa?

    Ni ajabu nasema ni ajabu kuutetea utawala wa Jk na ccm, ufisadi umetamalaki. una uwezo wa kuandika ukweli wanyonge tuujue ila unabaki kutumia kalamu ya yako kutetea watawala waliokosa nidhamu mbele ya umma.

    Nadhani wewe ni msomi wa kiwango fulani, nakuhsauri tumia kalamu yako kutetea wananchi badala ya watawala wasiojali wananchi

  • dsm said:

    Abdul, unaonekana una ushabiki, hutaki kuzungumzia hoja ya msingi, toa nafasi kwa akili yako kudigest mambo, usifuate ushabiki. Mtanzania yeyote asiye mwanachama wa chama chochote kile anaona mambo yalivyo, ni aibu kwako kujidai kipofu, watoto na wajukuu wako watakuja kukulaumu kuwa ulitoa michango mibovu katika mambo mambo makubwa kama haya yanayohitaji kujadiliwa kwa kina kwa ajili ya mstakabali wa taifa na vizazi jijavyo.

    hakuna kitu ambacho hakifahamiki, hata wenye uelewa mdogo wanaona mambo yanavyoenda kombo.

  • dsm said:

    Tatizo ni fikra za watu wengi haziko tayari kukosolewa, na ili uwe na utawala bora mojawapo ya nguzo mhimu ni kukubali kukosolewa ili ujipime kwa kupata maoni kwa watu wa nje. Huwezi ukawa unatoka wewe na familia yako unasema mimi ni baba mzuri, haiwezekani hiyo lazima isemwe na watu wanakuzunguka kwa kuwa ndio kipimo mhimu kwako, na si wale unaowapa chakula kila siku lazima watakupa ushauri zaifu wenye lengo la kukufurahisha bila kujali hali halisi ilivyo.

    Napenda kuwafahamisha wale wote wanaowapinga akina butiku kuwa wanakosa hekima. Pengine mawazo yao yangechukuliwa kama changamoto na kufanyiwa kazi kwa ustawi wa taifa. Nani hajui kuwa Serikali ya sasa ni ya kishikaji, niya kirafiki na kufahamiana? Ni vizuri kuweka marafiki unaowaamini kuwa watafanya yaliyopangwa lakini ukiona wanaharibu utafanyaje?

    Ifikie mahali taasisi ya urais lazima iheshimiwe pasiwepo watu wanafikiri kuwa wao ni milki wa nchi hii. Tanzania niya watanzania wote, na wanauhuru wa kusema ili hali hawavunji sheria.

  • Bi MKORA said:

    Hawa Kina Butiku na hiyo Taasisi yao ya Nyerere Foundation ni watafutaji tu kama watafutaji wengine, ukizingatia enzi ya Mwalimu walibanwa na hawakuwa na nafasi ya kuchuma, sasa hivi wanachuma kwa kupitia mgongo wa Mafisadi. Hivi tujiulize wanapata wapi mapesa yote hayo ya kuandaa makongamano wakati siku za nyuma Taasisi hiyo ilikuwa ina ukata? Chanzo chao cha pesa ni nani na nini? Hapo ndio unaeza kupata majibu kamili.

    CHA KUSHANGAZA KUANZIA HIYO TAASISI NA VYOMBO VYOTE VYA HABARI, VILIKUWA WAPI WAKATI MIZIZI YA UFISADI ILIPOKUWA INAJENGWA?

    Mwalimu Nyerere alimtukana sana Rais Ali Hassan Mwinyi kuwa anafanya biashara IKULU na anafuata ushauri wa mkewe, IKULU SI MAHALI PA KUFANYA BIASHARA, na akatuambia kuwa Raisi Benjamin Mkapa ni MSAFI, je kilichotokea ni nini? Hebu tupeni ushahidi wa biashara aliyoifanya Ali Mwinyi ili tuzilinganishe na BIASHARA alizofanya Benjamin Mkapa na familia yake, pamoja na kuajiri ndugu kibao IKULU ambao wengine mpaka leo bado wanafanya kazi.

    Kuna ya Mabenki (EPA), kuna ya madini (Bulyankulu na Kiwira)kuna mikataba, kuna mauaji ya Pemba, na mengi mengineyo, MBONA HATUISIKII HII TAASISI IKIKEMEA HAYA wakati yanatendeka, na hata sasa hatuwasikii wakisema kuwa Benjamin Mkapa alifanya makosa? Juzi juzi alienda Makerere kupokea shahada yake lakini aliwakimbia waandishi wa habari, alijua waandishi wa Uganda hawana mchezo wala mzaha, wala hawajagubikwa na pazia la Propaganda, wangemgrill mpaka asijue cha kujibu.

    Ninachoona kutoka kw Taasisi hii kwa kuwa Benjamin Mkapa alikuwa chagua la Mwalimu Nyerere kwa hiyo kwa kiasi kikubwa Taasisi hii imenufaika na UFISADI uliofanyika kipindi cha Mkapa na sasa inajaribu kuwaziba wati macho na kumkalia kooni kwa propaganda JK ili Mkapa asiwajibishwe.

    Ama mnataka tuseme kuna kaharufu ka udini au tusemeje, maana haya yanayomkuta JK sasa yalimkuta pia Ali Hassan Mwinyi ingawa wakemeaji wakati huo hawakuwa na ushahidi lakini walitumia nguvu zote kumpaka matope, na sasa apakwa matope JK ili ionekane kuwa si msafi. Alipokuwa akifanya ufisadi Mkapa alikuwa akipambwa na SIFA KUBWA KUBWA za UWAZI NA UKWELI! Haya twambieni ni uwazi na ukweli gani huo??

    TUmeshachoka na propaganda zenu, subirini Uchaguzi tutamchagua huyo huyo JK amalize miaka yake mitano maana sie tunayaona yake ni bora kuliko ya MKAPA anayeendelea kuimbiwa nyimbo za kusifiwa kwa sababu tu baadhi ya watu fulani walinufaika na Utawala wake na sasa hawayapati hayo manufaa tena.

  • Mswahili said:

    Tatizo sio tatizo lenyewe bali jinsi ambavyo mtu anavyoliona hilo tatizo ndio tatizo. Kwa kifupi naweza kusema ni mtazamo wetu ndio tatizo.

    Kwanza niseme hiyo TAASISI ya Nyerere Foundation imejaa wanafiki, na unafiki mkubwa sijapata kuona. Kwa sababu kiongozi au viongozi katika nchi wanatokana na wananchi wenyewe, wanakuwa constructed na social condition zilizopo, ambazo mojawapo naweza kusema ni malezi na makuzi. Haiyumkini Tanzania kumpata kiongozi mwenye socio condition za kizungu, kuanzia perfomance mpaka mambo mengine wakati mfumo wetu wa maisha ni tofauti na wazungu.

    Kwa kifupi ninachotaka kusema, ni kuwa kiongozi yeyote aliye sasa na atakayekuja chaguliwa baadae ni reflection ya tabia, maadili, malezi na makuzi yetu kwa sababu anatokana na sisi kwenye jamii zetu. Kama tunataka Kiongozi aliye tofauti na sisi (if we aspire for new leadership) basi itabidi sie wenyewe tubadilike, tuwe tofauti na tulivyo sasa.

    Wala tusilete uongo wetu tuliozoea wa kulaumu, maana hii ni tabia yetu kuu ya kupenda kutoa lawama kila wakati. Sisi muda wote hatujioni bali huwa tunatafuta scapegoat wa kumtupia lawama kutokana na matendo yetu. Nianze kidogo na hili la Ufisadi, au rushwa kwa maana nyingine, hivi kweli kuna mtu anaweza kujipa rushwa mwenyewe? Its take two to tangle, na rushwa imekuwa suala la kawaida kabisa katika jamii yetu ni kama vile sehemu ya utamaduni wetu. Mfano mdogo tu utamuona mtu anaondoka nyumbani bila leseni ya udereva, ana forge insurance, au gari yake ina makosa kibao. Huyu mtu akisimamishwa na polisi akaelezwa makosa yake, basi haraka haraka anaingiza mkono mfukoni anatoa shiling 5,000/ au 10,000/ kumpa trafiki polisi ili asimfikishe kunakohusika au asilipe faini. Hapo hakuna cha kupewa tiketi wala nini ni kumalizana hapo kwa hapo. Na hapo akitoka ataenda kujisifia kwa wenzake jinsi alivyotoa rushwa.

    Tuje kwenye biashara, hali ni mbaya kabisa, wafanyabiashara wanawahonga wafanyakazi wa TRA ili wasilipe kodi halali ili wapate super profit. Kwenye nafasi za kazi sio cheti chako kitakachokupatia kazi bali ni nani unamjua ndio kigezo chako cha kupata kazi tena kwa vyetu feki!

    Maofisini ndio kumeoza kabisa, wafanyakazi wa serikali wamekuwa miungu watu hasa wale watoao huduma muhimu kwa wananchi, usipomwamkia ukampa kitu kidogo basi hupatu huduma unayostahili, kuanzia mahakama, ofisi za ardhi, uhamiaji na kwingineko watu wanaomba rushwa bila hata woga wala haya. Mbali na kuomba rushwa, kuna wizi mkubwa wa kalamu unaendelea kwa kisingizio kuwa kila mtu anakula sehemu yake ya kazi, watu wanafoji risiti mbali mbali ili walipwe. Mbali na huo wizi wa kalamu, WIZI MKUBWA NI WA MUDA WA KAZI, watu wanatumia muda mwingi kufanya mambo yao kuchat kwenye internet, na upuuzi kibao badala ya kufanya kazi, matokeo yake majarada yanalundikana inabidi Jumamosi na Jumapili waende wakafanye overtime yaani wanalipwa ziada kwa wizi wao.

    Tukirudi kwa wasomi, hawa ndio wenye kuchonga sana na kujitia wakosoaji wakubwa lakini hakuna cha maana walichokifanya. Hebu niambieni tangu tumepata uhuru, hatuna wanasayansi nchini mwetu waliosoma mambo mbali mbali ya kisayansi, mbona sijasikia ugunduzi wowote ambao umeweza kutusaidi japo kutengeneza dawa zetu wenyewe za malaria na kukabilina na maradhi mengine nchini mwetu kutoka kwenye sayansi ya tiba?

    Achilia mbali sayansi nyingine na teknolojia, kila siku sisi tunaagiza kutoka nje. Je wanasayansi ya kilimo wamewezaje kumkomboa mkulima masikini angalau tukapunguza nusu ya wakulima waishio chini ya kiwango katika nchi yetu. Hata hao wasayansi ya jamii hatuoni kinachofanyika cha kuleta mabadiliko katika jamii.

    HAWA WAO kwao kubwa nimakongamano, masemina yasiyo na kichwa wala miguu ili mradi wapate posho (allowances).

    Na walioko vyuoni ndio usiseme, hao madokta na maprofesa, kubwa wao ni kuwasadia wageni kufanya utafiti, ili wapate malipo katika hizo tafiti. Na hata tafiti zao bianfsi wanazofanya hatuoni mrejesho wa hizo tafiti na jinsi zinazoweza kutusaidia kuondokana na umasikini ujinga na maradhi. Mwishoni kabisa wakishafikisha umri mkubwa ambao hawawezi tena kushiriki katika utafiti wanakimbilia kwenye siasa ili wakale kwa mgongo wa ubunge na uwaziri, maana huko kuna mamishahara kibao.

    Mwisho ni kwa wasomi walio nje, na wengineo wote mnaoishi nje na kula mkate kwa siagi, je ni kitu mnafanya au mmefanya kwa ajili ya nchi yenu zaidi ya kulaumu??? Hebu anzeni kuleta mabadiliko japo kwenye vijiji vyenu mlikotoka bila kulaumu, halafu muone jinsi mabadiliko yatakavyosambaa nchi nzima, maana haba na haba hujaza kibaba.

    Tumekaa tunapoteza muda bure kwa kunyoosheana kidole na kulaumu, wakati tukimnyooshea kidole kimoja JK vidole vilivyobaki vinatuelekea sisi. Hiyo ni law of nature, haikwepeki. Sisi ni wa kulaumiwa zaidi kwa matendo yetu!!

  • sds said:

    Bi mkora, unayosema, sawa, lakini tafuta source ya EPA ni nini? baada ya kupata jibu nafikiri huwezi kumlaumu BEN, amefanya mengi mazuri pamoja na mapungufu hayo yaliyojitokeza, lakini ebu rudi nyumbani kwako, umefanikiwa kiasi gani kuondoa kasoro zilizoko? ukipewa na ushauri na jamaa aliyekuwa mme wa mkeo utauchua au utauacha? maana anaweza kuwa na uzoefu na mke unayetaka kumuoa!

    Tuangalie mstakabali wa taifa tuache ushabiki jamani utatuharibia, tuepushe ndg yetu asingeakafika sehemu ambayo tunauwezo wa kumuepusha asifike huko. better to provide contructive and sound ideas for the betterment of next generation hata kama sisi tumekata tamaa.

  • Kibanda said:

    huyu muandishi anachekesha!

    hujui kuna uhuru wa kutoa maoni.
    uzuri wa maneno ya mtu ni kwmba huyalipii kodi - kama hutahatarisha usalama wa taifa hakuna wa kukuambia nyamaza.

    waaaaaaaaachi wazee watoe duku duku zao.

    nchi ambayo hairuhusu kutoa duku duku ni hatari sana.

    angalia somalia,iraq,iran,morococco n.k

    usikema ni lupango tuuuuuuuuuuuuuuuuuuuuuuuu
    ndio maana wanainzi wa nchi hizo wamekata tamaa na kuamua kularuana…kwa vita!

    demokrasi au domo krasia inaruhusu uhuru wa kupwayuka tena kwa saaaaaaannnnnnnnaaaa kama huchafui HEWA!

  • alimambo said:

    Inasikitika Taifa linakoelekea,nilawama juu ya utawala huu wa Rais Kikwete.Rais amekuwa ni mtu makini na akilitizama Taifa kwa jicho la huruma-wapo wanojaribu kumchokonoa ili kupata undani wake kwakuwa hawajui anacheza ngoma gani.Mkimlazimisha hatosia kutumia madaraka yake,kwani fahamu yakuwa Rais ana mamlaka namaamuzi mazito ktk mustakbali wa nchi.Mkiwa mnatapata tapa kwakutaka huruma au ujasiri wake pindipo dola ikifanya kazi yake asilaumiwe mtu.Mzee Butiku,Mzee Salim A.Salim kubalini kuwa kwenu jua limekuchwa na Bw.Mangula elewa madaraka hayakutolewa kwakujuana kama unavyodai bali kutokana na utendaji wa mtu ndiyo maaana akakabidhiwa zamana.
    Ni kweli hakuna mkamilifu na Rais pia nimtu alifanya baadhi yamakosa ktk uteuzi lakini hilo lisharekebishwa Je!Mheshimiwa Waziri Mkuu amechaguliwa kwa urafiki au kulipa fadhila,au mheshimiwa Katibu Mkuu wa CCM-Mheshimiwa Yusuf Makamba si ndio yeye alokuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar-jiji lilojaa kila aina ya harakati lakini aliweza kulidhibiti vilivyo hadi likaitwa Jiji la Makamba.Vipi Rais anahitaji shule gani kuelezwa juu ya uongozi thabiti namakini wa Mheshimiwa Makamba kubali yakuwa Mheshimiwa Mangula wewe ni muathirika wa mabadiliko ya siasa hapa nchini-naomba kaa pembeni kwani yatakapoanikwa mabaya yalopita msije mkatafuta pa kujificha.Kwa taarifa yenu mengi ya ufisadi yamejiri ktk uongozi wa serikali ya Tatu-sasa msimpige Rais kwa bakora yake mwenyewe.Eleweni maumivu yakimzidi hatotizama nani alikuwa nani kwangu na wengi waathirika mtakuwa ni nyinyi vinara wakukemea ufisadi-sikweli Rais ni dhaifu bali yupo makini ila kwakujua nguvu alonayo anaogopea kulitumbukiza Taifa katika hatari kubwa.Amekabidhiwa nchi ikiwa ya amani na utulivu bali si umoja kwani Taifa linatabaka zake tangu hapo awali bali tumejaaliwa masikilizano.Mungu Ibariki Afrika,Mungu Ibariki Tanzania na Mungu Mbariki Rais wetu Jakaya Mrisho Kikwete atufikishie Taifa letu ktk hatma njema ya upendo na amani,nakunyanyua hali zetu za maisha”Aamin”.

  • Mgayamlongo said:

    Kila jambo lina msukumo wake, na kwa kweli kwa hawa waliokuwa katika nafasi za juu za Uongozi wa Nchi katika kipindi kilichopita cha Uongozi wa Nchi hii,wanapozungumza wanavuta hisia za watu wengi.
    Lakini pia kuna haja ya kutafakari kwa undani na kuyarejea matukio ya nyuma piaili kujaribu kubaini msukumo wa watu hawa. Wakati wa Uongozi wa Mzee Mwinyi tuliyasikia mengi dhidi ya Uongozi wake, lakini alipoingia Mkapa madarakani kelele zilipungua sana, sasa zimerejea tena wakati wa uongozi wa Kikwete. Kulikoni?
    Nadhani ni muhimu Rais akapewa muda wa kufanya kazi badala ya kumfuata kwa bughudha za kila siku. Hii haiondoi uhuru wa kujieleza wa Wananchi. Hivi Butiku anaposema hayo,ina maana hakumbuki ukabila na ufisadi uliojikita katika kipindi chao cha Uongozi? Mpeni nafasi na raha JK afanye kazi, husuda na bughudha zenu hazitowasaidia kina Butiku na wala hazitoisaidia nchi yetu.

  • LUDOVICK JOSEPH said:

    Mwandish amethibitisha maneno ya butiku kuwa wanamtandao wakiwa chini ya kikwete wako tayari hata kuuza nchi ili wawe madarakani.yaani wanabeza mfuko wa mwalimu nyerere na wanabeza hata na baba wa wa taifa.kwakuwa aliyosemayanahatarishakikwete, basi usishangae siku watakaposema kuwa nyerere alipowakataa alikuwa na chuki binafsi. umeelewa au bado

  • mdau said:

    nafurahi kuona kama watanzania tunafikia mahala tujadili mambo ya maana kama haya.
    nikirudi kwenye mjadala huyu Bukuku na wenzake naona ni chuki tu na wivu wa madaraka,madaraka matam sasa unapoyakosa wkt bado huna hamu nayo matokeo yake ndio unaongea kama wanavyoongea hao watu,si suala la kukataa kwamba kikwete na uongozi yake unamapungufu mengi kama ulivyokua kwa maraisi waliomtangulia akiwemo nyerere,so kama tunaitakia mema tanzania ni vizuri kukosoa pale panapohitajika kukosolewa na kupongeza pale panapostahili kupongezwa.lakini hawa kina bukuku wao wanchoona ni mapungufu tu ya rais wetu lakini mazuri yake hawazungumzii,wanachojaribu kukifanya kinaweza kuwajengea chuki watanzania wenyewe kwa wenyewe kitu ambacho hatuoombi kitokee maana mifano tunaiona sudan,rwanda,drc.
    mungu mbariki raisi wetu mungu ibariki tanzania

  • Sabath said:

    Butiku?!!! Huyu jamaa ni nani kama sio kubebwa kupitia undugu, upendeleo, ukabila, udini na urafiki. Analalama kama vile nchi inaelekea motoni. Yeye uchungu aliokuwa nao ni wa wajukuu zake tu, si kwa watanzania wote. Wamekosa madaraka sasa analalama kwa vile ufalme wao hauko tena na muda si mrefu watasahauliwa. Waliizamisha nchi wanajifanya kama vile tumesahau. Nakama longolongo lolote likiikumba TZ wajue kuwa wao ndio wa kwanza kuathirika kwani hatutokubali wao kutuletea machavuzi kwa husda zao za mioyo mibaya kwa kutumia kichaka cha mwalimu na udini (padri) naye ashirikishwa katika hizo propaganda.

  • ibrahim Hussein said:

    Tuwaulize Mwalim Nyerere Foundation wamefanya nini miaka kumi ya kifo cha Nyerere zaidi ya kuwa upande wa Salim kaitika kugombea Urais?hakuna walichofanya sasa zimebaki chuki tu.Hakuna kitu kibaya ambacho walifanya kama kumuunga mkono Salim kwenye urais,wao walitakiwa kuwa NEUTRAL hata wakitoa maoni yao watu wangejua kwamba wanachoongea ni cha kweli si chuki kama inavyoonekana sasa,Wale wote walioongea pale kwa namna moja ama nyingine wana chuki na KIKWETE,kosa la kumuunga mkono SALIM limeharibu taasisi.Wamebaki majungu wafanye kitu ambacho kweli watanzania wakione kweli kile wanachokifanya kinafanana na mwali

Weka maoni yako hapa!

Add your comment below, or trackback from your own site. You can also subscribe to these comments via RSS.

Be nice. Keep it clean. Stay on topic. No spam.

You can use these tags:
<a href="" title=""> <abbr title=""> <acronym title=""> <b> <blockquote cite=""> <cite> <code> <del datetime=""> <em> <i> <q cite=""> <strike> <strong>

This is a Gravatar-enabled weblog. To get your own globally-recognized-avatar, please register at Gravatar.